Sunday, 26 November 2017

Ajira za watoto changamoto inayoikabili jamii

Pamoja na wanaharakati wa haki za binaadamu nchini kukemea ukiukwaji wa haki za binaadamu ikiwemo haki za mtoto, bado kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto.

Kwa miaka mingi nchini haki za watoto zimekuwa zikikiukwa hasa katika suala la kuwatumikisha watoto katika ajira mbali mbali ambazo haziendani na umri wao kisheria.
Watoto wengi wamekuwa wakitumikishwa katika ajira mbali mbali ambazo zinawaathiri kisaikolojia na hata makuzi ya watoto hao.

MAANA YA MTOTO.
Ibara ya 1 ya Mkataba wa Umoja wa Kimataifa wa haki za mtoto 1989 (CRC ) imetoa tafsiri ya mtoto ikiwa na maana kuwa ni binaadamu yoyote aliye na umri chini ya miaka 18, isipokuwa kama sheria inayotumika inatambua umri wa utu uzima kabla ya hapo.
Hakuna maana ya moja kwa moja ya maana ya mtoto isipokuwa maana hiyo hutegemea mazingira itakayotumika.
Kwa mujibu wakifungucha 3 (1) cha sheria ya ajira Zanzibar namba 11 ya mwaka 2005 inatoa maana ya mtoto
“Ni mtu aliye chini ya miaka 17 isipokuwa kwa shughuli za ajira katika sehemu za hatari mtoto ni kijana chini ya umri wa miaka 18”.
MAANA YA AJIRA ZA WATOTO.
Ajira za watoto ni kuwatumikisha watoto walio chini ya umri wa miaka 18 kufanya kazi ambazo hawastahiki kuzifanya kutokana na umri waokwani zinawadhoofisha na zinahatarisha maisha yao.
Kwa mujibu wa mkataba wa 182 wa shirika la kimataifa la ajira (ILO) wa 1999 kuhusu mifumo mibaya zaidi ya ajira ya watoto katika ibara ya 3 umetoa tafsiri ya ajira za watoto ni kazi zozote zinazoweza kudhuru afya,usalama na maadili ya watoto.
AJIRA ZA WATOTO NA SHERIA.

Ajira za watoto ni jambo linalopigwa vita dunia nzima kutokana na ukweli kwamba ni kazi zinazohatarisha makuzi ya mtoto na kumuweka katika hatari au hali tete na kumsababishia maisha mabovu mbeleni.

Sheria mbali mbali zinapinga ajira za watoto, kifungu cha 6 cha sheria ya Ajira Zanzibar namba11 ya 2005 kinakataza ajira za watoto, hakuna mtu yoyote atakayeruhusiwa kumuajiri mtoto isipokuwa kwa kazi za nyumbani ambazo hazitohatarisha ustawi wa mtoto.

Vile vile kifungu hicho kimeweka adhabu kwa mtu atakaemuajiri au kusababisha mtoto kuajiriwa kinyume na maelezo ya kifungu cha 6, mtu huyo atakuwa ni mkosa na atatozwa faini isiopungua shilingi laki tano (500, 00/=) au kifungo kwa kipindi sio chini ya miezi 6.

Watoto wana haki kama watu wazima na wanahitaji taratibu za kipekee ili haki hizo ziheshimiwe. Ibara ya 32 ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za mtoto CRC 1989 ambao Tanzania imeuridhia mkataba huo tarehe 2 DEC 1990 inasema na kusisitiza “kila  mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya unyonyaji wa kiuchumi na kufanya kazi yoyote ambayo inaweza kutatiza elimu, ama kuwa na madhara kwa afya au maendeleo ya kimwili, kiakili,kiroho, kimaadili na kijamii’

Pamoja na kuwepo kwa mikataba mbali mbali ya kuwalinda watoto dhidi ya utumikishwaji na udhalilishwaji  tatizo hili linaongezeka kwa kasi na watoto kujikuta wakikosa haki zao za msingi kama kucheza, kupata elimu, kutunzwa na kulindwa.

