KATIKA hali isiyo ya kawaida na inayoashiria uzembe
katika ulinzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, juzi kijana mmoja mkazi wa eneo la
Phillips katika Kata ya Sekei jijini Arusha, Hamad Rashid (32) aliiba kiti
(kigoda) cha kukalishia Mwenge.
Kuibwa kwa kiti hicho kumethibitishwa na Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas. Kiti hicho hutumika kuwekea Mwenge wa
Uhuru unapokuwa katika mbio zake nchi mzima.
Tukio la kuibwa na kisha kukamatwa kwa mtuhumiwa
lilitokea juzi saa 11 jioni Sanawari eneo la Mataa. Eneo hilo ndilo lilipangwa
kwa ajili ya mkesha wa Mwenge huo baada ya kukamilisha mbio zake na kazi ya
kuweka mawe ya msingi na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jiji
la Arusha.
Kufuatia tukio hilo, Kamanda Sabas aliyetafutwa kwa
njia ya simu kuzungumzia tukio hilo, alikiri kutokea kwa wizi huo na kuongeza
kuwa mtuhumiwa huyo alishakamatwa na polisi waliokuwa wakiulinda Mwenge pamoja
na kiti hicho.
Alisema tukio hilo lilitokea wakati Mwenge huo pamoja
na wakimbizaji wake kitaifa, kimkoa na viongozi wengine wakiwa katika harakati
za kusoma salamu za utii kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya
ratiba ya utangazaji wa ratiba ya mkesha kutolewa.
Alisema kabla ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo,
alionekana kwa muda mrefu akiwa amesogelea gari lililokuwa limebeba kiti hicho
kilichoelezwa na kamanda kuwa kilikuwa cha akiba.
Alisema mara baada ya wizi kijana huyo alikamatwa na
katika mahojiano alisema alikuwa anataka kukiangalia tu na kwamba haikuwa nia
yake kukiiba na kuomba msamaha.
Hata hivyo alisema polisi wanaendelea kumhoji ili
kubaini dhamira halisi ya kukichukua kiti hicho.
Alisema mara baada ya upelelezi wa kesi hiyo,
mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani ili kujibu mashitaka yanayomkabili ya wizi
wa kiti hicho cha Mwenge wa Uhuru.














No comments:
Post a Comment