Kiingilio cha chini katika mechi
ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Ivory Coast (The
Elephants) itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh.
5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti vya kijani katika uwanja
huo wenye uwezo wa kumeza watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya
rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya
chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio vya daraja la juu ni
kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni
kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni
sh. 30,000.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo
itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku mbili kabla ya mchezo
(Ijumaa na Jumamosi) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa,
Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo,
Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Salon iliyoko Sinza
Madukani.
Katika vituo hivyo tiketi
zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi
uwanjani siku ya mechi. Tunapenda kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi
mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi
bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
Utaratibu
katika mechi hiyo utakuwa kama ilivyokuwa katika mchezo wa Simba na Yanga,
ambapo hayataruhusiwa kuingia uwanjani isipokuwa kwa yale yatakayokuwa na
sticker maalumu kutoka TFF.














No comments:
Post a Comment