Tuesday, 7 March 2017

TADB, BODI YA NYAMA KUWAWEZESHA WADAU WA UFUGAJI WA NG’OMBE


Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) zimejidhatiti kusaidia mnyororo wa thamani wa ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa ili kuongeza tija kwenye sekta ya ufugaji wa ng’ombe nchini.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga na Afisa Masoko na Utafiti, Bw. Nicholai Chiweka kutoka TMB wakati wa majadiliano kuhusu Mkutano Mkuu wa Wadau wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 8 hadi 9 Machi, 2017.
Bw. Assenga amesema kuwa TADB imejidhatiti katika kuongeza tija kwa Ufugaji wa Ng’ombe wa Nyama na Maziwa kwa kutoa mikopo na kusaidia shughuli mbali mbali za uongezaji tija wa ufugaji huo.
“Katika kuhakikisha sekta hii inaendelea na kuongeza tija, TADB imejipanga kutoa mikopo itakayotumika kama mtaji kwa ajili ya uendeshaji wa mashamba, uongezaji wa thamani na gharama za uhifadhi wa nyama/maziwa na miundombinu masoko kwenye sekta hii,” alisema Bw. Assenga.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB ameongeza kuwa kwa kushirikisha wadau wa Kilimo, utafiti, huduma za ugani na madaktari wa mifugo TADB imelenga kuwapatia wafugaji mafunzo ya ufugaji wa kisasa wa ng’ombe wa nyama na maziwa kwa kutumia mbinu bora za ufugaji ili kufuga kibiashara na hivyo kujiongezea kipato na kupambana na umaskini.
Kwa upande wake Bw. Chiweka amesema kuwa TMB ina Mamlaka yenye dhamana ya kusimamia maendeleo ya tasnia ya nyama, iliyoanzishwa kwa Sheria ya Nyama Na. 10 ya Mwaka 2006 hivyo ina wajibu wa kuratibu mnyororo mzima wa thamani wa tasnia ya nyama na kuiomba TADB kushirikiana na TMB kunyanyua sekta ya nyama.
“Kifungu Na. 17 (1) cha sheria hii, kinazuia mtu yeyote kufanya shughuli ya aina yoyote katika tasnia ya nyama bila ya kuwa na cheti cha usajili kutoka Bodi ya Nyama Tanzania hivyo kama mdau wa kuendeleza sekta hii tunaiomba TADB kuwasaidia wadau wa mnyororo mzima wa thamani watasnia ya nyama ambao wamesajiliwa na TMB,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Chiweka wadau wa tasnia ya nyama inajumuisha  Wafugaji wa mifugo ya aina zote inayozalisha nyama;  Wafanyabiashara wa Mifugo; Wasafirishaji wa mifugo na nyama; na  Wenye machinjio za aina zote. Wengine ni Wenye bucha za kuuza nyama za aina zote; Wasindikaji wa nyama; maduka makubwa na duka la bucha, Wasambazaji wa bidhaa za nyama; Waingizaji wa nyama nchini; Wasafirishaji wa mifugo, nyama na bidhaa zake nje ya nchi; na Waendesha matamasha ya nyama choma.
Mnyororo wa thamani wa Ufugaji wa ng’ombe wa nyama na maziwa ni miongoni mwa minyororo ya mwanzo inayopatiwa mikopo na TADB ili kuongeza thamani mazao na mifugo mbalimbali nchini.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Francis Assenga (Kulia) akiwakaribisha maafisa kutoka Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) walipomtembelea Ofisini kwake kujadiliana juu ya Mkutano Mkuu wa Wadau wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 8 hadi 9 Machi, 2017. Kushoto ni Afisa Masoko na Utafiti, Bw. Nicholai Chiweka na Afisa Sheria, Bw. Praisegod Lukio (katikati).


Afisa Masoko na Utafiti wa TMB, Bw. Nicholai Chiweka (aliyeinama) akisaini Kitabu cha Wageni wakati alipomtembelea TADB. Wanaoshuhudia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kushoto), Afisa Sheria wa TMB, Bw. Praisegod Lukio (wa pili kushoto). Kulia ni Mkuu wa Huduma na Sheria wa TADB, Bibi Neema Christina John.


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (kushoto) akizungumza na maafisa kutoka Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) Afisa Sheria, Bw. Praisegod Lukio (wa pili kushoto) na Afisa Masoko na Utafiti wa TMB, Bw. Nicholai Chiweka (wa pili kulia) wakati walipomtembelea Ofisini kwake kujadiliana juu ya Mkutano Mkuu wa Wadau wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 8 hadi 9 Machi, 2017. Kulia ni Mkuu wa Huduma na Sheria wa TADB, Bibi Neema Christina John.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga akisisitiza jambo kuhusiana na umuhimu wa sekta ya nyama wakati akizungumza na maafisa kutoka Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) (hawapo pichani) kuhusu Mkutano Mkuu wa Wadau wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 8 hadi 9 Machi, 2017.

Afisa Masoko na Utafiti wa TMB, Bw. Nicholai Chiweka (kulia) akizungumza wakati walipomtembelea Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB (hayupo pichani) kujadiliana juu ya Mkutano Mkuu wa Wadau wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 8 hadi 9 Machi, 2017.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (wa pili kushoto) na Afisa Masoko na Utafiti wa TMB, Bw. Nicholai Chiweka (wa pili kulia) wakionesha fulana kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa Wadau wa Bodi ya Nyama utakaofanyika mkoani Dodoma kuanzia tarehe 8 hadi 9 Machi, 2017. Wengine pichani ni Mkuu wa Huduma na Sheria wa TADB, Bibi Neema Christina John (kushoto) na Afisa Sheria wa TMB, Bw. Praisegod Lukio (kulia).

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw. Francis Assenga (wa pili kushoto) na Afisa Masoko na Utafiti wa TMB, Bw. Nicholai Chiweka (wa pili kulia) wakionesha kauli mbiu ya ya Mkutano Mkuu wa Wadau wa Bodi ya Nyama “Maendeleo ya Endelevu ya Viwanda: Fursa kwa Uwekezaji katika Mnyororo wa Thamani wa Nyama.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!