Kutokana na kushamiri kwa ajira za watoto visiwani mwetu, ambapo baadhi ya wananchi katika jamii zetu wanatumia nafasi hiyo kuwapa ajira ngumu watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ambapo sheria inawatambua kuwa bado ni watoto.
Mfano wa ajira hizo ni kufanya biashara, kubanja kokoto, kufanya kazi za nyumbani (house girl), kupara samaki n.k

Vile vile kuna watoto ambao wanaingizwa katika mifumo mibaya zaidi ya ajira za watoto. Fasiri hii ya mifumo mibaya zaidi ya ajira za watoto imokatika  kifungu cha 7 cha sheria ya ajiranamb. 11 ya 2005 sheria ya Zanzibar ambapo unajumuisha:-

  1. Aina zote za matendo ya utumwa mfano uuzaji, usafirishaji, utoroshaji wa watoto, kazi za lazima na utumwa au kuajiri kwa lazima kwa ajili ya kuingia katika mgogoro ya kivita.
  2. Matendo ya ukahaba kwa mfano kupigwa picha za uchi au kufanya maigizo yenye picha za uchi.
  3. Kuwatumilia watoto kwa kufanya kazi zisizo halali hasa ikiwemo kusafirisha madawa ya kulevya.
  4. Kazi ambayo kwa mazingira yake inaweza kupelekea kupata athari ya kiafya, usalama pamoja na kuharibu maadili ya watoto.

Ili kukipa nguvu kifungu hiki sheria pia inaweka adhabu kwayule ambaye atafanya makosa yaliyoelezwa hapo juu na adhabu yake ni faini sio chini ya milioni tatu (3,000,000/=) au kifungo kisichopungua mwaka mmoja au adhabu zote mbili.

 Kifungu cha 8(i) cha sheria hii pia kinakataza ajira kwa kijana ambae anasoma elimu ya lazima (compulsory education) kwa kijana ambae hayuko katika elimu ya lazima, ajira inaruhusiwa lakini kwa masharti yafuatayo:-

  1. Asipewe kazi nzito zikiwemo za kutumia kemikali au kazi nyengine yoyote abayo inaweza kuhatarisha afya na usalama wa kijana huyo.
  2. Awe anafanyiwa uchunguzi wa afya yake, na daktari athibitishe kijana huyo kulingana na umri wake anaweza kuajiriwa katika kazi hiyo.
  • Muajiri ahakikishe kwamba kijana aliyeajiriwa anafanya uchunguzi wa afya yake mara kwa mara mpaka atakapofikia umri wa miaka 21.

Kimsingi haimaanishi kwamba mtoto asifanye kazi yoyote kabisa, hivyo shughuli za nyumbani ni muhimu mtoto kushiriki kwa vile kazi ni sehemu ya makuzi ya binaadamu.
Ajira kwa watoto inayokatazwa ni ile yenye uwezekano wa kumnyima mtoto haki yake ya elimu, kimakuzi katika maeneo ya saikolojia, kimwili, kihisia, kiakili na kimaendeleo.

Kwa vile watoto bado wana akili changa, hufanya maamuzi ambayo huhatarisha maisha yao wakiwa katika ajira, hupenda kujaribu mambo mbali mbali na hata yale ya hatari na hivyo hujikuta wakiumia pale pale au baada ya kipindi kirefu madhara ya kiafya hujitokeza.

Kuna watoto ama kwa kulazimishwa na wazazi/walezi wao au kwa kujishauri wenyewe, hufanya biashara mbali mbali ili wajipatie fedha kwa matumizi yao. Watoto wanawake nao wamekuwa wakibeba majukumu makubwa ya kifamilia kuliko uwezo wao, ukilinganisha na wenzao wavulana, wasichana ndio wahudumu wakuu katika majumba ya watu tofauti, licha ya kulipwa ujira mdogo wamekuwa wakikabiliana na vitendo vingi viovu ikiwwemo kunyanyaswa kijinsia.

Ajira hizi za watoto zimekuwa zikihusisha kuwapatia shughuli ambazo ni nzito sana kwa umri wao. Kama hii haitoshi bado shughuli hizi zinakuwa ktika mazingira magumu na yasiyofaa kwa afya ya mwanaadamu yoyote. Na bila kusahau kuna mamilioni ya watoto wanaofanyishwa kazi ambazo hazifai kwa hadhi ya utu.

Ajira za watoto zinastahili kupigwa vita kila kona duniani kutokana na ukweli kwamba, kwa kutumia umri wao mdogo, waajiri wa watoto hawa huwadanganya na kuwalipa kiasi kidogo sana cha ujira na mara nyengine kutowalipa kabisa.



MADHARA YATOKANAYO NA AJIRA ZA WATOTO.

