RAIS John Magufuli ameitaka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee kuhakikisha inapanga upya mgawanyo wa wahudumu wa afya nchini ili wananchi katika maeneo yote wapate huduma bora za afya.
Aliyasema hayo jana wakati akizindua Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Kampasi ya Mloganzila iliyopo wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani.
Hospitali hiyo imejengwa kwa Sh bilioni 206.7 na kati ya hizo Sh bilioni 39.4 zimetolewa na serikali, wakati Sh bilioni 167.3 zimetolewa na Korea Kusini, ikiwa ni mkopo wenye masharti nafuu. Hospitali hiyo imejengwa katika eneo la ekari 3,865.6.
Aponda mpangilio wa Madaktari Akifafanua zaidi haja ya kufanya mabadiliko hayo, Rais Magufuli alisema asilimia 60 ya madaktari bingwa wako Dar es Salaam na asilimia 40 ndiyo wako kwenye hospitali za mikoani.
Alisema mgawanyo huo haufai kwa kuwa unaathiri utoaji wa huduma bora za afya kwa maeneo mengine ya nchi. “Kwa mfano Hospitali ya Taifa Muhimbili ina vitanda 1,600 na madaktari bingwa, madaktari wanafunzi na madaktari wahadhari jumla 532.
Maana yake kwa Muhimbili daktari mmoja anahudumia vitanda vitatu, wakati Hospitali ya Mkoa wa Tabora daktari mmoja anahudumia wagonjwa 208,329 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012.
“Lakini pia Hospitali ya Manispaa ya Temeke yenye kuhudumia wastani wa wajawazito 100 wanaojifungua kwa siku na ina madaktari bingwa wa akina mama wawili, wakati Hospitali ya Muhimbili inayowahudumia wajawazito wanaojifungua kati ya 40 hadi 50 kwa siku, ina madaktari bingwa 40, hii inaonesha kuwa hakuna mgawanyo mzuri wa madaktari wachache tulionao,” alieleza Rais Magufuli.
Hospitali za Mikoa kuhamishiwa Wizara ya Afya Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema tatizo hilo la mgawanyo usiofaa linasababishwa na mambo makubwa mawili, la kwanza ni kwa kuwa hospitali kubwa nyingi ziko Dar es Salaam ambako mazingira ya kazi mazuri, na pili ni kitendo cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuamua kuzisimamia Hospitali za Rufaa na Hospitali Maalumu Bingwa pekee na kuziacha Hospitali za Mikoa chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Kutokana na sababu hizo, Rais Magufuli aliigiza Wizara ya Afya kuhakikisha inarekebisha kasoro hiyo na kuzirejesha Hospitali zote za Mikoa chini ya Wizara ya Afya na zile za Wilaya kushuka chini ndiyo zibaki Tamisemi.
Alisema hali hiyo ikiruhusiwa kuendelea, wananchi wengi watakuwa hawahudumiwi vizuri kwenye hospitali za chini, lakini hata wakipewa rufaa kwenda hospitali kubwa wanakuwa wameshachelewa na hivyo inakuwa vigumu kutibika.
Alisema hospitali zote za mikoa 31 zihudumiwe na Wizara ya Afya. “Huwezi kuongeza bajeti ya dawa kutoka Sh bilioni 31 hadi Sh bilioni 269, halafu hospitali za mikoa ziendelee kuwa chini ya Tamisemi, zinaendeshwa na watu ambao si wataalamu, lazima tuheshimu taaluma.
Wizara ya Afya ndiyo wasimamizi wa sera, mnajua daktari gani aende mkoa gani, nani asimamie wapi, na siyo Tamisemi,” alisema Rais Magufuli. Asisitiza madaktari wa kutosha Mloganzila Ili kuhakikisha Hospitali ya Mloganzila haikabiliwi na changamoto ya madaktari na wauguzi, Rais aliagiza wafanyakazi wa kitengo cha ndani wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuhamishiwa Hospitali ya Mloganzila.
Alisema Hospitali ya Mloganzila ina uhitaji wa wafanyakazi 950. Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Muhimbili ina jumla ya wafanyakazi 2,892 ambao kati yao madaktari ni zaidi ya 400, wauguzi zaidi ya 1,100, wahudumu wa afya zaidi ya 500 na wafanyakazi wengine zaidi ya 800.
Alisema Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) ina wafanyakazi 700, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ina wafanyakazi 220, lakini kwa pamoja Muhimbili, MOI na JKCI zina wafanyakazi 3,817.
“Wakati Hospitali ya Mloganzila ina vitanda tupu 571, Wodi ya Mwaisela Muhimbili ina vitanda 244 na inatibu wagonjwa wa nje zaidi ya 400 na kulaza wengine kati ya 25 na 35, kuna madaktari bingwa wenye shahada ya kwanza 73, madaktari wanaofanya mazoezi kwa vitendo wako kati ya 10 na 20 na wauguzi 169.
“Kwa upande wa Sewahaji kuna vitanda 224, Kibasila vitanda 206 na Wodi ya Wagonjwa wa Akili vitanda 66,”alieleza Rais Magufuli. Alisema kitengo cha wagonjwa wa ndani kina uniti 8, hivyo kama wahudumu wote wa kitengo hicho pamoja na wagonjwa wakihamishiwa Mloganzila, hospitali hiyo itakuwa imepata jumla ya madaktari 73 na 40 kati yao ni madaktari bingwa, wauguzi wahudumu 169 na wagonjwa zaidi ya 250.
Rais aliwataka madaktari na wahusika wengine wote kutanguliza uzalendo na kuepuka ubinafsi ambao hauna faida. Aliwataka watu wa Muhimbili, Chuo, MOI, JKCI, Wizara ya Afya na wataalamu wengine kulishughulikia hilo kwa faida ya taifa.
Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa mahitaji ya wahudumu wa afya nchini ni 184,901 lakini waliopo ni 89,842, hivyo kuna upungufu wa watumishi wa afya 95,059, na vibali vya ajira vilivyotolewa ni 3,410.
No comments:
Post a Comment