SERIKALI imewazawadia na kuwatunuku cheti cha ushujaa watu watatu, waliojitolea kuokoa maisha ya wananchi wenzao, walipokumbwa na dhoruba kwa vyombo walivyokuwa wakisafi ria kuzama, akiwamo mwanafunzi aliyeokoa wenzake tisa baada ya mtumbwi kupinduka.
Tuzo hizo zimetolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa niaba ya serikali ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Usafirishaji Majini. Siku hiyo ilifanyika kitaifa mkoani Kigoma, ambako watu hao walipewa vyeti vya heshima, kutambua mchango wao sanjali na Sh milioni moja kila mmoja.
Miongoni mwa waliopewa tuzo hiyo ya ushujaa ni Mjaka Fakhi Hassan, ambaye alitumia muda wa saa 10 kuogolea baharini katika mkondo wa Nungwi kisiwani Unguja na kufanikiwa kuwaokoa watu watano, ambao mtumbwi waliokuwa wakisafiria ulipigwa dhoruba na kupinduka.
Pia tuzo hiyo ilitolewa kwa Leonald Sudi ambaye ni Kiongozi wa kundi la uokoaji la Aqua Lodge mjini Kigoma, aliyewaongoza wenzake Mei 2015 na kufanikiwa kuokoa familia ya watu 35, waliokuwa wakienda kwenye harusi na mtumbwi waliokuwa wakisafiria kupigwa dhoruba katika eneo la Mlima Nondwa mkoani Kigoma.
Pamoja na hayo tuzo hiyo, pia ilitolewa kwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Butwa wilaya ya Geita mkoani Geita, Tisekwa Gamungu ambaye Mei mwaka huu, aliwaokoa wanafunzi wenzake tisa baada ya mtumbwi wao kupinduka walipokuwa wakielekea shuleni.
Akikabidhi tuzo hizo na fedha taslimu, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga alisema ni heshima kubwa kuwatunuku watu waliojitolea maisha yao kwa ajili ya wengine na kwamba uzalendo huo unapaswa kujengwa kwa Watanzania wote.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ulinzi, Usalama Majini na Mazingira katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Stella Katondo alisema tuzo hizo zitaendelea kutolewa kila mwaka katika maadhimisho hayo ili kuenzi na kuheshimu mchango unaotolewa na watu mbalimbali katika sekta ya usafirishaji majini nchini.
No comments:
Post a Comment