Saturday, 9 September 2017

Mawaziri wang’oka


BARAZA la Mawaziri la Rais John Magufuli limetikisika tena baada ya Waziri na Naibu Waziri kung’oka kutokana na matokeo ya ripoti ya kamati mbili maalumu za Bunge zilizochunguza biashara ya madini ya tanzanite na almasi nchini.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani, wameamua kujiuzulu kupisha uchunguzi wa vyombo vya dola, saa chache baada ya Rais Magufuli kuwataka wakae pembeni.
Miezi michache iliyopita, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alifutwa kazi baada ya ripoti za kamati mbili za Rais za kuchunguza makinikia kuwatia hatiani watendaji wa serikali wakiwamo mawaziri, kushindwa kuzuia wizi mkubwa wa fedha za umma katika usafirishaji wa makinikia nje ya nchi.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kupokea ripoti mbili za Kamati za Bunge zilizoundwa na Spika Job Ndugai kwa ajili ya kuchunguza biashara ya almasi na tanzanite nchini, Rais Magufuli aliwataka wateule wake wote waliotajwa kwenye ripoti hizo kujiuzulu ili kupisha uchunguzi.
Aidha, pamoja na kubainisha kuwa hawezi kuingilia mhimili mwingine unaojitegemea kufanya kazi yake, alimshauri Ndugai kutumia Kamati ya Bunge ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge, kuwajadili na ikiwezekana kuwachukulia hatua wabunge wanaotajwa mara kwa mara katika matukio ya kuhujumu uchumi wa nchi.
“Lakini kwenye taarifa hii, wapo watu wametajwa na wengine mimi nilihusika kuwateua, sasa ukishatajwa tajwa, inawezekana uko so much clean, lakini umetajwa, inawezekana wewe ni mchapakazi kweli, mpole tena handsome kweli, lakini umetajwa tena na wabunge…” “Nafikiri Zungu (Mussa, Mbunge wa Ilala), Ndasa (Richard, Mbunge wa Sumve), Silinde (David, Mbunge wa Momba), Kiula (Allan, Mbunge wa Iramba Mashariki), Adadi (Balozi Rajab, Mbunge wa Muheza), Dotto (Biteko, Mbuge wa Kasulu Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya tanzanite), Spika Ndugai aliyepokea ripoti hawawezi kumuonea mtu, sitaki kuamini kwamba kuna wabunge wanaweza kumuonea mtu, kwani hawa wameapa kuilinda nchi,” alisema.
Alisema kwa sasa yeye ndiye aliyewateua na kwa vile ripoti zote mbili wametajwa mara kadhaa ni vyema wakajiweka pembeni na kupisha vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi yake haraka. Alisema waliotajwa wote kwenye ripoti hizo wenye hadhi ya waziri, naibu waziri, katibu mkuu, katibu tawala wa mkoa, mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa wilaya wajiweke pembeni kwanza kupisha uchunguzi zaidi.
“Najua mmenielewa, nazungumza haya si kwa sababu nawachukia watu, lakini tukienda kwa utaratibu huu, nchi itasimama imara, tunaibiwa mno, ni maajabu saa nyingine wanaohusika ni watendaji wetu,” alieleza na kuongeza kuwa japokuwa suala la mfumo linaweza kuwa sababu ya matatizo hayo, lakini zilikuwepo njia ambazo viongozi hao wangeweza kuzichukua kunusuru hali halisi.
Simbachawene, Ngonyani Simbachawene ambaye ni Mbunge wa Kibakwe mkoani Dodoma, alitangaza kujiuzulu uwaziri jana saa 8:07 mchana, akisema amechukua uamuzi huo ili kupisha uchunguzi. Alimshukuru Rais Magufuli kwa kumpa heshima ya kuwa waziri katika baraza lake na kusema kwamba kujiuzulu kwake, pia ni kutunza heshima ya uteuzi huo. Simbachawene ametajwa katika sakata la kuridhia mabadiliko katika ubia wa kampuni zilizokuwa zikifanya kazi kwa ubia na serikali katika madini ya tanzanite.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Tamisemi mkoani Dodoma, alisema, “Nimeamua kujiuzulu baada ya kusikiliza hotuba ya Rais baada ya kukabidhiwa ripoti ya kamati teule za Bunge kwamba wateule wake waliotajwa wakapisha uchunguzi...” Alisema anamshukuru rais kwa kumweka katika wizara nyeti na kusema ataendelea kumsaidia katika ujenzi wa Taifa; na kwamba Rais anastahili kusaidiwa kwani anapofanya mabadiliko makubwa kwa maslahi ya taifa kuna watu wataumia.
