LEO ni Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu kama Mei Mosi. Kihistoria, ni siku ambayo inatukumbusha yaliyojiri katika karne ya 18 wakati wa Mapinduzi Viwandani (Industrial Revolution). Katika karne hii, teknolojia ilikuwa imeanza kukua na kushika nafasi yake ambapo mitambo na mashine mbalimbali za uzalishaji viwandani ziligunduliwa na kufanya kazi, hatua ambayo pia ilibadilisha mtindo wa uchumi.
Wakati uchumi ukibadilika kutoka uliotegemea kilimo kwenda kwenye viwanda, nguvu ya binadamu ilihitajika kuendesha mitambo na mashine hizo. Huu ndio ukawa mwanzo wa binadamu kuajiriwa na kufanya kazi viwandani kwa kulipwa ujira na hivyo kuibuka kwa tabaka la wafanyakazi na wenye viwanda au waajiri, mfumo ambao ulioitwa ubepari.
Kadiri uzalishaji viwandani ulivyoongezeka na kupatikana kwa ziada kubwa, ndivyo ubepari ulivyoshamiri na kukomaa. Kukomaa kwa ubepari kulizua matatizo mengi kwa tabaka kubwa la wafanyakazi na jamii kwa ujumla. Tatizo lililokuwa kubwa zaidi ni lile la wafanyakazi kufanyishwa kazi kwa saa nyingi zaidi kati ya 14 hadi 18 kwa siku. Matatizo mengine yaliyoibuka kutokana na mapinduzi haya ya viwanda ni pamoja na mishahara kuwa midogo iliyolipwa kwa ubaguzi, mazingira machafu ya kazi, ajali nyingi kazini, kufukuzwa kazi kiholela, kukithiri kwa vitendo vya uonevu, unyanyasaji na udhalilishaji.
KWA NINI MEI MOSI
Mwaka 1884 nchini Marekani, Shirikisho la Wafanyakazi lilipitisha azimio kuwa ifikapo tarehe 1 Mei, mwaka 1886 na kuendelea saa za kufanya kazi zitambulike kisheria kuwa ni nane tu kwa siku. Azimio hili lilisababisha kuibuka kwa maandamano makubwa ya amani yaliyohusisha maelfu ya wafanyakazi ili kushinikiza waajiri na serikali kukubaliana na azimio hilo.
Kufanyika kwa maandamano hayo kulisababisha viongozi wa wafanyakazi kukamatwa, kufungwa, kuteswa na baadhi yao kuuawa. Hatimaye wafanyakazi walipata ushindi kwani mwaka 1886 ilikubalika nchini Marekani kuwa saa za kazi ziwe nane tu kwa siku. Mkutano mkuu wa pili wa kimataifa wa Jumuiya ya Wafanyakazi ulifanyika Paris Ufaransa mwaka 1890.
Mkutano huo ulipitisha azimio kuwa tarehe Moja Mei ya kila mwaka iadhimishwe duniani kote, ikiwa ni namna ya kuwakumbuka wale walioteswa na kupoteza maisha yao wakipigania haki za wafanyakazi wenzao ambazo nasi tunazifurahia hadi hivi leo.
Mei Mosi, huadhimishwa duniani kote kwa namna mbali mbali. Hapa nchini Tanzania wafanyakazi wamekuwa na jadi ya kuadhimisha siku hiyo, kwa kutathmini mafanikio ya kazi zao, kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao na kupima hali ya uhusiano na ushirikiano baina yao, waajiri na Serikali (ambayo pia ni mwajiri).
SHIRIKA LA KAZI DUNIANI
Shirika la Kazi Duniani (ILO) ni mojawapo ya vyombo au taasisi maalumu za Umoja wa Mataifa (UN) vinavyohusiana na masuala ya wafanyakazi. Shirika hili lilianzishwa mwaka 1919 kwa lengo la kuinua na kuendeleza haki za binadamu na haki za kazi zinazotambulika kimataifa ili kudumisha amani katika ulimwengu wa kazi. Shirika la Kazi Duniani ni chombo cha Utatu kwa maana kuwa, Utendaji wake uhusisha wafanyakazi, waajiri na serikali.
Chombo hiki huweka sera na programu za kimataifa za kusaidia kuboresha mazingira ya kazi na maisha ya watu kazini na huweka viwango vya kazi kimataifa vinavyotumika kama mwongozo kwa nchi mwanachama katika kuandaa sheria, kanuni au sera mbali mbali za kazi. Pia huendesha programu za ushirkiano wa kiufundi ili kusaidia serikali husika katika kutekeleza mikataba au sera za kazi zilizowekwa na shirika hilo.
Shirika la Kazi Duniani hufanya mkutano wake kila mwaka ambao hushirikisha wadau kutoka nchi zote wanachama. Wafanyakazi wanayo haki ya kujua kupitia wawakilishi wao hoja zote na mapendekezo yanayotokana na mkutano huo. Makao makuu ya shirika hili yako Geneva, Uswisi. Tanzania ni mwanachama wa Shirika la Kazi Duniani na tayari imekwisha ridhia baadhi ya mikataba ya shirika hilo ikiwemo ile minane ya msingi.
