ZIKIWA zimebaki siku chache kabla ya kumalizika kwa mwaka 2016, moja ya matatizo makubwa yaliyoikumba Tanzania kwa mwaka huu ni maafa ya mafuriko pamoja na tetemeko kubwa la ardhi lililotokea mkoani Kagera.
Katika miaka ya karibuni, Tanzania imekuwa ikishuhudia maeneo mbalimbali ya nchi yakipata mvua kubwa kuliko inavyotarajiwa, na mvua hizo husababisha mafuriko ambayo si tu wakati mwingine hupoteza uhai wa watu, lakini mara nyingi huacha miundombinu ikiwa imeharibika vibaya pamoja na makazi ya watu.
Kwa mfano, wakazi wa Wilaya ya Iringa mkoani Iringa, Februari mwaka huu walikumbwa na mafuriko makubwa ambayo yaliacha nyumba 86 kuharibika kutokana na mvua hiyo na kusababisha hadi leo hii wananchi wake wasiwe na makazi yao ya kudumu.
Waathirika wa mafuriko hayo ya Iringa walikuwa ni wananchi kwenye vijiji vya kata ya Mlenge, tarafa ya Pawaga, Wilaya ya Iringa Vijijini Mkoa wa Iringa. Mafuriko hayo yalibomoa nyumba 82 katika kitongoji cha Kilala, Kijiji cha Kisanga na kuwaacha wananchi wake bila makazi.
Kwa mujibu wa taarifa aliyoiotoa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea waathirika hao Februari 22, mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema jumla ya kaya 82 zilikosa makazi kutokana na mvua zilizonyesha Februari 12 na kusababisha mafuriko.
Kabla ya hapo, kaya nyingine 75 zenye wakazi 377ziliathirika kutokana na mvua zilizoanza Februari 3, mwaka huu.
Alisema miundombinu ya barabara na ya maji safi iliharibiwa vibaya na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 250. Pia wakazi hao walikumbwa na ugonjwa wa kipindupindu kutokana na mto Mapogoro kufurika na kusomba baadhi ya vyoo vya wakazi hao.
Lakini pia mwaka huu, mafuriko hayakuliacha kando Jiji la Dar es Salaam kwani Aprili mwaka huu, jiji hilo kitovu cha biashara cha Tanzania lilikumbwa na mafuriko ambayo kama kawaida yaliathiri watu wanaoishi sehemu za mabondeni pamoja na kuathiri shughuli za kiuchumi kwa siku kadhaa.
Kana kwamba hiyo haitoshi, jiji jingine kubwa nchini, Mwanza lilikumbwa na mafuriko mwanzoni mwa mwaka huu ambayo yalisababisha vifo vya watu wawili akiwamo mwanafunzi aliyesombwa na maji akitoka shuleni kwenye mto Mirongo. Lakini maafa ambayo hayatasahaulika kwa Watanzania wengi mwaka huu ni tetemeko la ardhi lililoukumba Mkoa wa Kagera na mikoa mingine jirani ya Kanda ya Ziwa alasiri ya Septemba 10, mwaka huu.
Tetemeko la ukubwa wa mtikisiko wa kipimo cha Ritcher 5.7 lilitokea katika mikoa mitatu nchini ya Kagera, Mwanza na Mara na kusababisha vifo vya watu 17 na wengine 120 wamejeruhiwa huku majengo mengi yakibomoka. Pia tetemeko hilo liliukumba mji wa Kampala na Rakai nchini Uganda siku hiyo saa 9.27 alasiri.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Profesa Abdulkarim Mruma, tetemeko hilo lilikuwa kubwa kwa nusu ya kipimo cha juu cha Ritcher 10 na limezidi kipimo cha chini cha ukubwa wa Ritcher tatu. Alisema limezidi lililotokea Dodoma hivi karibuni.
Profesa Mruma alieleza wakati huo wa tetemeko hilo kwamba limetokea katika mpaka wa Tanzania na Uganda, kilometa 47 kaskazini mwa Bukoba mkoani Kagera na sababu ni mpasuko wa ardhi katika Bonde la Ufa la Magharibi karibu kabisa na Ziwa Victoria.
