PICHA HAIHUSIANI NA HABARI HUSIKA!
BILA shaka upo salama na unaendelea kuzikabili changamoto za maisha.
Usisahau kwamba hata wewe unaweza kuwa adui wa maisha yako wa kukata tamaa.
Yabadili matatizo kuwa changamoto na muombe Mungu akupe ujasiri upambane, ushindane hadi ushinde. Kumbuka, maisha ni kutafuta, atafutaye hachoki, akichoka amepata. Mtaji wa masikini ni nguvu zake, iga kazi usiige matumizi.
Kabla ya kuendelea natoa pole kwa wazazi na familia ya mtoto David Ndung’u (14) aliyeaga dunia baada ya mwalimu kumpiga Oktoba 3 mwaka huu kwa sababu alipata maksi za chini mtihani wa maswala ya jamii! Mtoto huyo mkazi katika kijiji cha Arash alikuwa akisoma darasa la nane katika Shule ya Msingi Subukia nchini Kenya.
Sikumshangaa mama wa marehemu, Elizabeth Nyokabi, akibubujikwa machozi wakati anazungumza na mwandishi wa habari kuhusu tukio hilo. Inauma sana kumpoteza mtoto kwa sababu eti amefeli mtihani. Inadaiwa kuwa mwalimu alimpiga mtoto huyo kwa viboko, mateke na vibao kwa kufeli na kulirudisha nyuma darasa.
Kabla ya kuaga dunia, David alimweleza mama yake kwamba, mwalimu amempiga sana kila mahali mwilini ikiwemo kichwani na alikuwa anaumwa. Mama huyo alimpa mwanawe dawa na kumaliza maumivu lakini kichwa kiliendelea kumuuma David, baadaye alizidiwa akashindwa hata kutembea, na alilazwa katika Hospitali ya Nyahururu akafariki dunia.
Mama wa mtoto huyo alisema mwanawe alimweleza kuwa, alikuwa anafikiria kutofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi kwa kuwa mwalimu alikuwa amemkatisha tamaa na alikuwa pia amechoka kupigwa shuleni.
Tukio la Kenya linanikumbusha yaliyotokea kwa mwanafunzi katika Shule ya Kutwa Mbeya na si vibaya hata wewe ukijiuliza kwamba, nini hasa mantiki ya kumwadhibu mtoto nyumbani au shuleni. Ninaamini kwamba, mtoto anaadhibiwa kuonywa ili ajirekebishe.
Kwa yanayotokea sasa, watoto wanaadhibiwa ili waumie hasa kimwili na kisaikolojia jambo ambalo si sahihi. Mtoto anakwenda shule kujifunza na si kuumizwa. Kama uwezo wa kuelewa masomo ni mdogo, kumpiga haisaidii kumwezesha mwanafunzi afaulu. Walimu acheni ukatili, zungumzeni na wanafunzi mjue kiichi cha matatizo badala ya kuwapiga.
No comments:
Post a Comment