MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira ametangaza rasmi kuachana na Chama cha ACT-Wazalendo na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM) huku akisema hakuna atakayebaki upinzani chini ya uongozi wa sasa wa Rais John Magufuli unaochapa kazi.
Mghwira ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo alitangaza uamuzi huo jana katika Mkutano Mkuu wa tisa wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT). Mkuu wa Mkoa huyo, alitangaza uamuzi huo baada ya kukaribishwa na Rais John Magufuli kuwasalimia wanachama wa umoja huo na kupewa nafasi ya kuzungumza.
Mgwira alisema, amefikia uamuzi huo wa kuachana na ACT-Wazalendo kutokana na kuiona CCM inabadilika kwa kukataa rushwa na kulitanguliza Taifa mbele. Alisema alikuwa ACTWazalendo kama Mwenyekiti lakini alipenda utaratibu wa CCM wa namna watu wanavyojipanga na kuendesha mambo yao kwa namna inayoeleweka ndani ya chama na wanachama wenyewe na mbele ya umma wa nchi.
Mgwira alisema akiwa Mkuu wa Mkoa anashirikiana na watu wa vyama vyote bila kuwabagua na katika vyama hivyo vyote, anaona CCM ndiyo inayobadilika. Alisema anaona juhudi za kila mtu, lakini za mtu anayebadilika ni tofauti.
“Mtu anayebadilika anataka atambulike amebadilika. Wakristo wanajua maana ya kuokoka siyo wanahama duniani lakini wanataka kusema wamebadilika na watakuwa watu wema,” alisema.
Alibainisha kuwa chini ya Uenyekiti wa CCM wa Rais Magufuli hakuna ambaye atataka kubaki katika vyama hivyo vya upinzani. Mghwira anaendeleza wimbi la viongozi wa ACT- Wazalendo na wa Chadema kujiunga na CCM katika nyakati tofauti kwa kuvutiwa na sera za CCM.
Wengine waliojiunga kutoka ACT- Wazalendo ni Katibu Mkuu, Samson Mwigamba na mshauri wao, Professa Kitila Mkumbo. Alisema baada ya kufanya kazi chini ya Serikali ya awamu ya tano kwa miezi saba, anaona ana kila sababu ya kutangaza kujiunga na CCM.
Baada ya kutangaza uamuzi hao, Rais Magufuli alimpongeza kwa uamuzi wake na kuwapongeza pia wanachama 2,880 waliojiunga na UWT jana kwenye mkutano huo. Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wastaafu wakiwemo wake wa marais wastaafu wakiongozwa na Maria Nyerere na wenyeviti wa umoja huo waliostaafu akiwemo Sophia Simba.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu wa CCM, Abdrahman Kinana na mke wa Rais, Janeth Magufuli.
No comments:
Post a Comment