Monday, 1 May 2017

Tembelea Rubondo, hifadhi yenye upekee ziwani Victoria

IDADI ya watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Visiwa cha Rubondo imeongezeka. Imetoka watalii 452 kwa mwaka katika kipindi cha Julai 2005 hadi Juni 2015. Kati ya hao, wageni kutoka nje walikuwa wastani wa 380 na wa ndani ni 72.


Hivi sasa, lipo ongezeko kutokana na wastani wa watalii 879 kwa mwaka idadi ambayo imepatikana kutoka Julai 2015 mpaka Juni 2016. Kati ya hao, 525 ni watalii wa nje na 354 ni wa ndani.
Miongoni mwa mambo yaliyowezesha ongezeko ni pamoja na hatua ya uongozi kuitangaza hifadhi hiyo hasa kupitia mitandao ya kijamii. Uwapo wa migodi mingi katika Kanda ya Ziwa, ni kichocheo kingine cha ongezeko la watalii.
Migodi hiyo ni mgodi wa dhahabu wa Geita, Kahama na Buzwagi. Baadhi ya watumishi wa migodi hiyo, wakiwemo wageni hutumia muda wa mapumziko kutembelea hifadhi hiyo.
Aidha, kitendo cha wataalamu wa wanyamapori kutoka Ulaya la kuwafundisha Sokwe mtu waliopo hifadhini kuzoea binadamu, ni miongoni mwa vivutio vya watalii wengi katika hifadhi hiyo.
“Rubondo ni nyumbani kwa aina pekee ya mnyama Nzohe hapa Tanzania wenye asili ya Afrika Kusini, ndege aina 400, samaki aina 13, Sokwe mtu wa asili ya Afrika ya Magharibi na misitu minene mikubwa ya asili ya Kongo,” anasema Gara. Hifadhi ya Rubondo inasifika pia kwa utajiri wa aina mbalimbali za samaki.
Wanapatikana sato, sangara, ngege, mbiru, furu, ningu, kuyu, mbofu au hongwe, domodomo au mbete, soga, gogogo, kambale mumi, kambale mamba au kamongo, na dagaa.
“Baadhi ya aina samaki wanakuwa wakubwa hadi kufikia hadi kilo miamoja,” anasema mhifadhi huyo. Rubondo pia ni makazi ya ndege wa aina mbalimbali hususani zumbuli, chechelee na taisamaki.
Zipo fukwe zilizojaa rasilimali za uoto wa asili wenye harufu nzuri ya kipekee. Lipo eneo la kulala watalii ambalo pia linatajwa kuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vinavyofanya watalii wengi wa nje na ndani kutembelea hifadhi hii.
Vile vile yapo malisho, maji, matunda asilia, vipepeo, wadudu na mbegu za nafaka asilia kwa mwaka mzima. Akielezea historia ya Hifadhi ya Taifa ya visiwa vya Rubondo Gara amesema wakazi wake waliojulikana kama Banyarubondo ambao walilazimika kuondolewa 1964 ili kupisha hifadhi kutokana na tangazo la waziri mwenye dhamana ya masuala ya maliasili.
Kazi ya kuwaondoa wananchi hao ilikamilika mwaka 1965 baada ya wananchi hao kulipwa fidia na mwaka uliofuata (1966) Rubondo ilitangazwa kama pori la akiba na miaka 10 baadaye, yaani mwaka 1977 ikapandishwa daraja na kuwa hifadhi ya taifa.
Inaelezwa kwamba, uamuzi huu wa serikali wa kuanzisha hifadhi hiyo ulichangiwa pia na matokeo ya utafiti uliofanywa na Shirika la Frankfurt Zoological Society la Ujerumani lililobaini hatari ya baadhi ya wanyama kutoweka duniani wakiwemo wanaopatikana katika kisiwa hicho.
Muikolojia wa hifadhi, Wickson Kibasa anasema miaka ya 1960, dunia ilianza kupata wasiwasi kuwa baadhi ya wanyama wangeweza kutoweka dunia. Hivyo, wataalamu wa Ikolojia waliangalia uwezekano wa kuhamisha baadhi ya wanyama kama sokwe mtu, tembo na wengine kuwapeleka nchi za Ulaya .
Lakini baada ya kufananisha/kulinganisha uhalisia wa mazingira na uoto wa asili wa Afrika Mashariki wakapendekeza sehemu pekee duniani ya kuhifadhi wanyama hao na wanapoweza kuishi sawa na maeneo yao ya asili ni Rubondo.
Kibasa anasema wakati katika maeneo mbalimbali ya hifadhi barani Afrika, baadhi ya wanyama kama tembo wanapotea kwa ujangili, hali ni tofauti katika hifadhi ya Rubondo. Kila mwaka tembo waliopandikizwa wanaongezeka na wanyama kama, twiga, sokwe mtu, nzohe, ngedere weusi, weupe, mamba na viboko na wanyama wengine walipandikizwa Rubondo wanaongezeka.
