Wednesday 7 August 2013

TANZANIA YASHAURIWA KUANZISHA KAMPUNI MAALUM ITAKAYOSHUGHULIKIA MAENDELEO YA CHANZO CHA UMEME CHA JOTOARDHI(GEOTHERMAL)

Serikali ya Tanzania imeshauriwa kuanzisha kampuni maalumu itakayoshughulikia maendeleo ya chanzo cha umeme cha Jotoardhi (Geothermal). Ushauri huo ulitolewa na Serikali ya Kenya kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Petroli ya nchini humu, Mhandisi Joseph Njoroge alipokutana na Ujumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ya Tanzania wakati wa ziara ya mafunzo ya jotoardhi, jijini Nairobi. 
Katibu Mkuu huyo alisema serikali ya Kenya kwa kuchukulia umuhimu wa chanzo hicho, iliamua kuanzisha kampuni inayojishughulisha na uendelezaji wa jotoardhi nchini humu ambayo inajulikana kwa jina la Geothermal Development Company (GDC). 
“Sisi tumeanzisha kampuni hii ambayo kazi yake ni kuendeleza chanzo hiki cha umeme ambacho gharama ya umeme wake ni nafuu ikilinganishwa na gharama ya umeme wa vyanzo vingine” alisema. Alishauri serikali ya Tanzania kushirikiana na sekta binafsi ili kuweza kuwa na uchimbaji wenye tija wa chanzo hicho ambacho gharama yake kubwa ni katika uchimbaji. 
 Aidha, alisema serikali ya Kenya inashirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha chanzo hicho kinaendelezwa. 
“Gharama za kuchimba ni kubwa sana takribani dola za kimarekani milioni 4.2 zinatumika katika uchimbaji pekee hapo bado gharama nyingine hiyo ni kuchimba tu” alisema 
Alisema serikali ya Kenya imekuwa na ushirikiano wa karibu na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya kupata fedha za utafiti wa awali wa kisayansi na fedha kwa ajili ya uchimbaji. Alisisitiza bila sekta binafsi maendeleo ya nishati hayawezi kufikiwa. 
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini wa Tanzania, Eliakim Maswi alisema ni wakati muafaka kwa Tanzania kushirikiana na nchi zingine za Afrika Mashariki ili kuendeleza rasilimali zinazopatikana katika nchi hizo. 
Alisema serikali ya Tanzania imeamua kujifunza uendelezaji wa jotoardhi kutoka Kenya kwaajili ya kuzalisha nishati ya umeme kwa kuwa nchi hii imepiga hatua ikilinganishwa na nchi nyingine za jirani. 
“Afrika Mashariki tuwe mfano wa kuigwa, tushirikiane katika kuendeleza rasilimali zilizopo nchini mwetu kwa manufaa ya umma” alisema. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Tanzania, Victor Mwambalaswa alisema serikali ya Tanzania imeonesha dhamira ya kweli katika kuendeleza jotoardhi. 
“Tumekuja hapa kwa lengo kuu moja ambalo ni kujifunza masuala ya uendelezaji wa jotoardhi ili nasi tuweze kunufaika na chanzo hiki cha kuzalisha umeme” alisema. 
Katibu Mkuu Maswi alisema ziara hiyo ya mafunzo imekuja baada ya Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kutembelea maeneo ambayo umeme wa jotoardhi unazalishwa na kuahidi kuleta wataalamu kutoka nchini Tanzania ili kujifunza. Alisema Serikali ya Tanzania ina nia ya dhati kuhakikisha wananchi wake wanapata umeme wa uhakika na wabei nafuu huku ziada inayopatikana inauzwa nchi nyingine.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!