Uchaguzi mkuu nchini Marekani utafanyika hapo kesho kuchagua atakayemrithi Rais Barack Obama. Je, hali ikoje sasa na nani ana nafasi nzuri ya kushinda?
Mwandishi wa BBC wa Amerika Kaskazini Anthony Zurcher anachambua:
Leo Jumatatu ni siku nyingine ambayo wimbi la uungwaji mkono linatarajiwa kubadilika, hasa baada ya FBI kutangaza kwamba hawajapata ushahidi dhidi ya Bi Hillary Clinton baada ya kuchunguza barua pepe zilizopatikana hivi majuzi.
Bi Clinton anaendelea kuongoza dhidi ya mgombea wa Republican Donald Trump kwenye kura ya maoni ya kitaifa ya Washington Post/ABC, uongozi wake ukiwa alama tano. Kwenye kura ya maoni ya IBD/TPP, Bw Trump anaongoza kwa alama moja.
Hivyo, ni vigumu kubaini hali halisi kutoka kwa kura za maoni.
Aidha, kura zote za maoni ambazo zimefanywa kufikia sasa hazikuzingatia habari za karibuni zaidi za FBI kumuondolewa Bi Clinton makosa.
Lakini kunaweza kukatokea jambo la kuwashangaza watu?
Ukitazama kura za maoni katika majimbo muhimu, kunaonekana kuwa na udhaifu kidogo kwenye ngome ya Clinton.
Hii inaweza kuwa ndiyo sababu Bw Trump anatumia muda mwingi sana kwenye kampeni majimbo ya Michigan, Wisconsin na New Hampshire.
New Hampshire, ni moja ya majimbo ambayo yameonekana kuunga mkono chama cha Democratic kwa dhati miezi ya karibuni, lakini sasa jimbo hilo linaonekana kushindaniwa sana. Si ajabu kwamba Bi Clinton na Rais Barack Obama wamepanga mikutano ya dakika za mwisho kuimarisha uungwaji mkono.
Na katika jimbo la Michigan, ambapo Obama alishinda kwa kuwa mbele alama 10 mwaka 2012, mambo hayaonekani kuwa salama sana kwa Democratic.
Lakini kuna habari njema kwa Bi Clinton kutoka Ohio, ambapo utafiti wa maoni uliofanywa na kampuni ya kuaminika unamuonesha akiwa mbele kwa alama moja (hata hivyo, alama hiyo moja bado imo eneo la makosa yanayoweza kutokea kwenye utafiti).
Ikizingatiwa kwamba upigaji kura za mapema unaonyesha watu wengi weusi, ambao ni wengi kiasi eneo hilo, hawajajitokeza sana, Bi Clinton amefika huko siku za karibuni kufanya kampeni.
Alihudhuria tamasha ya muziki ya rapa Jay-Z na nyota wa muziki wa pop Beyonce siku ya Ijumaa kisha akahudhuria hafla ya pamoja na nyota wa mpira wa kikapu LeBron James Jumapili.
Ushindi wa Clinton Ohio unaweza kuimarisha sana nafasi yake kushinda, kwa hivyo ishara za matumaini - baada ya kura kadha za maoni awali kuonyesha alikuwa nyuma ya Trump - ni habari njema.
Bi Clinton atafurahia hali jimbo la Nevada, ambapo kumekuwepo na foleni ndefu za wapiga kura wa mapema, ishara kwamba watu wa asili ya Hispania (Latino/Mexico) wamejitokeza kwa wingi.
Kwa jumla, ana nafasi nzuri ya kushinda ukimlinganisha na mpinzani wake lakini lolote linaweza kutokea.
Kwa mujibu wa:
- New York Times Upshot: Clinton ana uwezekano wa 84% kushinda
- FiveThirtyEight: Clinton ana uwezekano wa 65% kushinda
BBC.
No comments:
Post a Comment