MAREKANI: Wamarekani zaidi ya milioni 200 leo Novemba 8, 2016 wanapiga kura kuamua atakayekuwa rais wao wa 45.
Hapa ni mambo muhimu ya kufuatilia wakati wa uchaguzi.
Majimbo yote 50 pamoja na Washington DC (eneo ambalo halijatambuliwa kama jimbo) watapiga kura katika nyakati sita tofauti za uchaguzi.
Tofauti hii inatokana na ukubwa wa taifa hilo, ambapo majimbo yaliyo mashariki yatatangulia kupiga kura na yale yaliyo magharibi yatakuwa ya mwisho.
Lakini tofauti na demokrasia ya nchi nyingine nyingi duniani, nchini Marekani anayeshinda kura nyingi kitaifa si lazima awe ndiye atakayeibuka mshindi.
Marekani huwa na mfumo tofauti wa uchaguzi ambapo mshindi anahitajika kushinda kura 270 za wajumbe kati ya 538 zinazoshindaniwa.
Maeneo mengi Marekani yatasubiri vituo vifungwe- sana kati ya 19:00 EST (24:00 GMT – Saa 09:00 usiku Afrika Mashariki) na 20:00 EST (01:00 GMT – Saa 10:00 usiku Afrika Mashariki) – kuanza kupokea matokeo na makadirio ya matokeo katika majimbo mbalimbali.
Hata hivyo, kijiji kimoja kwa jina Dixville Notch katika jimbo la New Hampshire, kina desturi ya kupiga kura usiku wa manane. Kijiji hicho kitakuwa kimetangaza matokeo yake hata kabla ya upigaji kura kumalizika katika maeneo mengine. Hilo litakuwa mwendo wa saa 00:01 EST (05:01 GMT – Saa mbili asubuhi).
Hapa ni baadhi ya mambo ambayo huenda yakatokea, kwa kutegemea wakati ambao vituo vya kura vitafungwa. Hata hivyo, kuna uwezekano wa kuwepo tofauti kidogo katika wakati wa kufungwa kwa matokeo.
BBC itakuwa inategemea makadirio ya mshirika wake Marekani, ABC, kwa sababu inaweza ikachukua siku kadha kabla ya kura zote kuhesabiwa.
Na kuhusu matokeo kamili? Kaa chonjo na simu yako au uwe macho kwenye runinga mwendo wa saa 23:00 EST (04:00 GMT – Saa moja asubuhi Afrika Mashariki). Ukiona huenda ukapitwa kwa sababu ya usingizi, unaweza kuweka kengele ya saa ya kukuamsha. Huo ndio wakati upigaji kura utamalizika pwani ya Magharibi mwa Marekani. Historia inaonesha huo ndio wakati mshindi hutangazwa. Ilikuwa kabisa wakati huo ambapo mshindi alijulikana mwaka 2008, na dakika 15 baadaye mwaka 2012.
19:00 EST (00:00 GMT – Saa tisa usiku Afrika Mashariki)
Vituo vya kura Pwani ya Mashariki vyafungwa na kuhesabiwa kwa kura kuanza.
Macho ya wengi yatakuwa jimbo la kushindaniwa la Virginia (kura 13 za wajumbe), ambalo lilimpigia kura Barack Obama mwaka 2008 na 2012 lakini awali lilikuwa la Republican.
Donald Trump akishinda huko, au amkaribie sana Hillary Clinton, itakuwa ishara kwamba huenda ukawa usiku mrefu kwa wafuasi wa Democratic, kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Amerika Kaskazini Anthony Zurcher.
Jimbo la Georgia (16) pia ni muhimu. Jimbo hilo limeunga mkono chama cha Republican tangu 1996, lakini ubabe wa chama hicho umekuwa ukipungua miaka ya karibuni.
Pia, kunatarajiwa makadirio ya matokeo kutoka jimbo la Indiana (11), nyumbani kwa mgombea mwenza wa Trump Mike Pence, Kentucky (8), South Carolina (9) na Vermont (3).
19:30 EST (00:30 GMT – Saa tisa unusu Afrika Mashariki)
Vituo vya kupigia kura vyafungwa katika majimbo mengine mawili muhimu, Carolina Kaskazini (15) na Ohio (18).
Carolina Kaskazini ni taifa ambalo halijakuwa na sifa kama za majimbo mengine Marekani.