Alipokuwa akiahirisha mkutano wa Tano wa Bunge, Novemba 11, mwaka huu mjini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa alisema jumla ya watu 117,721 wameathirika kwa kupoteza makazi yao, mali na athari za kisaikolojia katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba, Karagwe na Kyerwa. Aidha, jumla ya watu 17 walipoteza maisha na 560 walijeruhiwa.
Vilevile, nyumba 2,072 za makazi zilianguka kabisa na nyumba 14,595 za makazi zilibomoka, baadhi zina kuta au kupata nyufa kubwa na hivyo kuzifanya kuwa hatarishi kwa makazi ya binadamu.
Vilevile, maafa haya yalisababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na majengo ya serikali 1,718 yaliyoharibika kwa viwango tofauti. Serikali ilianzisha Kituo cha Operesheni na Kuratibu Maafa kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwa lengo la kuharakisha huduma. Aidha, serikali ilitoa matibabu bure kwa majeruhi wote, kuandaa na kugharamia maziko ya watu 17.
Vilevile, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iliwahudumia wananchi walioathirika na tetemeko kwa kuwapatia misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula, madawa, nguo, makazi ya muda, vifaa vya ujenzi, vifaa tiba, vifaa vya shule na huduma ya ushauri wa kisaikolojia.
Kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa na wadau mbalimbali, serikali ilifanya tathmini ya pamoja ya mahitaji ya haraka katika kukabiliana na athari za tetemeko hilo, ambako utekelezaji wa masuala muhimu yaliyoainishwa katika tathmini hiyo unaendelea.
Waziri Mkuu alieleza wakati huo kwamba taarifa ya kikosi kazi cha wataalamu imeainisha kuwa takribani Sh bilioni 63.2 zitahitajika kurejesha hali ya kawaida katika Mkoa wa Kagera kutokana na maafa hayo.
Gharama hiyo inajumuisha ukarabati wa shule za msingi, sekondari, vituo vya afya na taasisi nyingine katika wilaya zote sita za mkoa huo, ujenzi mpya wa shule za Ihungo na Nyakato (tayari wafadhili wamejitolea kujenga shule hizi).
“Aidha, hadi kufikia tarehe 10 Novemba, 2016 kiasi cha Sh 966,898,826 zilitumika katika kufanya ukarabati mkubwa na mdogo wa shule za msingi na sekondari pamoja na zahanati katika Halmashauri za Mkoa wa Kagera. Serikali inaendelea na ujenzi wa zahanati mpya (Ishozi) inayojumuisha chumba cha upasuaji na wodi ya kinamama na watoto na usimamizi wa ujenzi wa shule za Ihungo na Nyakato.
“Aidha, katika kuongeza nguvu ya urejeshaji hali jumla ya askari 96 wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wakiwemo wahandisi, mafundi, wapishi, na madereva waliwasili mkoani Kagera tarehe 19 Oktoba, 2016 kushiriki katika zoezi la kurejesha hali ya majengo na miundombinu,” alieleza Waziri Mkuu.
Alilihakikishia Bunge na wananchi kwa jumla kuwa serikali ipo pamoja na waathirika hawa katika suala hilo na ina mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunarejesha hali bora kwa kuendelea kurudisha miundombinu, kutoa huduma za kibinadamu na matibabu kwa waathirika.
Kwa hakika, tetemeko hilo limeacha athari kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera, na ni ukweli usiofichika kwamba bado juhudi zinahitajika kuendelea kufanyika ili kuhakikisha wananchi walioathirika wanapatiwa huduma muhimu hasa za makazi wakati huu wakiendelea kujipanga upya kurejea katika hali zao.
Wananchi wa Kagera wanapaswa kuendelea kusaidiwa kutokana na athari za mafuriko kwani wapo wengi ambao hawajapata misaada na pia makazi yao yameendelea kuathirika kwa sababu ya kutokuwa na uwezo wa kukarabati au kujenga nyumba zao zilizoanguka na kuharibika vibaya.
Aidha, ni muhimu kwa mamlaka husika zikiwamo zinazoshughulika na majenzi, kuendelea kutoa elimu ya ujenzi wa nyumba hasa katika maeneo ambayo yako hatarini kupata majanga ya asili kama matetemeko ya ardhi kwani mara nyingi yanapotokea huacha athari kubwa sana kwa jamii.
No comments:
Post a Comment