Friday, 3 March 2017

Faini zashindwa kumaliza ajali barabarani

VIWANGO vikubwa vya faini zinazotozwa kwa makosa mbalimbali ya vyombo vya usafirishaji, imedaiwa kuwa havisaidii kumaliza tatizo la ajali za barabarani, badala yake serikali itafute njia ya kumaliza tatizo hilo.


Maoni hayo yalitolewa na wadau wa sekta ya usafiri jijini Dar es Salaam jana katika mkutano ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Ulikuwa wa maboresho ya kanuni za usafirishaji kwa magari ya abiria, ya mizigo na pikipiki za miguu mitatu na miwili. Mjumbe kutoka Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Ibrahim Awadhi alisema mambo mengi yaliyopo katika maboresho ya kanuni hizo sio mapya, isipokuwa ongezeko la viwango vya faini.
“Mambo yote hayo yapo muda mrefu, hakuna jipya hapo zaidi ya faini, ni kama vile kinachopiganiwa hapo ni faini hiyo, faini hizo haziondoi ajali tutafute njia nyingine ya kutatua tatizo hilo,” alisema Awadhi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala wa Dar es Salaam (DACOBOA), Sabri Mabrouk alisema ukubwa wa viwango vya faini kwa wamiliki wa magari ni tatizo, ambalo linawakatisha tamaa wafanyabiashara.
“Kwa mfano faini ya mtu akikutwa hana mzani wa kupimia mizigo ya abiria unafungwa mwaka, ufungwe kwa sababu hiyo?” alihoji Mabrouk.
Awali, Mabrouk alilalamikia Sumatra kutoa taarifa ya kikao hicho cha wadau muda mfupi kabla ya kikao, jambo ambalo halitoi ruksa kwa wadau kutoa maoni yao.
Katika baadhi ya kanuni hizo mpya, mmiliki wa gari anatakiwa kufunga kidhibiti mwendo kwenye kila gari, kuwa na mzani wa kupimia mzigo wa abiria na kwamba abiria aruhusiwe kusafiri na kilo 20 bure bila kulipia.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo, mmiliki atakayekutwa hana mzani atatakiwa kulipa faini, kifungo au vyote viwili ambapo viwango vya faini vimeainishwa kuwa ni kuanzia Sh 200,000 hadi Sh 500,000. Baadhi ya wadau waliomba kuwa abiria aruhusiwe kusafirisha bure mzigo mdogo, unaokaa ndani ya basi pekee na alipie mzigo wowote, ambao utakuwa ni mkubwa na kulazimika kuwekwa kwenye buti la basi.
Aidha kwenye kanuni hiyo, imeainishwa dereva anayeruhusiwa kuendesha gari la shule, awe na umri wa kuanzia miaka 30 hadi 60, jambo ambalo wadau hao waliomba ishushwe iwe kuanzia miaka 25 kutoa fursa ya ajira kwa vijana wengi zaidi.
Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Giliard Ngewe akifungua mkutano huo alisema sababu za marekebisho ya kanuni hizo pamoja na mambo mengine ni ongezeko la ajali kutokana na kukiukwa kwa sheria, kanuni na masharti ya leseni za usafirishaji na madereva wasiotaka kutii maadili yao.
“Suala la ajali ni mtambuka, sio la Sumatra pekee, kila mdau ana sehemu ya kufanya kupunguza ajali hizo na sisi tuna wajibu wa kuboresha mazingira ya huduma na pia kanuni,” alisema.
Aliongeza kuwa sababu nyingine ni kwamba kanuni zinapitwa na wakati, hivyo zinahitaji maboresho kadiri muda unavyokwenda ili kuboresha huduma za usafiri nchini.
“Hivyo vitu kwa kifupi ndivyo vilivyotufavya kuja na mapendekezo ya rasimu ya kanuni kurekebisha kanuni zilizokuwepo, leo tunakutana ni kutokana na maelekezo ya sheria,” alisema Ngwewe na kuongeza kuwa rasimu hizo nne ambazo zilijadiliwa jana, Sumatra itaendelea kupokea maoni kwa njia ya maandishi hadi Machi 16 mwaka huu.
Alisema katika kuboresha huduma vyombo vya usafirishaji, lazima viwe na viwango kila mtumiaji wa barabara

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!