“Limeshuhudia kufika kwa wageni wengi. Wengi wafuasi wa Democratic. Wapiga kura maskini ambao ni Wazungu wanafanya maeneo mengi ya mashambani yaegemee sana upande wa Donald Trump,” mwandishi wa BBC Katty Kay anasema.
Jimbo hilo huenda likawa ishara ya mapema ya mwelekeo wa uchaguzi.
Ohio ni jimbo ambalo matokeo yake yanasubiriwa zaidi. Jimbo hilo limeunga mkono mgombea aliyeshinda urais kila uchaguzi wa urais isipokuwa wakati mmoja pekee tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Huenda pia kukatangazwa makadirio ya matokeo Virginia Magharibi (5), jimbo ambalo limeunga mkono Republican tangu 2000.
Kipindi cha pilkapilka.
Maine (4), Maryland (10), Massachusetts (11), New Jersey (14), Rhode Island (4), Delaware (3), Connecticut (7) na District of Columbia (3) are ni miongoni mwa majimbo ya Pwani ya Mashariki ambayo makadirio ya matokeo yake yanatarajiwa kipindi hiki.
Jimbo muhimu linaloshindaniwa la Florida (29), ni muhimu kwa mgombea yeyote. Jimbo hilo lilimpigia Obama mwaka 2008 na 2012 (Democratic), lakini George W Bush (Republican) alishinda uchaguzi uliotangulia 2000 na 2004. Jambo la kushangaza ni kuwa alikuwa mbele na kura 537 pekee mwaka 2000. Hata hivyo, ilichukua siku 36 kwake kuthibitishwa kuwa mshindi, kwa hivyo iwapo wagombea watakaribiana sana usitarajie matokeo yatangazwe haraka.
Iwapo Trump atashindwa Florida na Ohio, matumaini yake ya kushinda urais yatakuwa finyu.
Huenda kukapokelewa pia matokeo kutoka Pennsylvania (20), jimbo ambalo lilibadilika na limekuwa likiunga mkono wagombea wa Democratic katika chaguzi sita zilizotanguliwa. Litakuwa pigo kuu iwapo Clinton hatashinda huko.
New Hampshire (4) ni jimbo ambalo pia litafuatiliwa kwa karibu kwani kura za maoni zinaonesha Trump na Clinton wanatoshana nguvu.
Ngome kadha za Republican – Mississippi (6), Missouri (10), Alabama (9), Tennessee (11) na Oklahoma (7) – zinafaa pia kutangaza matokeo wakati huu. Aidha, jimbo la Obama la Illinois(20), ambalo linatarajiwa kumuunga mkono Clinton matokeo yake yanatarajiwa wakati huu.
Kufikia hapa, huenda tukawa na wazo kuhusu nani ataibuka mbabe, hata kabla ya majimbo hayo mengine kutangaza makadirio ya matokeo.Wapiga kura wakipiga kura kituoni.
20:30 EST (01:30 GMT – Saa kumi unusu usiku Afrika Mashariki)
Upigaji kura utamalizika Arkansas (6), jimbo ambalo lilimuunga mkono Bill Clinton uchaguzi mkuu mara mbili miaka ya 1990, lakini limepigia kura Republican tangu 2000.
Hayo yakijiri, masoko bara Asia yanatarajiwa kufunguliwa wakati huu, na kutoa ishara ya jinsi sarafu mbalimbali zitaathiriwa na matokeo ya uchaguzi, kwa kutegemea nani atashinda, Clinton au Trump.
21:00 EST (02:00 GMT – Saa kumi na moja alfajiri Afrika Mashariki)
Fuatilia makadirio ya matokeo ya uchaguzi upande wa Clinton New York (29), ambapo ana wafuasi wengi.
Katika jimbo lililogawanyika sana la Colorado (9), watu wa asili ya Kilatino wanaongezeka lakini kuna idadi kubwa ya wahafidhina. Litakuwa jimbo muhimu kufuatilia. Katika historia, ndilo jimbo lililobadilisha msimamo zaidi. Lilimuunga mkono George W Bush wa Republican mwaka 2004 kwa kiwango kikubwa kuliko wastani kitaifa, lakini miaka minne baadaye likabadilika na kuunga mkono pakubwa Barack Obama wa Democratic.
