RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni amesema, amefi kisha umri wa miaka 73 kwa sababu hanywi pombe na hana muda wa kuugua.
Mwanasiasa huyo amezungumzia umri wake, siku chache tu baada ya kusema kuwa kwa kuwa yeye ni Mkristu na mfuasi wa Yesu Kristu, haogopi kifo kwa sababu anaamini atafufuka.
Museveni ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa, ukiwa mlevi unakuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa, yakiwemo yanayosababishwa na virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga mwilini (Ukimwi).
“Nimekuwa hapa kwa miaka 30 iliyopita na kwa muda wote huo hamjasikia kwamba Museveni ni mgonjwa na amelazwa. Sina muda wa kuugua,” aliandika kiongozi huyo kwenye ukurasa huo. Museveni amekuwa Rais wa Uganda tangu mwaka 1986.
Kwenye ukurasa huo, Rais Museveni alisema, magonjwa mengi yangezuilika milele, kama watu wangejihakikishia usafi unaohitajika, wangepata lishe nzuri, wangelala kwenye vyandarua vyenye dawa ya kuua mbu, na wangepata kinga.
“Pia watu waache tabia hatarishi na ulevi kwa sababu wanakuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa kama vile Ukimwi,” aliandika Rais Museveni. Siku chache kabla ya kuandika hayo, Rais Museveni alihudhuria mazoezi ya wanajeshi ya kupiga risasi katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Karama, ambako alitoa ushauri kwa askari kuacha mitindo hatarishi ya maisha.
“Hongera kwa askari na ushauri wangu kwao ni kwamba wajiepushe na mitindo hatarishi ya maisha, waepuke umalaya, pombe na rushwa. Maisha yenu siku zijazo ni mazuri,” aliandika kwenye ukurasa huo wa twitter.
Wakati anazungumza na Wakristu kwenye uwanja wa Akii-Bua mjini Lira, wakati akizindua uchangiaji wa ukarabati wa Kanisa Kuu la Jimbo la Lira, Rais Museveni alisema kwa kuwa yeye ni mfuasi wa Yesu Kristu, haogopi kifo, na atakishinda kwa kufufuka.
Kiongozi huyo alisema ufufuo wa Yesu Kristu, unathitisha kwamba hata yeye anaweza kufufuka. “Sasa sisi wote ni Wakristu, kwa nini? Kwa sababu Yesu alikuja, akateswa na alizikwa lakini alifufuka. Alipofufuka alitupatia tumaini kwamba, sisi pia tutafufuka,” alisema Rais Museveni.
Katika hadhara hiyo, Museveni aliunga mkono kilichoandikwa kwenye kitabu cha 1 cha Wakorinto 15:26 kwenye Bibila Takatifu kwamba ‘Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni kifo’ “Kama hakuna ufufuko hakuna Ukristu. Bado sijafa na kufufuka, lakini natumaini kwa sababu mimi ni Mkristu” alisema.
No comments:
Post a Comment