Tuesday, 19 December 2017

Wafungwa 2 wakuta wake,watoto wamekufa

YOHANA Chengula (71) na Aloyce Mwalongo (80) ni miongoni mwa wafungwa 61 ambao kamwe hawataisahau Desemba 9, 2017, siku ambayo waliachiwa huru kutoka gerezani.


Wafungwa hao walipata msamaha wa Rais John Magufuli wakiwa wamesota gerezani kwa takribani miaka 44. Walikuwa wakitumikia adhabu iliyobadilika kutoka kunyongwa na kuwa kifungo cha maisha baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya mauaji mwezi Machi mwaka 1978.
Rais Magufuli alitoa msamaha huo wakati wa maadhimisho ya Miaka 56 ya Uhuru ambapo wafungwa 8,157 waliokuwa wamehukumiwa kwa makosa mbalimbali walinufaika na msamaha huo.
Chengula akuta mke watoto 4 wamefariki dunia Akizungumzia maisha mapya nje ya gereza, Chengula alisema: “Nashukuru kwa sasa nipo uraiani nimepata fursa ya kuona ndugu zangu waliobaki, wajukuu na mwanangu pekee aliyebakia baada ya wale wanne niliozaa na mke wangu wa kwanza kufariki, sasa nafsi yangu ipo huru nikiamini hata kama Mungu ananichukua nitakuwa kwenye mikono yao.
“Mke wangu aliyesababisha mimi nikapatwa na masahibu haya naye niliambiwa alishafariki dunia, sina kinyongo naye na nina muombea amani huko alipotangulia nikiamini sisi binadamu sote njia yetu ni moja, si ajabu hata kesho mimi au wewe tunaweza tukaitwa na Mwenyezi Mungu aliyetuumba,” alisema Chengula.
Alisema mbali na msamaha mkubwa alioupata kutoka kwa Rais Magufuli, anamuomba asiache kumuangalia yeye na wafungwa wenzake walioachiwa ikibidi kuwawezesha kwa chochote kutokana na hali mbaya ya kiuchumi waliyonayo na mazingira ya huko kijijini wanayokwenda kuishi mara baada ya kuwa huru.
“Tunarudi kijijini, hatuna ndugu wala familia tena…tunakwenda kuanza maisha upya nasi ni wazee, hatuna jipya la kufanya huko tuendako zaidi ya kupambana na hali ya umasikini nami ndiyo kama unavyoniona niliingia gerezani nikiwa mzima na sasa nikiwa mlemavu.”
Aidha Chengula amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kumsaidia mguu utakaomwezesha kutembea akidai kuwa alipata taarifa kuhusu uwezeshaji wa viungo bandia unaofanywa na Makonda akiwa gerezani, huku naye akiwa mmoja wa walemavu walioandika barua kuomba kusaidiwa.
Mwalongo naye akuta majonzi nyumbani Kwa upande wake Mwalongo ambaye mwili wake bado unaonekana upo imara licha ya uzee alionao, alisema aliingia gerezani kutokana na kesi hiyo akiwa kijana wa miaka 35 huku akiacha mke na watoto watano wa kuwazaa na mkewe ambaye kwa sasa ni marehemu. “Ukiacha mke wangu, pia watoto wangu watatu nao wamefariki dunia.
Utaona ni matatizo kiasi gani yameipata familia yangu… ila naamini hii yote ni mipango ya Mungu kwa kuwa yameshatokea basi, ila tunashukuru Mungu tunarudi nyumbani japo tuweze kuhani katika makaburi yao.” Alisema alikwenda gerezani akiamini mwisho wa maisha yake yote yatakuwa humo, lakini Desemba 9, mwaka huu imebadilisha kile alichokiamini miaka yote baada ya kupewa msamaha na Rais Magufuli.
Alisema tangu waingie gerezani ni awamu tatu za marais zimepita, hivyo kitendo cha Rais Magufuli kutoa msamaha kwao, kinaonesha wazi ni namna gani Mungu anaweza kutenda miujiza…zaidi anamshukuru kwa moyo wake wa huruma aliouonesha kwao na kwa wafungwa wengine waliopata msamaha huo. Aidha alisema kwa kuwa sasa wanarejea kijijini mkoani Njombe, hawana namna nyingine ya kuendesha maisha yao zaidi ya kuwa tegemezi kutokana na hali waliyonao baada ya kutoka gerezani.
