Thursday 30 January 2020

Wafungwa wataja vigogo dawa za kulevya

Image may contain: food
WAFUNGWA 130 katika Magereza ya Hong Kong nchini China, wametaja majina ya watu maarufu wakubwa, wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya nchini.

Majina hayo ya wafanyabiashara wakubwa, baadhi yao wanamiliki maduka makubwa yakiwemo ya vifaa vya ujenzi, ‘supermarket’, maduka ya nguo na maeneo ya kuuza magari maarufu yadi.

Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, James Kaji amesema katika majina waliyopokea, wengi wao ni wafanyabiashara wakubwa na kwamba wameanza kuyafanyia kazi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamishna huyo alikutana na Padri raia wa Marekani, John Wotherspoon maarufu ‘Father John’ ambaye alimkabidhi orodha ya wafungwa wa Tanzania wanaotumikia kifungo Hong Kong, baada ya kukamatwa na dawa za kulevya walizoingiza huko.
Katika orodha hiyo, Kamishna Kaji alisema “tumepokea na taratibu za kiuchunguzi zinaendelea, njia wanazotumia kuwatumia hao watu, lengo letu ni kung’oa mizizi ya tatizo.

“Kuna majina nikikuonyesha hutaamini, ni ‘mabig fish’, wapo mstari wa mbele kulipa kodi na kusaidia jamii, lakini nyuma ya pazia wanaendesha biashara haramu kwa kuwatumia watu.”

Alisema baadhi ya raia kutoka nje wanaokuja nchini, hawaji kwa nia njema, kwani wmekuwa wakitoa mafunzo na kuwaandaa vijana wadogo, kujiingiza katika mtandao huo wa dawa za kulevya, ikiwemo biashara ya madangulo kwa wasichana.

Alisema kitengo chake kipo mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kama vile kokeini, heroin na aina nyingine ya dawa za kulevya. Alieleza kuwa hiyo ni vita ngumu, hatari na inahitaji kubadili mbinu kila wakati.

“Wauzaji, wabebaji Tanzania na kwingineko duniani, wamekuwa wepesi katika kubadili mbinu ili kukwepa jicho na mkono wa dola, ni wajanja sana sana na mbaya zaidi ni watu wenye mikono mirefu,” alisema.

Hata hivyo, Kaji alisema baada ya kudhibiti uchochoro wa kiwanja cha ndege, wamebaini kuwa njia ya bandari imekuwa uchochoro kwa dawa hizo kupitia kwenye magurudumu na milango ya gari, kuwekwa kwenye saruji nyeupe na pipi.

Alisema kwa nchini wamedhibiti utumiaji na uingizaji wa dawa hizo kwa asilimia 98. Kwamba kwa sasa wauzaji hao wa dawa za kulevya, wanatumia nchi za Afrika Kusini na Msumbiji, kama uchochoro wa kupitishia dawa hizo.

“Kuna Watanzania watatu ambao wamekamatwa mwezi huu wa Januari Hong Kong. Watanzania hao walitokea Ethiopia, hawakupita kwenye ‘airport’ zetu,” alisema.

Kauli ya Kaji imekuja kufuatia mwishoni mwa wiki, ‘Father John’ ambaye anahudumu kwenye magereza, alikutana na familia za wafungwa wa dawa za kulevya waliopo Hong Kong na China.

Alisema zaidi ya Watanzania 1,000 wapo kwenye magereza mbali mbali duniani huku 68 wakisubiri kunyongwa.
Kwa mujibu wa Kaji, Gereza la Hong Kong peke yake lina wafungwa 130 na wengi wao ni vijana wadogo, waliotumika kubeba dawa hizo.
Magereza mengine yenye idadi kubwa ya Watanzania ni ya India na Afrika Kusini.

Chanzo: Habari Leo

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!