Friday, 29 September 2017

Majambazi wapora msikitini, wamjeruhi mlinzi kwa panga


WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wamevamia Msikiti Mkuu wa Ijumaa ulioko Kata ya Igunga Mjini wilayani hapa mkoani Tabora, kisha kumjeruhi mlinzi na kupora baadhi ya vitu ikiwemo vitabu vya dini ya Kiislamu.


Mlinzi aliyejeruhiwa ni Juma Mussa (55), mkazi wa Mtaa wa Nkokoto kata ya Igunga ambaye amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga na hali yake bado ni mbaya. Mkuu wa Wilaya ya Igunga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, John Mwaipopo alithibitisha kutokea kwa uhalifu huo na mtuhumiwa mmoja amekamatwa pamoja na vitu vilivyoibwa.
Alimtaja mtuhumia huyo kuwa ni Juma Mponi (45) ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Stendi ya Mabasi mjini Igunga, na kutamba kuwa hakuna jambazi atakayetoka salama Igunga kwa kuwa polisi wamejipanga kikamilifu kukabiliana na matukio kama hayo.
Akizungumza kwa shida akiwa wodini, mlinzi huyo alisema shambulio hilo limetokea Septemba 25, mwaka huu saa 8 usiku, ambako watu hao walifika msikitini hapo kisha kurusha jiwe kwenye eneo alilokuwa amekaa.
Alisema baada ya kuona jiwe hilo, aliamua kusimama na mara jambazi mmoja aliruka uzio wa msikiti kisha akaingia na kuanza kumshambulia kwa mapanga kichwani. Alibainisha kuwa wakati akishambuliwa, aliona majambazi wengine wakifungua milango ya msikiti na mmoja wao akimweleza mwingine “wewe maliza kabisa huyo mlinzi.”
Hata hivyo, mlinzi huyo aliendelea kuuomba msaada kwa kupiga kelele ili asaidiwe, hali iliyowafanya majambazi kukimbia kusikojulikana wakiondoka na baadhi ya mali za msikiti. Mhasibu wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa, Issa Said Feruzi alitaja vitu vilivyoibiwa na majambazi hao kuwa kuwa ni misahafu minne, feni moja, saa kubwa, vitabu vya hitima 30, kitabu cha mapato na matumizi, daftari za Tabligh nne, maikrofoni na stendi yake, miswala miwili; vyote vikiwa na thamani ya Sh 374,000.
Hata hivyo, alisema vitu vyote vimepatikana na viko Kituo cha Polisi Igunga; huku Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Melchades Magongo amekiri kumpokea Juma Mussa, akieleza kuwa alimpokea hospitalini hapo akiwa na majeraha kichwani ambayo yanaonesha alikatwa na kitu chenye ncha kali. Dk Magongo alisema hali ya mlinzi huyo bado si nzuri akiendelea kupatiwa matibabu zaidi katika wodi namba nane hospitalini hapo

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!