“Ningependa kuwa mfugaji kama nikibahatika kupata mifugo, sina jambo lolote la msingi nitakalokwenda kulifanya kwa sasa zaidi ya kukaa nyumbani na kulea wajukuu hivyo nikipata msaada wa kuwezeshwa japo mifugo nitashukuru.”
Chengula na Mwalongo ni kati ya wafungwa watano waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa, lakini walibadilishiwa adhabu hiyo na kuwa kifungo cha maisha katika msamaha uliotolewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere, Aprili 18, 1983. Chengula na kisa cha kukatwa mguu Akizungumzia mkasa mzima Chengula ambaye kwa sasa ni mlemavu akiwa na mguu mmoja, anasema: “Chanzo cha matatizo haya yote ni mke wangu niliyezaa naye watoto wanne ambaye hadi matatizo yananipata nilikuwa nimeshatengana naye.
“Vitendo vyake vya uhuni ndivyo vilivyosababisha mimi na wenzangu kupewa kesi ya mauaji ya raia mmoja wa India, wakati huo wote tukiishi mjini Njombe mkoani Iringa. “Nakumbuka siku ya tukio, wakati huo nikiwa na miaka 28, mimi na marafiki zangu tulikuwa nyumbani tukiendelea na maongezi huku tukipata soda na bia, vinywaji nilivyokuwa nikiiuza katika baa yangu, tukiwa hatuna hili wala lile ghafla tulisikia kelele za moto kutoka nyumba ya jirani umbali mfupi kutoka kwangu, ndipo ikatulazimu sote tutoke kwa ajili ya kwenda kutoa msaada”.
Alisema baada ya kufika walikosa namna ya kuokoa chochote kutoka ndani ya nyumba hiyo kutokana na moto mkali uliokuwa ukiwaka, lakini baada ya muda mfupi walipata usaidizi kutoka kwa wanajeshi waliokuwa wakipita kuelekea Songea ambao waliisogelea nyumba hiyo na kupiga mlango teke kuona kama kuna mtu yeyote angeweza kutoka ingawa hawakuwa na uhakika kama kulikuwa na mtu.
Alisema baada ya muda kidogo polisi walifika wakati huo moto ukiwa umezima na waliingia ndani ya nyumba hiyo na kutoka na mwili wa raia huyo wa India akiwa ameshafariki dunia baada ya kuteketea kwa moto.
“Baada ya tukio hilo tulikaa mtaani kwa siku kadhaa huku nikiendela na biashara zangu ikiwemo ya usafirishaji abiria na mizigo nikitumia gari yangu mwenyewe aina ya Toyota Stout niliyoinunua kwa Sh 15,000 kipindi hicho, lakini ghafla Oktoba 30, 1974 jioni, nilishitukia nafuatwa na polisi wakinitaka kwenda kuhojiwa kutokana na kifo cha mtu huyo.
“Sikuwa na wasiwasi pale nilipofuatwa kwa kuwa nilijua wazi kuwa sikuhusika na kitu chochote kutokana na kifo cha mtu huyo ambaye kwa kipindi fulani pia aliwahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na aliyekuwa mke wangu ambaye kwa kipindi hicho nilikuwa tayari nimeshamuacha.
“Ndiyo maana hadi sasa nasema aliyekuwa mke wangu ndiyo hasa chanzo cha mimi na wenzangu kwenda jela kwa sababu kama angekuwa ametulia ndani ya ndoa tusingekuwa tumeachana naye na baadaye yeye kuwa na uhusiano na mtu huyo ambaye kifo chake kilihusishwa na fikra kuwa mimi nilihusika kutokana na uhusiano wake na mke wangu.”
