Thursday 23 January 2020

Neno la leo toka kwa Maggid Mjengwa!


Neno La Leo: Ya Akina Trump Na Tabia Za Mbweha...
Ndugu zangu,
Nimesikia uvumi kuwa Trump anakusudia kuiingiza nchi yetu kwenye orodha ya nchi za kufungiwa (Travel ban) watu wake kusafiri kuingia Marekani.


Nasema uvumi kwa vile siamini kama ni kweli. Na kama itakuwa kweli, basi itakuwa ni kichekesho. Kwamba katika nchi za dunia hii, Tanzania iliyojituliza kama kasuku , na huku watu wake kuna ambao hawajawahi kusikia mlio wa bastola, eti, ije kuwa miongoni mwa nchi zenye kuhatarisha amani ya Marekani!
Katika dunia hii hata kama wewe umeamua kuwa mhisani, basi, mheshimu pia unayemhisani, maana, yumkini kesho nawe utamhitaji akuhisani.
Usimnyanyase na kumdharau unayemhisani kwa vile tu ana shida. Inasikitisha taifa kama Marekani likiamua kutufanyia hila hiyo ya mbweha.
Mapungufu kwa nchi yaweza kuwepo, lakini katika dunia ya diplomasia , yanajadilika.
' Kuiwekea vikwazo vya safari ' nchi huru ni kuidhalilisha.
Ona, duniani hapa kuna mifano hai ya mataifa yenye kukiuka misingi ya demokrasia na utawala bora, na hata kuwazuia wananchi wao wasitumie mitandao ya kijamii kwa kuifunga, lakini, wakubwa hawa , kwa vile wana maslahi ya kiuchumi na nchi hizo, masuala hayo huyafumbia macho.
Huu uvumi wa Trump kutuweka kwenye orodha ya nchi za kufungiwa safari kwenda Marekani ukiwa kweli, basi, ni kama kisa kile cha mbweha na mwanakondoo.
Mbweha alikuwa mlimani na kunywa maji yaliyokuwa yakitiririka chini bondeni. Alipomwona mwana kondoo chini bondeni, naye akiyanywa maji hayo hayo, mbweha akamtamani mwanakondoo na akawa anatafuta sababu ya kumtafuna.
Mbweha akaanza kwa kulalamika;
" We mwana kondoo, mbona unayachafua maji ninayokunywa?"
" Hapana, mbona mie nakunywa maji yanayotoririka kutoka kwako" Alijibu mwanakondoo.
Mbweha akaendelea..
" Ah, nimekumbuka, ni mwaka jana ulichafua maji niliyokuwa nikiyanywa"
" Hapana, mie mwaka jana nilikuwa sijazaliwa."
Mbweha baada ya kukosa sababu, akatamka kwa hasira;
"Potelea mbali, kama si wewe basi alikuwa ni mama yako!"
Mwanakondoo pamoja na majibu yake mazuri na yenye mantiki hakunusurika na kuliwa na mbweha...!
Naam, wahenga wetu walisema; " Hasidi hana sababu.."
Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!