Baada ya kuonya wananchi wanaotumia dawa za tiba mbadala ambazo hazijathibitishwa, Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), sasa inawataka wananchi kuacha kutumia mafuta ya ubuyu kwa kunywa kama dawa.
Akizungumza juzi katika Maonesho ya 37 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza, alisema Mamlaka hiyo ilipima na kubaini mafuta hayo yana tindikali ya mafuta.
Alifafanua katika maonesho hayo maarufu kama Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, kwamba mafuta hayo hayafai kuliwa na binadamu na anayekunywa kwa wingi, yuko hatarini kupata saratani za aina tofauti tofauti.
"Hivi karibuni kumekuwa na wimbi la wajasiriamali wanaouza mafuta ya ubuyu kama dawa, kwa kuwaelekeza wananchi kunywa. Napenda kuwataarifu kuwa mafuta hayo ni hatari kwani yana tindikali ya mafuta," alisema.
Mwandishi alipata sampuli ya vielelezo vya matumizi yake na manufaa yake mwilini, kama inayotangazwa na wajasiriamali katika maeneo mbalimbali na hata katika mitandao.
"Ni mafuta yatokanayo na mbegu za ubuyu {au kokwa}. Hukamuliwa kiini chake na kutoa mafuta. Yana ubora kuliko mafuta mengine ya kupikia, yana Vitamin A, B, C, D na F. Pia yanatibu magonjwa mbalimbali," kielelezo kimoja kilinadi ubora wake katika mitandao ya jamii.
Mafuta hayo yamedaiwa kutengeneza seli zote ndani ya mwili, kuzuia ngozi isiharibike wala kupata makunyanzi, kuondoa mafuta ndani ya mishipa ya damu na yanapunguza uzito uliozidi.
Pia inadaiwa yanarutubisha ini na figo, yanaleta hamu ya kula, yanaimarisha mifupa, kucha na nywele, yanaongeza kinga ya mwili (CD4), yanaondoa sumu na yanatengeneza sukari iwe katika kiwango kinachotakiwa.














No comments:
Post a Comment