“Jambo la msingi hapa si ubinafsi, bali uhai wa taifa na watoto wetu,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa hakuna maana ya cheo chake kama nchi inateketea na kuongeza kuwa wapiga kura wake na marafiki wasichanganyikiwe katika hilo kwa kuwa nchi ni bora zaidi kuliko yeye. Aliahidi kuendelea kuwatumikia wananchi waliomchagua, kutumikia serikali na kusema siyo tu cheo cha uwaziri anachoweza kuachia, bali hata roho yake iwe ibada na sadaka kwa manufaa ya Taifa hili kama ikibidi.
Ngonyani Kwa upande wake, Naibu Waziri Ngonyani alisema ameamua kujiuzulu na sasa ni Mbunge wa Namtumbo na kwamba anajisikia vizuri katika hilo. “Nimeamua kukaa pembeni kupisha uchunguzi, lakini siyo tu kupisha uchunguzi, lakini pia kuna msemo wa mke wa mfalme akishatuhumiwa ni tatizo, hivyo inabidi mke atolewe ili mfalme aweze kutawala vizuri.
“Leo (jana) niliingia bungeni kama Naibu Waziri, lakini kesho (leo) nitaingia kama mbunge wa kawaida na katika hilo najisika huru kabisa,” alisema Ngonyani ambaye ametuhumiwa akiwa Stamico, kuizuia serikali kununua mgodi wa almasi kwa dola milioni 10 na kuikosesha serikali zaidi ya dola milioni 300, fedha ambazo zilienda kwa kampuni iliyonunua hisa.
Mbunge huyo wa Namtumbo mkoani Ruvuma, alisema ameandika barua ya kujiuzulu na amekabidhi kwa Katibu Muhtasi wake anaamini itafikishwa inakotakiwa kufika na kwamba nakala nyingine ataituma kwa njia ya barua pepe. Maswi Akizungumza kwa simu na gazeti hili, Maswi aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini ambaye sasa ni Katibu Tawala Mkoa wa Manyara, alijibu kwa kifupi, “sina cha kuzungumza kwa sasa, subiri.”
Maswi anatajwa kuwa alienda katika mgodi wa almasi na kueleza kwamba alipatwa na hasira baada ya kutoka na kujionea madudu na kuapa kutokanyaga tena, kulielezwa na kamati hizo kuwa moja ya sababu ya watendaji kuacha mambo yakiharibika. Akifafanua zaidi hotuba yake, Rais Magufuli alisema, “Nasikia kuna mtu alienda mahali akakuta hali ya hovyo akachukia sana akarudi na kuendelea na shughuli zake. Sasa kama umekuta ya hovyo kwa nini unachukia tu huchukui hatua? Sasa nyie kamati kama mliyoyakuta huko mngekaa tu mkachukia, Spika nawe ungechukia baada ya kujua, nani angechukua hatua? Tufike mahali tuweke maslahi ya nchi mbele.”
Alisema kazi yake ya urais na maisha anayoishi sasa ni ya muda tu, ila ilimuumiza alipoingia na kukuta mambo ya ajabu na mengine ya aibu yakiendelea. “Mengine ni aibu hata kuyataja na watu walikuwepo, lakini sitaki na mimi nikae waje waseme walikuwepo,” alieleza. Alimshauri Spika Ndugai kutumia mamlaka aliyonayo kupitia Kamati ya Maadili ya Bunge na kuwajadili wabunge wote wanaoendelea kutajwa kwenye kashfa mbalimbali zinazoibuka nchini kwani kuendelea kwao kuwepo bungeni ni aibu kwa chombo hicho.
