Thursday 19 October 2017

Mishahara itapanda kulingana na uwezo wa serikali

RAIS John Magufuli amesisitiza kuwa serikali yake haina nia ya kutowaboreshea watumishi wa umma mishahara yao isipokuwa inaangalia uwezo iliyonao.


Aidha alisema kwa kuanzia, tayari watumishi wa umma 59,027 wanatarajiwa kurekebishiwa mishahara yao itakayogharimu kiasi cha Sh bilioni 103. Dk Magufuli alitoa kauli hiyo siku chache baada ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi kutoa tamko la kulaani kauli ya Rais Magufuli waliodai aliitoa kwenye mkutano wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kuwa hatopandisha mishahara ya watumishi wa umma.
Akizungumza katika kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru na Maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 18 ya kifo cha Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais Magufuli alisema serikali yake haina nia ya kutoboresha maslahi ya watumishi wa umma, ila inaangalia kwanza uwezo wake.
Akimzungumzia Baba wa Taifa na hoja hiyo ya maslahi ya mishahara, alisema Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiongozi aliyeweka mbele zaidi maslahi ya wananchi wake kuliko maslahi yake na ndiyo maana alipotakiwa ama aache kazi au aongoze chama cha ukombozi cha TANU alichagua kuongoza chama hicho.
“Sasa leo hii sisi viongozi tupo tayari kujipunguzia mishahara yetu ili kusaidia kuboresha huduma za jamii kwa wananchi wetu? Je tuko tayari kupunguza mishahara na marupurupu kwa faida ya wenzetu?” alihoji.
Hata hivyo, alisisitiza serikali inayo nia ya kuboresha maslahi ya watumishi wake na ndiyo maana baada ya kuondoa watumishi hewa takribani 20,000 na watumishi waliokuwa na taaluma feki 12,000 sasa inajipanga kuboresha mishahara ya watumishi hao 59,027.
“Endapo tusingechukua hatua hii kwanza leo hii tungeboresha mishahara na kupoteza zaidi ya Sh bilioni 89 kwa watumishi wasiostahili,” alisema. Katika tamko lao hilo TUCTA walionesha kulalamika na kudai kuwa kauli hiyo ya Dk Magufuli ya kutoongeza mishahara watumishi wa umma haiendani na ahadi aliyoitoa wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi ya mwaka huu.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alisema serikali imeanza kulipa madai ya wafanyakazi ambapo zaidi ya Sh bilioni 70.4 zimeshalipwa ikiwa kama madai yasiyo ya mishahara kwa mwaka wa fedha 2016/17 na kwamba kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu tayari imeshalipa Sh bilioni 37.4.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!