Tuesday 4 April 2017

Fisi alivyoua watoto watatu


WATOTO watatu wamefariki dunia kwa kuraruliwa na fisi huku wengine wawili wakijeruhiwa, baada ya mnyama huyo kuvamia makazi ya watu katika kijiji cha Ntungwa wilayani Momba, mkoa wa Songwe.



Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Songwe, Ambwene Mwanyasi, alisema tukio hilo lilitokea katikati ya wiki iliyopita.
Akisimulia, Mwanyasi alisema fisi alivamia watoto hao walipokuwa wakicheza kando ya dimbwi lililopo Mto Upofu.

Alifafanua kuwa wakati watoto hao wakipatwa na mkasa huo, wazazi wao walikuwa shambani kando kando ya mto huo wakivuna mtama.

Kamanda Mwanyasi aliwataja watoto waliopoteza maisha kuwa ni Yunge Kija (4), Subira Schela (11) na Doto Labson (miezi 6).
Aidha, aliwataja majeruhi kuwa ni Hanifa Labson (5) na Frank Schila (4), wakazi wa kijiji hicho ambao alisema walijeruhiwa wakati fisi huyo akiwa katika harakati za kutoroka.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi iliyopo mamlaka ya Mji wa Vwawa, Malema Mwasile, alithibitisha kupokea majeruhi wawili.
Mwasile alisema hali za majeruhi wote zinaendelea vizuri na miili ya watoto hao imehifadhiwa hospitalini hapo.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Subira Kaminyoge ameilalamikia Idara ya Maliasili na kushauri iwe inatoa ushirikiano pindi majanga kama hayo yanapotokea.
Alisema tangu kutokea kwa tukio hilo, maofisa wa idara hiyo walikuwa hawajawasili kutoa msaada wowote au rambirambi.
Alisema maofisa wa idara hiyo wamekuwa wakikaa maofisini licha ya kuwa kumekuwapo na majanga ya watu kuuawa na fisi kwenye eneo hilo.
Aliwashauri maofisa wa idara hiyo kuhakikisha wanafanya doria za mara kwa mara ili kupunguza vifo visivyo vya lazima.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!