“Wapo wabunge wamekuwa wakitajwatajwa kwenye kashfa hizi, likitajwa hili yupo, lile yupo, lakini wapo tu bungeni tena wakichangia hadi mishipa inawasimama, na watu wanawajua, hii ni aibu kwa Bunge ambalo lina wabunge makini kabisa,” alisema. Pamoja na hayo, alimuunga mkono spika huyo kwa nia yake ya kutaka kuviandikia vyama vyote vya siasa ambavyo wabunge wake wamekuwa wakitajwa kwenye kashfa hizo kupitia aina ya viongozi inaowachagua kuongoza wananchi.
“Mimi hapa kwa kweli ni Mwenyekiti (wa CCM) kwa hiyo wabunge wa namna hiyo wanaotajwa tajwa usisite kuandika na matatizo yao, sisi huwa tuna taratibu zetu tunaweza kuwaonya, kuwajadili labda watajitetea, lakini chama kitafuata taratibu zake,” alisema Rais Magufuli. Miongoni mwa wabunge waliotajwa ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM) na Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (CCM).
Avikabidhi vyombo vya dola Aidha, Dk Magufuli alitumia fursa hiyo, kuvikabidhi ripoti hizo vyombo vya ulinzi na usalama, vikiwemo Polisi, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na kuviagiza kuanza kuchukua hatua mara moja dhidi ya wote waliotajwa kwenye ripoti hizo. Alivitaka vyombo hivyo kutosita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kuchezea rasilimali za nchi lakini pia alivihimiza vyombo hivyo vianze kujipanga namna ya kuilinda rasilimali ya nchi.
“Kwa hawa waliotajwa, nitashangaa sana ikifika hadi wiki ijayo sijasikia mtu kakamatwa, naomba mfanyekazi yenu kwa haraka na mchukue hatua stahiki,” alisisitiza. Wakati akikabidhi ripoti hizo, alisema muda wa miaka 50 umeshapita huku nchi ikiibiwa. “Mimi nimekuja kufanyakazi tumecheza sana kwa miaka 50 sasa, sasa sikuja hapa kutafuta mchumba, nafanyakazi, nikimaliza ndipo watakuja wale wanaotafuta wachumba, potelea mbali sitaki kuwa mwanasiasa maarufu,” Aidha, alimuagiza Waziri Mkuu na mamlaka husika kuhakikisha zinapitia sheria za madini yote nchini na kuzifanyia marekebisho yanayotakiwa ili kuweza kuokoa rasilimali hiyo isiishie mikononi mwa wachache kwa kigezo cha matatizo ya sheria hizo.
Ndugai awachongea wabunge Awali, Ndugai wakati akizungumza katika hafla hiyo, alisema ripoti hizo zimewataja wanasiasa wakiwemo wabunge na wengine walipata fursa ya kuwa mawaziri. Alisema ofisi yake inaangalia namna ya kuandikia barua vyama vya siasa vyenye wabunge wanaotajwa mara kwa mara kwenye matukio ya kashfa ili kuvikumbusha juu ya aina ya viongozi wanaochagua kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.
“Juzi Lipumba (Mwenyekiti wa CUF) alitutolea majina mapya, nimewaapisha tayari, wakiletwa wengine nitawaapisha,” alisisitiza. Majaliwa Naye Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alishukuru ofisi ya Bunge kwa kuunda kamati hizo ambazo zimebaini madudu mengi yakiwemo masuala ya wizi, rushwa na ufisadi katika sekta ya madini na kuahidi serikali itawachukulia hatua wale wote watakabainika kuhusika. “Kamati imebaini mambo mengi ya hovyo, uzembe, rushwa na wizi, wapo waliotajwa wako kwenye ngazi ya rais na wengine wako ngazi ya wizara, serikali itatekeleza yale yote yaliyoshauriwa na kamati hizi. Pale itakapothibitika kuwepo kwa wizi, uzembe na rushwa hatua zitachukuliwa,” alisisitiza.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!