Tuesday 6 June 2017

Neno la leo toka kwa Maggid Mjengwa


Neno La Leo; Jua Linapozama Afrika...

Ndugu zangu,

Kwa mwanadamu, mila yake ndio dini yake ya kwanza. Kwa Mwarabu na Mzungu sawia, Uislamu na Ukristo uliingia katika jamii hizo na kuzikuta jamii hizo zikiwa na mila zao.


Na sisi Waafrika vivyo hivyo, tuna mila zetu. Uislamu na Ukristo ni imani za kimapokeo. Hakuna dhambi kwa mwanadamu kupokea imani mpya. Hata hivyo, ni vema kwa anayeipokea akawa pia amejitambua, kuwa naye pia ana mila zake. Na mwanadamu anayeikana asili yake ni mtumwa.

Uafrika ni imani. Uafrika umejijenga katika upendo na ujamaa. Ndio maana Mwalimu aliijenga TANU na nchi yetu katika misingi ya Ujamaa wa Kiafrika, hivyo basi itikadi. Ni tofauti kabisa na Ukomunisti.

Mathalan, Afrika unapokuwa safarini na jua likazama, basi, Mwafrika hutafuta yalipo makazi ya watu. Afrika safari zetu nyingi ni za miguu, na kwa kawaida hatutembei usiku.

Na jua likizama na ukakutana na Mwafrika mwenzako kwenye mji wake, husemi kuwa unataka kusaidiwa pa kulala na mengineyo. Kwa mila zetu, utasema;

" Mwenzenu niko safarini na jua limezama nikiwa hapa".

Kwa Mwafrika, hapo umehitaji msaada. Mwenyeji ataandaa pa wewe kulala. Utaandaliwa chakula na hata maji ya moto ya kuoga. Atakayefanya ukarimu huo hatajali kama wewe ni Mkristo, Muislamu, au wa kabila tofauti na yeye. Atafanya hivyo kwa vile wewe ni mwenzake katika ubinadamu na Uafrika.

Na asubuhi kukipambazuka, utapewa kijana wa kukusindikiza kilomita kadhaa. Uendelee na safari yako. Ndio, Uafrika ni imani iliyojengeka katika misingi ya upendo, umoja na kusaidiana bila kubaguana.

Na katika hili la misuguano ya kiimani kwenye jamii. Misuguano inayotokana na dini hizi za kimapokeo; Uislamu na Ukristo. Imefika mahali, kwa makusudi kabisa, tuandae mitaala ya kufundisha mashuleni maarifa ya imani tofauti za humu duniani.
Dini nyingi za dunia hii zina mengi yenye kufanana. Mathalan, dini zote kwa maana ya dini zinahubiri amani, upendo, usawa na mshikamano kwa wanadamu wote. Yenye kuhubiri tofauti na hayo, yumkini si dini za kweli.

Huko mashuleni watu wote wafundishwe, na waalimu mahiri, juu ya masuala ya imani za humu duniani, ikiwamo dhana ya Uafrika kama imani pia.

Maana, mingi ya misuguano hii ya kidini inatokana na watu kukosa maarifa, au kuwa na maarifa haba sana.

Naam, Afrika jua linapozama unamtafuta Mwafrika mwenzio, bila kujali dini au kabila lake.

Ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!