Mgombea mwenza wa Clinton, Tim Kaine akiwa na mama yake mzazi Mary baada ya kupiga kura katika Jimbo la Virginia.
Jimbo la Michigan (16) katikati mwa Marekani, linaweza pia kuwashangaza watu. Jimbo hilo limeunga mkono mgombea wa Republican tangu 1988, lakini athari za utandawazi zimewafanya wengi wa Wazungu jimbo hilo, pamoja na wale ambao hawajapata elimu sana, kumuunga mkono Trump.
Mgombea mwenza wa Bi Clinton, Tim Kaine, amefika katika kituo cha kupigia kura Virginia kupiga kura yake kwa mujibu wa mwandishi huyu wa Fox News.
Vituo vya kura pia vitafungwa Texas (38), Kansas (6), Louisiana (8), North Dakota (3), South Dakota (3), Minnesota (10), Wyoming (3) naNebraska (5).Ni muhimu kutambua kwamba Nebraska na Maine ndiyo majimbo pekee ambayo huwa hayampatii mshindi kura zote za wajumbe.
Usisahau pia Wisconsin (10), jimbo ambalo halijawahi kuunga mkono Republican tangu 1984. Trump amekuwa akifanya juhudi dakika za mwisho kuwashawishi wampigie kura.
New Mexico (5) walizoea kubadilika badilika lakini Democratic wameshinda chaguzi tano kati ya sita za karibuni zaidi. Msimamo wa Trump dhidi ya wahamiaji na tishio kwamba atajenga ukuta mpaka wa Marekani na Mexico huenda ukafanya jimbo hilo kumuunga mkono Clinton.
22:00 EST (03:00 GMT – Saa kumi na mbili alfajiri Afrika Mashariki)
Jimbo la Nevada (6) kawaida hupigia kura chama cha Republican, lakini mambo yanaweza kubadilika. Taarifa zinaonyesha huenda watu wa asili ya Hispania walijitokeza kwa wingi kupiga kura mapema jambo linaloweza kumfaa Clinton. Hali ni sawa Arizona (11), ambalo limeunga mkono Republican kila uchaguzi tangu 1952 ila walipompigia Bill Clinton mwaka 1996.
Utah (6) ni jimbo jingine la kusisimua. Ajenti wa zamani wa CIA ambaye ni wa dini ya Mormon Evan McMullin, anawania urais kama mgombea huru na anafanya vyema sana kwenye kura za maoni. Jimbo hilo huenda likawa jimbo pekee ambapo Clinton na Trump watashindwa, licha ya kwamba jimbo hilo liliunga mkono Republican awali.
Iowa (6) ni jimbo ambalo Trump anafaa kushinda, ikizingatiwa uungwaji mkono wake miongoni mwa Wazungu, na watu wasiosoma sana hadi vyuo, lakini jimbo hilo lilipigia kura Obama mwaka 2008 na 2012 kwa hivyo si lazima ashinde.
Montana (3) limekuwa jimbo la Republican tangu 1968, ila tu mwaka 1992 mgombea wa Democratic Bill Clinton aliposhinda.
Makadirio ya matokeo hufanywaje?
Huwa kuna shinikizo kwa vituo vikubwa vya runinga Marekani, kila kituo kikitaka kuwa cha kwanza kutangaza mshindi, kabla ya kura zote kuhesabiwa, shughuli ambayo huchukua siku kadha.
Lakini shinikizo zaidi huwa katika kuhakikisha matokeo yanayotangazwa na vituo hivyo ni sahihi.
Hakuna anayetaka marudio ya 2000, pale vituo vya habari vilipolazimika kufuta matokeo ambayo vilikuwa vimetangaza kuhusu jimbo la Florida ambapo walimtangaza George W Bush kuwa rais mapema.
Vituo vya runinga huwa vina “madawati ya maamuzi”, yenye makundi ya wataalamu wa utafiti, takwimu na data ambao huwa kando na waandishi wa habari. Ni kazi ya wataalamu hao kutoa makadirio ya matokeo.
BBC itatumia makadirio ya wataalamu wa ABC News, mshirika wa BBC nchini Marekani, kwa ajili ya uchaguzi wa rais.
Kwa Bunge la Wawakilishi, Seneti na Gavana, BBC itatumia shirika la Associated Press, ambalo hukufanya data kuhusu upigaji kura kutoka kwa maafisa wa jimbo na maeneo husika.