Ajira za watoto huwa kikwazo kikubwa katika ukuaji wa kimwili, kimaono na kijamii. Ni kutokana na ukweli huu kwamba, athari za ajira za watoto ni kubwa mno, watoto wanathirika kimwili, kisaikolojia, wanakosa haki zao za msingi na mambo mengine mengi, miongoni mwa hayo ni:-

  1. Kukosa elimu. Watoto wengi wanaojiingiza katika ajira za utotoni wanakosa haki yao ya msingi ya kielimu kutokana na ukweli kwamba muda wa kuwepo katika masomo wao wapo katika ajira.
  2. Watoto wanaathirika sana kisaikolojia pamoja na kiafya. Huko kwenye ajira hujifunza na kuiga mambo mengi kama uvutaji bangi, utumiaji wa madawa ya kulevya na tabia mbali mbali zisizoendana na utamaduni wetu.
  3. Ongezeko la watumiaji madawa ya kulevya. Kutokana na watoto kujifunza mambo tofauti wakiwemo kwenye ajira kama vile utumiaji wa madawa ya kulevya, hali hii inapelekea ongezeko la watumiaji wa madawa hayo.
  4. Kuongezeka kwa mimba za utotoni. Kuna baadhi ya watotowakike ambao huajiriwa kwenye ma bar ya usiku, ajira ambayo inahatarisha usalama wa watoto na kupelekea kudhalilishwa kijinsia.
  5. Kuongezeka kwa vifo vya watoto. Kuna watoto ambao huajiriwa katika migodi, ajira ambayo ni hatari kwa watoto, kuna baadhi ya watoto hupoteza maisha yao kwa kuangukiwa na mwamba wa mawe.



CHANGAMOTO

  1. Uwezekano wa kuendeleza mipango ya uondoaji ajira ya watoto katika hali ya umasikini.
  2. Ukimwi unaoacha mayatima na wengine wanaoathiriwa kushindwa kujikimu na hivyo kuingia katika ajira ya watoto.
  3. Umasikini unaopelekea kuzuka kwa watoto wanaohitaji utunzaji maalum wakiwemo watoto walioajiriwa.
  4. Ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu haki za watoto. Kukosekana kwa elimu hii kunapelekea uonevu, afya na usalama duni kwa watoto.
  5. Kutokuheshimiwa kwa haki za msingi za watoto.


SULUHISHO

  1. Mzazi/ mlezi ahakikishe kuwa anawatunza vyema na kuwapatia huduma zote muhimu kwa maisha ya binaadamu na maendeleo yake.
  2. Wazazi waelewe kuwa elimu ndiyo njia pekee na makini katika kuwalinda watoto hawa dhidi ya dhulma wanazokumbana nazo.
  3. Wazazi wafanye jitihada za kuondokana na tatizo la umasikini nchini bila ya kuathiri ustawi wa haki za watoto. Kwa kufanya hivyo tutaondokana na wimbi kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira magumu ambao hulazimika kutumbukia katika ajira mbaya.
  4. Serikali ifuatilie kwa kina ustawi wa watoto na vile vile kuweza kuwathibiti wale wote wanaowatumikisha watoto kwa maslahi yao binafsi.
  5. Jamii nzima, vijana kwa wazee inaweza kufaidika kwa kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa ajira za watoto, hivyo basi nguvu za pamoja zinahitajika kufanikisha hilo.
  6. Kama tunataka mabadiliko katika jamii ni lazima kutambua tatizo lililopo, chanzo cha tatizo hilo kwa kuliweka wazi na kulifanyia kazi.

HITIMISHO

Mtoto ni nguzo muhimu katika jamii hivyo ana haki ya ya kulindwa, kuthaminiwa na kupewa haki zote hali ambayo itaweza kumjenga kimawazo, kifikra na kiakili.Watoto ni hazina kubwa duniani ili hazina hio ionekane kuwa ya manufaa na kutoa mchango muhimu kwa maendeleo ya taifa na dunia kwa ujumla ni muhimu mzazi au mlezi wa watoto hao ahakikishe kuwa anawatunza vyema na kuwapatia huduma zote muhimu kwa maisha ya binaadamu na maendeleo yake.

Vile vile serikali, taasisi zisizo za serikali na jamii kwa ujumla wana jukumu kubwa kuhakikisha ustawi wa watoto  unaendelezwa kwa kupatiwa elimu, afya bora pamoja na mahitaji muhimu ya watoto kwani watoto ni nguvu kazi za baadae.

Mlinde mtoto sasa.
Weka akilini kwamba kumlinda mtoto ni jukumu lako.

IMETAYARISHWA NA
SAFIA SALEH SULTAN
ZLSC – PEMBA.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!