VYAMA VYA WAFANYAKAZI TANZANIA
Muungano au shirikisho la vyama vya wafanyakazi umesajiliwa kwa mujibu wa Sheria namba 6 na 7 za mwaka 2004 zinazosimamia vyama vya wafanyakazi. Awali vyama vya wafanyakazi vilikuwa chini ya chama tawala enzi nchi ikiongozwa na chama kimoja ambapo chama hicho kilichowaunganisha wafanyakazi kiliitwa kwa kifupi NUTA, yaani Chama cha Wafanyakazi Tanzania. Baadaye wafanyakazi waliwakilishwa na Jumuiya ya Wafanyakazi Tanzania (JUWATA).
Vyama hivi vwili vilifanya kazi kati ya mwaka 1964 hadi 1991. Baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa siasa vya vyama vingi mwaka 1992, vyama vya wafanyakazi vililazimika kubadilisha mfumo wa kujiendesha kwa kutenganisha shughuli zake na zile za chama pamoja na kujiendesha kwa uhuru ambapo wafanyakazi waliruhusiwa kujiunga na vyama vyao kulingana na sehemu au sekta wanazotoka.
Vyama vya wafanyakazi viliundwa chini ya Sheria ya Chama cha Wafanyakazi Tanzania (OTTU) namba 20 ya mwaka 1991 na kuthibitishwa rasmi Novemba 1994 baada ya mkutano mkuu kupitisha katiba na kuchagua viongozi wa kitaifa. Kwa sasa wafanyakazi wanaongozwa na shirikisho (Tucta) linaloundwa na vyama mbalimbali vya wafanyakazi. Tabia ya matajiri (waajiri) kuwanyonya na kuwakandamiza waajiriwa wao haikuwa Ulaya tu bali ilienea duniani kote.
Hapa Tanzania historia inatuambia kuwa wafanyakazi walioajiriwa viwandani na kwenye mashamba makubwa ya Wakoloni walifanyishwa kazi ngumu za shurti kwa saa nyingi na kwa ujira mdogo. Aidha watanzania hao walidharauliwa, walibaguliwa na kudhalilishwa. Wafanyakazi hawakuridhishwa na hali hiyo na ndipo walipoanza harakati za kujikomboa mwaka 1927 ambapo walijiundia vyama vyao vya kutetea, kulinda na kuendeleza haki zao.
Leo tunapoadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), tunapaswa kujiuliza swali la msingi kuwa; Je, mazingira yaliyosababisha kuundwa kwa vyama vya wafanyakazi katika karne ya 18 bado tunayo au yameondoka? Je, majukumu ya Vyama vya Wafanyakazi yamebadilika au ni yale yale?
Ukweli ni kwamba mazingira yaliyosababisha kuundwa kwa vyama vya wafanyakazi katika karne ya 18 bado yapo hadi leo hii, ingawaje kwa mfumo usio wazi na pengine kutokana na kuwepo kwa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambalo limefanya kazi kubwa ya kuleta maridhiano sehemu za kazi na kujaribu kuimarisha uhusiano mzuri baina ya Serikali, waajiri na vyama vya wafanyakazi.
Aidha, maazimio na matamko ya kimataifa kuhusu haki za binadamu yamesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa baadhi ya vitendo vya uonevu sehemu za kazi. Nikirejea swali la msingi hapo juu, mazingira ya kazi tuliyo nayo leo hii sio mazuri sana na hayatofautiani sana na yaliyojitokeza wakati wa karne ya 18 kulipotokea mapinduzi ya viwanda huko Ulaya na Marekani.
Ikumbukwe kuwa ubepari ndio mfumo uliyoshamiri hivi sasa duniani. Mojawapo ya sifa za ubepari ni kuwepo kwa watu wachache wenye nguvu za kiuchumi ambao huendesha na kufanikisha shughuli zao kwa kunyonya wengine kwa njia ya kuwatumikisha kwa ujira mdogo kadri iwezekanavyo. Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika, tumeachia shughuli za uendeshaji wa biashara kuwa mikononi mwa sekta binafsi inayoshikiliwa na wawekezaji kutoka nje na ndani ya nchi.
Wawekezaji wanachojali ni faida na kushamiri kwa biashara zao. Wengi wao hawana huruma na hali za Wafanyakazi. Ndio maana leo hii kuna malalamiko mengi ya Wafanyakazi kulipwa mishahara midogo sana, kufanyishwa kazi kwa masaa mengi, kufukuzwa kazi kiholela, kudhalilishwa na kufanyishwa kazi katika mazingira hatarishi yasiyozingatia Afya na Usalama wa Wafanyakazi.
Baadhi ya kazi zinazofanywa na wafanyakazi hazina Staha (nondecent work) kwa maana kuwa zinadhalilisha, zina ujira mdogo na ni za muda mfupi na baada ya hapo mfanyakazi anakuwa hana kazi tena. Kwa vyovyote vile mazingira haya yanahitaji vyama vya wafanyakazi vyenye nguvu.
No comments:
Post a Comment