Mkuu wa Hifadhi, Gara, anasema, “Ili kuondoa changamoto za uvamizi, ujangili na uharibifu wa mazingira hifadhi imejikita katika kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa namnukuu: “Kutoa elimu ya uhamasishaji wa jamiii kulinda na kuheshimu mipaka yote ya vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi nchini kwa lengo la kuondokana na migogoro mingi iliyokuwa ikijitokeza baina vijiji vya jirani na hifadhi”.
Waziri Mkuu alitoa maagizo alipokuwa kwenye ziara mkoani Manyara hivi karibuni. Alisisitiza utakelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuongeza na kuboresha mazalia ya samaki katika maeneo oevu au chepechepe ili kuwaletea wananchi uhakika wa chakula na kipato.
Kitengo cha ujirani mwema cha Rubondo kinatoa elimu ya uhifadhi katika jamii zinazopakana na hifadhi, kupitia elimu hiyo wananchi wamekuwa wakielimishwa kuhusu madhara ya uvuvi haramu katika Ziwa Victoria.
“Wanaelimishwa pia mbinu za uvuvi endelevu ndani ya ziwa”, anasema David Kadomo, ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ujirani mwema.
Kadomo anasema: “Hifadhi kwa kushirikiana na maofisa uvuvi katika wilaya zinazopakana na hifadhi yetu, tumekuwa tukiwaelimisha wananchi na kuhimiza utunzaji wa ardhi oevu kwenye mialo za Ziwa Victoria”.
Akifafanua mkakati huo, Kadomo anasema hifadhi imeandaa mpango kwa kushirikiana na wananchi katika mialo ya Bulongero kata ya Izumacheli wilaya ya Geita, Kabiga kata ya Maisome wilaya ya Sengerema, Kasenyi kata ya Ikuza wilaya ya Muleba na Mwerani kata ya Mganza wilaya ya Chato katika kuboresha na kuongeza vituo vya mazalia ya samaki katika mialo hiyo.
Matarajio ya hifadhi ni kuboreshwa kwa mazalia ya samaki na kuanzisha vituo mbalimbali kando mwa ziwa ili, wananchi kuzalisha samaki kwa wingi kama azma ya serikali ilivyokusudia na kuondoa changamoto ya kutoweka kwa samaki wenye uzito mkubwa unaotakiwa viwandani.
Kadomo anasema kitengo cha Ujirani Mwema kinaandaa ziara za makundi mbalimbali ya jamii kuja kutembelea hifadhi na kuona vivutio mbalimbali ndani ya hifadhi. Makundi haya yamekuwa yakihusisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari zinazo jirani na hifadhi”.
Makundi mengine ni viongozi wa serikali za vijiji na kata zinazopakana na hifadhi. Hifadhi ya Rubondo, kijiografia ipo Mkoa wa Geita. Imezungukwa na visiwa vidogo 11 ambavyo ni sehemu ya hifadhi.
Kuna majabali makubwa mawili; moja upande wa Kaskazini na lingine upande wa Kusini ndani ya misitu minene ya asili ya Kongo. Hifadhi ya Taifa ya visiwa vya Rubondo ipo jirani na visiwa kadhaa vya makazi ambayo ni Mizo, Nyamitundu, Chitende, Katera, Iroba, Chambuzi, Munyila, Makosi, pamoja na Izilambula.
Rubondo ni hifadhi pekee nchini na Afrika inayopatikana katika makazi ya maji ya ziwa. Kijiografia hifadhi hii inapatikana katika Ziwa Victoria Kaskazini mwa ghuba ya Emini pasha mkoani Geita.
Hifadhi ya Rubondo ina ukubwa wa kilometa za mraba 457 ambazo kati yake, 237 ni nchi kavu na 220 ni maji. Hifadhi hii ipo ndani ya Ziwa Victoria ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani, lenye kilometa za mraba 69,485, likitanguliwa na Ziwa Superior la Amerika ya Kaskazini lenye ukubwa wa kilometa za mraba 82,414.
Taarifa juu ya Rubondo zinadhihirisha kuwa Watanzania hawahitaji kusoma au kuhadithiwa juu ya hifadhi hii ya taifa ya Rubondo. Bali panahitajika utamaduni wa kwenda na ujionee kwa macho vivutio mbalimbali vya utalii kama hifadhi hii ya Rubondo.
Hifadhi inafikika kwa njia ya usafiri wa maji ya Ziwa Victoria. Ni takriban kilometa 165 kutoka Sengerema na kutoka Geita hususani katika Kata ya Nzera, kuna umbali wa kilometa sita mpaka saba.
Lakini pia changamoto iliyopo ni kuhakikisha jamii inathamini na kutunza hifadhi kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo. HABARILEO IJUMAA MACHI 3, 2017 Tembelea Rubondo, hifadhi yenye upekee ziwani Victoria Michoro ya mapangoni na umaarufu wa Kondoa Irangi

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!