Sunday 1 October 2017

CCM yakanusha Kinana kujiuzulu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepuuza habari zinazoenezwa katika mitandao ya kijamii kuwa Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana amejiuzulu nafasi yake na pia madai kuwa baadhi ya wanachama wake wamefukuzwa.


Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) imefuta uchaguzi wa wenyeviti wa chama hicho ngazi ya wilaya katika wilaya nne nchini mpaka utakapotangazwa upya kutokana na kasorombalimbali. Hayo yalisemwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
Polepole akizungumza kwenye mkutano huo alikanusha taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Kinana ameandika barua ya kujiuzulu. “Taarifa hizo si za kweli, Katibu Mkuu Kinana anasimamia matibabu ya mmoja wa ndugu zake wa karibu,” alisema Polepole. Aidha aliwaambia waandishi wa habari kuwa pia si kweli kwamba wapo wanachama waliofukuzwa na chama hicho, kama inavyovumishwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kwa siku tatu sasa.
Kuhusu wilaya ambazo uchaguzi wake umefutwa, Polepole alizitaja wilaya hizo kuwa ni Makete, Moshi Mjini, Hai na Siha. Alisema wagombea katika wilaya hizo walikuwa na kasoro nyingi za kimaadili, kikanuni na walikuwa na viashiria hatarishi kwa chama. Uchaguzi huo ambao utafanyika Oktoba 5 na 6, mwaka huu, pia hautazihusu Wilaya za Musoma Mjini na Musoma Vijijini.
“Halmashauri Kuu imeelekeza kuundwa kwa wilaya za kichama mbili katika wilaya ya kiserikali ya Musoma, hivyo kwa sasa Wilaya ya Musoma ya Kiserikali itakuwa na wilaya za kichama ambazo ni Musoma Mjini na Musoma Vijijini,” alieleza Polepole. Kwa maamuzi hayo ya CCM, uchaguzi kwa nafasi ya mwenyeketi wa chama, nafasi ya mwenezi na viongozi wote wa wilaya pamoja na chaguzi za jumuiya kwa Wilaya za Musoma Mjini na Musoma Vijijini, zitatangazwa tena ili wana CCM kutoka Wilaya ya Musoma waweze kutumia haki yao ya kupata viongozi katika wilaya hizo.
Polepole alieleza kuwa zaidi ya wana CCM 1,400 walijitokeza kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo, lakini majina yaliyopitishwa ni 161. CCM kimewataka wagombea hao kuzingatia kanuni ya uongozi na maadili ya CCM, kanuni ya uchaguzi, Katiba ya CCM ambayo inasisitiza nidhamu ya chama katika uchaguzi. Polepole alisema kuwa vitendo vyovyote vinavyokiuka taratibu hizo ikiwemo kutoa na kupokea rushwa, chama kitafuta chaguzi hizo na kuwachukulia hatua kali wahusika ikiwemo kufukuzwa chama.
“Pia chama kinasisitiza kama sehemu ya mabadiliko ya Katiba ni mtu mmoja kofia moja, mwana CCM mwenye kofia zaidi ya moja ajitafakari. “Wapo ambao wamechaguliwa kama wenyeviti wa kata, serikali za mitaa, wale watakaopewa dhamana ya juu kwenye uchaguzi ujao, watalazimika kuachia nafasi zao za awali na kubakia ili kuendelea kuzingatia msingi wa mtu mmoja kofia moja,” alisisitiza Polepole.
Alisema Kanuni ya uchaguzi ya CCM kifungu cha 28 inaeleza kuhusu malalamiko ya uchaguzi kabla, wakati wa vikao vya uchaguzi au baada ya uchaguzi na kinawataka wale wasioridhika kutoa taarifa mara moja wakati uchaguzi unaendelea au si zaidi ya wiki mbili baada ya uchaguzi ili haki itendeke.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!