Vituo vingine vingi hutumia AP na Edison Research, ambao hufanya utafiti kuuliza watu kuhusu uamuzi wao baada yao kupiga kura.
BBC haitafanya utafiti wake binafsi, kama ambavyo ingetarajiwa Uingereza.
Kinyume na vituo vingi vya Marekani, BBC haina uwezo wa kukadiria nani atashinda. Itaripoti makadirio ya wataalamu wa ABC, ambao watayatoa baada ya utathmini wa wataalamu kabla ya kura zote kuhesabiwa.
23:00 EST (04:00 GMT – Saa moja asubuhi Afrika Mashariki)
Vituo vya kura vitafungwa katika jimbo lenye umuhimu mkubwa uchaguzini kutokana na wingi wa wajumbe, California (55), ambayo ni ngome ya Democratic, pamoja na Oregon (7), Washington (12), Idaho (4) na Hawaii (4).
Kwa kutegemea hali itakavyokuwa, mshindi anatarajiwa kutangazwa wakati huu.
Kwa kufuata desturi, atakayeshindwa anatarajiwa kutoa hotuba ya kukubali kushindwa muda mfupi baadaye. Ilikuwa saa 00:00 EST (05:00 GMT) mwaka 2012 na 2008. Hata hivyo, mwaka 2004, John Kerry alisubiri hadi siku iliyofuata kukubali kushindwa.
Ukuzingatia madai ya Bw Trump kwamba kura zitaibwa, iwapo atashindwa, huenda akataka kura zihesabiwe tena au akatae kukubali kushindwa. Hilo likifanyika, hakuna ajuaye mshindi wa urais atatangazwa wakati gani.
01:00 EST (06:00 GMT – Saa 03:00 asubuhi Afrika Mashariki)
Jimbo la Alaska (3). Iwapo kutakuwa na ushindani mkubwa sana, jimbo hili huenda likawa na maana, lakini kawaida kufikia hapa mshindi huwa tayari amejulikana.
Wanakijiji Kenya ‘wampigia kura’ Clinton
Wakazi katika kijiji alikozaliwa babake Rais wa Marekani Barack Obama wameandaa uchaguzi wa mwigo ambapo mgombea wa Democratic Hillary Clinton ameibuka mshindi.
Bi Clinton amepata 78% ya kura dhidi ya Bw Trump aliyepata 22% kwa mujibu wa gazeti la The Star la Kenya.
Babake Obama, Barack Obama Sr. alitoka kijiji cha Kogelo, jimbo la Siaya, magharibi mwa nchi hiyo.
Nduguye wa kambo wa Rais Obama, Malik Obama, hata hivyo anamuunga mkono Bw Trump.
Akihojiwa awali, alisema anampenda sana Bw Trump kutokana na “uwazi wake” na kuongeza kwamba amesikitishwa sana na uongozi wa Rais Obama.
Aliambia BBC kwamba anaamini BwTrump, ni mtu mwenye huruma, mkweli na mwenye ushawishi.
“Akizungumza kwenye runinga anaonekana mtu anasemaye ukweli, kuhusiana na dunia kwamba imeharibika na hakuna usalama,” amesema Bw Malik.
Mambo mengine ya kufuatilia
Wamarekani pia wanawachagua Maseneta 34 (kati ya 100) na wabunge 435 wa Bunge la Wawakilishi. Democratic wanahitaji maseneta wanne kutwaa udhibiti Seneti na 30 kutwaa tena udhibiti Bunge la Wawakilishi.
Nyadhifa 12 za ugavana pia zinapigiwa kura.
20 Januari 2017
Rais mteule atasubiri hadi 20 Januari mwakani kuapishwa kuwa rais wa 45 wa Marekani. Hili limeelezwa vyema kwenye katiba. Rais mteule ataweka mkono wake kwenye Biblia na kula kiapo saa sita mchana. Kuanzia hapo, atachukua udhibiti wa serikali.
Wataingia pia White House. Kawaida, rais anayeondoka na mkewe huandalia Rais anayeingia mamlakani na mkewe dhifa kabla ya sherehe ya kuapishwa. Saa sita baadaye, familia mpya huingia ikulu.
Imeletwa kwenu kwa hisani ya Gpl.
No comments:
Post a Comment