Saturday, 16 November 2019

MWANAFUNZI ALIYEFICHWA VIFO VYA WAZAZI, NDUGUZE WATATU APATA TAARIFA

Image may contain: 1 person, standing and outdoor
Hatimaye Anna Zambi (16), binti aliyefiwa na wazazi wake wawili na ndugu zake watatu waliopata ajali wakati wakienda kwenye mahafali yake mkoani Kilimanjaro Oktoba 26, 2019 leo Jumamosi Novemba 16, 2019 amefahamishwa kuhusu vifo hivyo.


Amewasili nyumbani kwao Goba Dar es Salaam saa 10.30 alfajiri akitokea shule ya Sekondari ya Mather Theresia of Calcuta baada ya kumaliza mtihani wa Taifa wa kidato cha nne ulioanza Novemba 4, 2019.
Wazazi wake, Lingston Zambi na Winifrida Lyimo na wadogo zake watatu, Lulu, Andrew na Grace walikufa katika ajali hiyo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa iliyonyesha wilayani Handeni mkoani Tanga.
Baada ya vifo hivyo, Anna ambaye hakuelezwa chochote na hata alipomaliza mitihani yake pia hakuambiwa mpaka leo alipofika nyumbani na kupewa habari hizo.
Ndugu zake walipata wakati mgumu kuhusu jinsi ya kuanza kumpa taarifa hiyo ya huzuni.
"Alipofika watu wanne walikwenda kumweleza. Kwa kweli alilia sana. Alipoingia ndani alijilaza miguuni mwa bibi yake na kuendelea kulia.”
"Aliongea mengi huku akilia akasema alihisi jambo hilo na kuna wakati alikuwa anaamka usiku na alisema mitihani yake amefanya kwa taabu sana," amesema Ibrahim Zambi ambaye ni baba yake mdogo.
Ibrahim amesema Anna alikuwa akilia na kuzungumza maneno ya simanzi, “mwenyewe alisema ‘kwanini mliniacha, hamkuja kunichukua tuondoke wote’.”
Ameongeza, “tunashukuru Mungu tulihofia sana angepata shida kubwa ila amepokea vizuri anaomboleza tu.”
Dk Doya Frederick aliyepo nyumbani kwa kina Anna, ameshauri mtoto huyo apumzike na baadaye asaidiwe kiimani na kisaikolojia.
"Mtu anapopata taarifa za jambo gumu anapitia hatua kadhaa ili akae sawa ndipo asaidiwe kisaikolojia lakini pia ajengwe kiimani. Hatua hizo ni kukataa, hasira, kubishia kwamba haiwezekani lakini baadaye kukubali uhalisia," amesema Dk Doya.
Tangu alipofika nyumbani kwao hadi saa 4 asubuhi leo alikuwa amepumzika kabla ya kushiriki ibada maalumu.
Baada ya ibada atapelekwa katika makaburi walikozikwa wazazi na ndugu zake kwa ajili ya kuweka mataji ya maua.
Na: Mwananchi

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!