Thursday, 17 August 2017

Jamii ishirikishwe katika kupambana na kifua kikuu

Image result for kifua kikuu
Afya ya jamii ni miongoni mwa mihimili ya maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.
Kila inapobidi, ni vyema kuhakikisha mipango ipo tayari kukabiliana na mlipuko wowote unaoweza kuhatarisha ustawi huu.


Kwa magonjwa ya muda mrefu, bado mipango inahitajika kufanikisha hilo. Kwa kutambua umuhimu wa kuishirikisha jamii, Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI) ilifanya tamasha huko Zinga kwa Mtoro, mjini Bagamoyo, mkoani Pwani kuihamasisha kukabiliana na kifua kikuu.
Hilo lilifanywa kwa ufadhili wa asasi isiyo ya kiserikali ya TB Alliance.
Kitengo cha Ushirikishaji Jamii cha IHI Bagamoyo kilishirikiana na Bodi ya Ushauri wa Jamii (CAB) wilayani humo kuandaa tamasha hilo licha ya kuburudika kwa mashindano ya mpira wa miguu, washiriki walijifunza mambo mbalimbali kuhusu TB kutoka kwa wataalamu wa IHI juu ya kinga na tiba ya ugonjwa huo.
Mratibu wa Ushirikishaji Jamii wa IHI wilayani Bagamoyo, Dk Omary Juma anasema uhamasisha wa jamii kuhusu masuala ya afya unasaidia kufanikisha utafiti na kuongeza uelewa wa kujikinga hata kukabiliana na maradhi yanayoweza kujitokeza.
“Kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na kuwahusisha wananchi, kumekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha utafiti wa malaria na kifua kuu,” anasema.
Tamasha hilo lilihudhuriwa na wataalam wa IHI, viongozi wa serikali ya mtaa, wanachama wa CAB na maofisa wa afya wa Kata ya Zinga iliyopo kilometa 15 kusini mwa Bagamoyo.
Lilikuwa ni sehemu ya uhamasishaji wa jamii juu ya hatua wanazopaswa kuchukua kuzuia maambukizi ya kifua kikuu na jinsi ya kukabiliana nao pindi wanapoupata.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeiorodhesha Tanzania miongoni mwa nchi 30 duniani zilizobeba ‘mzingo mzito’ wa ugonjwa wa TB kwa sasa.
Burudani na elimu
Diwani wa Kata ya Zinga, Mohammed Mwinyigogo anasema licha ya kuwachangamsha wananchi, mtindo huo wa utoaji elimu ni rahisi kueleweka kwa walengwa.
“Tunafuraha kupata fursa hii. Tumejifunza mengi kuhusiana na kinga dhidi ya TB. Ujumbe uliotolewa umewafikia hata vijana walioshiriki michezo na burudani mbalimba,” anasema Mwinyigogo.
Licha ya mchezo ya mpira wa miguu, kulikuwa na burudani ya muziki uliokuwa na ujumbe ulijikita kutahadharisha jamii kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu . Ulielimisha kuhusu dalili zake, jinsi unavyo ambukiza, namna ya kujikinga na matibabu yavyopatikana kwa walioambukizwa.
Kabla washindi hawajakabidhiwa zawadi zao, wanasayansi wa IHI walitoa ujumbe mahsusi kuhusu TB, huku wakisisitiza umuhimu wa kubaini dalili zake, namna ya kujikinga na jinsi jamii inavyoweza kushiriki kuutokomeza.
Ushiriki kutokomeza TB
Taasisi ya Afya Ifakara inafanyakazi kwa karibu na serikali kupitia Wizara ya Afya ili kuwezesha utekelezaji wa mpango mkakati wa Taifa wa afya.
Ushirikiano wa karibu baina ya serikali na IHI tangu taasisi hiyo ilipoanzishwa zaidi ya miaka 50 iliyopita, umeiwezesha kupata mafanikio kwenye kuchangia mabadiliko ya sera na kuinufaisha jamii moja kwa moja kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa.