Alisema alipofika polisi aliwakuta marafiki zake wanne wakiendelea kuhojiwa na baada ya hapo walipelekwa Gereza la Iringa wakisubiri kesi yao kusomwa wakati huo ikiwa tayari wameshakaa jela kwa takribani miaka minne.. ..na ilipofika Machi 14, 1978 ilitolewa hukumu ambayo ilibadili ndoto zao zote za kimaisha. Alisema katika hukumu hiyo yeye na mwenzie mmoja aliyekuwa akitekeleza kifungo chake katika Gereza la Isanga Dodoma walihukumiwa kunyongwa, wengine wawili waliwekwa gerezani wakisubiri kutolewa kwa amri ya Rais huku mmoja wa mwisho (Mwalongo) akipewa adhabu ya kifungo cha miaka 10 gerezani.
“Hukumu yenyewe ilimshangaza kila mmoja, lakini tunaamini kuwa yote haya yalipangwa kwetu kwa sababu maalumu, kwani hata mazingira ya kesi yenyewe na ushahidi ulijawa na uongo mtupu, pia mazingira ya kesi yenyewe yalikuwa na utata yaani kimsingi ni jambo tulilokuwa tumeandaliwa lituhusu,” alisema Chengula.
Mateso gerezani Chengula alisema kilichomuuma wakati akiwa gerezani ni familia yake, na hasa mke wake mdogo ambaye wakati anapewa hukumu hiyo alimuacha akiwa na mtoto mwenye umri wa wiki mbili (Feines Chengula), ambaye kwa sasa ni mwalimu mkoani Morogoro alipoamua kuikimbia familia yake na kuiacha ikitangatanga.
“Mbali na mke wangu na mtoto wangu huyo mdogo niliyezaa naye, lakini pia niliacha watoto wanne niliokuwa nimezaa na mwanamke niliyeachana naye, ambao aliwatelekeza. “Lakini pigo lingine ilikuwa ni biashara zangu za maduka, nyumba ya kulala wageni pamoja na gari yangu ambavyo vyote vilitaifishwa na Polisi kwa madai kuwa nyumba yangu ilihusika katika kuhamisha mali zilizokuwa kwenye nyumba ya mhindi huyo kabla ya kuteketea.”
Chanzo cha kukatwa mguu Alisema akiwa gerezani, maisha yake yalikumbwa na misukosuko ya kila aina lakini kubwa ni magonjwa yakiwemo kipindupindu kilichompata akiwa Gereza la Isanga Dodoma, na kisukari kilichompata akiwa gerezani mkoani Morogoro ambacho baadaye mwaka 2003 kilifanya ahamishiwe katika Gereza Kuu la Ukonga.
Chengula alisema akiwa Gereza la Ukonga hali yake ilianza kuwa mbaya na kusababisha mguu kujaa maji kutokana na ugonjwa wa kisukari, hatua ambayo baadaye ililazimu kukatwa kwa mguu huo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kumuokoa dhidi ya kifo alichodai kuwa kwa wakati huo aliona dalili za waziwazi kuwa kilikuwa kinamuita.
Alisema akiwa katika Gereza la Ukonga aliendelea kumuomba Mungu usiku na mchana huku akiamini kabisa siku zake za kuishi gerezani huko zikienda ukiongoni kutokana na uzee aliokuwa nao ukichanganya na maradhi ya hapa na pale yaliyokuwa yakimkabiri. Shemeji atoa ushuhuda Kwa upande wake Rosemary Mkwama ambaye ni shemeji wa Chengula, alisema wakati shemeji yake huyo akikamatwa alikuwa na umri mdogo na wakati huo alikuwa akisubiri matokeo yake ya mtihani wa darasa la saba.
Alisema wakati huo alikuwa akiishi kwa Chengula ambaye mdogo wake alikuwa mume wa dada yake huku yeye akilelewa katika ukoo huo, wakiishi kwa amani mustarehe pasina shaka yoyote hadi siku walipofika polisi katika nyumba wanayokaa na kumkamata shemeji yake.
Alisema wanashukuru kwa kuwa sasa ndugu yao huyo yupo uraiani, huku wakitoa pongezi na shukrani kwa Rais Magufuli kwa kitendo chake cha kuwaachia huru wakiamini kuwa walionewa. Alisema wanatarajia Chengula ataanza safari ya kuelekea Njombe leo huku baadhi ya ndugu zake kutoka maeneo mbalimbali nchini na wanakijiji aliokuwa akiishi nao wakimsubiri kwa hamu ili waweze kumsabahi na kumkaribisha kuanza upya maisha ya uraiani kijijini Njombe.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!