Kwa kujisogeza karibu na wananchi, kumesaidia kuibua changamoto za afya kwenye jamii husika, kurahisisha kufanya utafiti na kurudi kutoa mrejesho wa matokeo moja kwa moja.
Katika maadhimisho ya Siku ya TB Duniani mwaka huu, WHO inazitaka nchi na wadau wa afya kuungana kutokomeza kifua kikuu.
Shirika hilo linaamini ‘mafanikio ya kutokomeza TB yanaweza kupatikana kwa ushirikiano mkubwa wa serikali, jamii na wadau kutoka asasi za kijamii na watafiti.’
Kwa sasa, shirika hilo na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, wanatekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambayo ynasisitiza kutokomeza TB ifikapo mwaka 2030.
Ingawa zaidi ya watu milioni 43 wamepona maradhi hayo tangu mwaka 2000, mapambano dhidi ya ugonjwa huo unaoambukiza yanapaswa kuendelea kwa sababu ushindi uliopatikana hautoshi na ni kama nusu.
Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 4,000 wanapoteza maisha kila siku kutokana na ugonjwa huu na nchi nyingi ambazo watu wake wanaathiriwa zaidi ni maskini hasa zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo.
WHO linasisitiza, ugonjwa wa TB utatokomezwa kwa ushirikiano wa wadau wote, zikiwemo serikali, asasi za kiraia, watafiti, sekta binafsi na wahisani. Hii ina maanisha kuwa mwelekeo unaopaswa kuchukuliwa ni ule wa mapambano yanayohusisha wadau wote muhimu.
Katika mkakati w akupambana na maradhi hayo, Serikali inatoa vipimo na matibabu bure kwa wananchi wote kwenye vituo na hospitali za umma zilizopo maeneo tofauti nchini.
Hiyo ni moja ya mikakati ya kukabiliana na maradhi hayo hasa kw akutambua kwamba imo miongoni mwa mataifa 30 yaliyoathirika zaidi na TB.
Kwa mujibu wa WHO, nchi hizo 30, zina zaidi ya asilimia 85 watu wote wenye maambukizi.
WHO inasema nchi nyingi zimeimarisha uhamasishaji na kuboresha mipango ya kupambana na ugonjwa huu kwa kuanza kutumia zana mpya, kupanua huduma za afya na kupunguza gharama za tiba kwa wagonjwa.
“Nchi nyingine zinashirikiana na watafiti kuongeza kasi ya uchunguzi, upatikanaji wa dawa na chanjo,” taarifa ya WHO inasema.
Tanzania
Miongoni mwa nchi 30 ambazo WHO inasema zina maambikizi makubwa ya TB, Tanzania miongoni.
Nchi 20 zilizoathiriwa zaidi na ugonjwa huo kwa mujibu wa shirika hilo ni Bangladesh, Brazil, China, Korea, DRC, Ethiopia, India, Indonesia, Kenya, Msumbiji, Myanmar na Nigeria.
Nyingine ni Pakistan, Papua New Guinea, Philippines, Urusi, Afrika Kusini, Thailand na Vietnam. Tanzania ipo kwenye orodha hii.
Nchi nyingine 10 ambazo pia zipo kwenye orodha hiyo kwa kuwa na wagonjwa wengi wenye TB waliobainika ni Angola, Cambodia, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo, Lesotho, Liberia, Namibia, Sierra Leone, Zambia na Zimbabwe.
Miongoni mwa maeneo yanayohitaji kupewa msukumo mkubwa ni kuongeza uhamasishaji wa wananchi kupima afya zao ili kubaini kama wameambukizwa au la.
Wariathirika wakianza matibabu hupunguza uwezekano wa kuambukiza wengine hivyo kuongeza mapambano kabla viwango hivyo havijashuka.
Takwimu zinaonyesha TB ni ugonjwa wa tatu kwa kusababisha vifo nchini ukiwa nyuma ya malaria na Ukimwi.
Kwa miaka mitano mfululizo iliyopita, wagonjwa 65,000 wamekuwa wakibainika hivyo kuiweka Tanzania juu ikilinganishwa na nyingine

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!