BAADHI ya maneno katika lugha ya Kiswahili yameshazoeleka kiasi cha kutoweza kuyabadilisha kimatumizi. Mifano michache ni maneno kilo, uzito na futi. Maneno haya yanapotumika katika maisha ya kawaida huweza kuvumilika kwa kuwa watu wengi wanayaelewa na hayawapi matatizo yoyote. Matatizo yanaanza wakati wa kutumika kama istilahi hasa kwenye sayansi.
Tuanze na neno kilo. Ni jambo la kawaida kusikia watu wakisema, “nipe kilo moja ya nyama,” au “niuzie kilo tatu za sukari” au “nipimie kilo mbili za misumari ya inchi nne.” Mawasiliano hayana matatizo hapo. Muuzaji anachukuwa mizani yake na kuweka ‘mawe’ ya kupimia kulingana na mahitaji.
Lakini kilo sio kigezo cha upimaji. Ni neno linalotambulisha kiwango. Kwa mujibu wa kamusi ya Bayolojia, Fizikia na Kemia iliyotolewa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chapa ya pili 2004, neno kilo ni kiambishi awali cha SI chenye maana ya 1,000 (elfu moja).
Ndio sababu kwa mfano, urefu wa kilometa moja ni meta elfu moja. SI ni vipimo vilivyokubalika kimataifa kama vile meta, lita na gramu. Kipimo rasmi cha masi (jumla ya maada ya dutu) ni gramu.
Mara nyingi watu katika matumizi ya kawaida huita masi (uzani) lakini wanafizikia huzitofautisha dhana hizo. Kwa hiyo, gramu zinapotimia elfu moja hufanya kilogramu moja. Watu wanapozungumzia kilo huwa wana maana kilogramu.
Kiusahihi wangesema “kilogramu moja ya mchele, kilogramu tatu za unga wa ngano, na kadhalika.” Hii ni kwa sababu kusema ‘kilo’ unamaanisha SI 1,000 ambayo inaweza kuwa vipimo vya urefu yaani kilometa! Neno jingine, kama ulivyokwishaona hapo juu, ni uzani. Wengi wetu huuita uzito.
Hili ni neno lenye uhusiano wa karibu sana na masi. Wanasayansi wanafasili uzito kuwa ni kiasi cha masi katika kizio kimoja cha ujazo. Dutu huweza kuwekwa juu ya maji kujulisha kama ni kizito zaidi ya maji kwa ujazo unaolingana. Kikizama ni kizito kuliko maji.
Tunapolinganisha uzani tunajikuta tunazungumzia uzito. Hata hivyo, maana halisi ya uzani ni kani ya uvutano kati ya dunia na gimba au kitu. Kwa kifupi wanafizikia wanatafsiri neno ‘density’ kuwa ni ‘uzito’. Futi ni neno jingine lililozoeleka sana kwa Watanzania, na hata kwa jirani zetu. Vipimo vya metriki vimefundishwa katika shule zetu kwa muda mrefu sasa.
Si ajabu ukakutana na watu ambao hawaijui futi. Wanajua meta, sentimeta na kilometa. Wanalijua neno futi kwa mazoea tu. Wengine hawajui hata urefu wa futi moja. Wanaendelea kutumia kifaa kiitwacho ‘futi kamba’ ambacho ukikichunguza utakuta pengine kigezo chake ni meta na sentimeta na sio futi.
Neno jingine linaloleta utata katika matumizi ni mwendokasi. Hili neno hutumika katika maisha ya kawaida lakini pia ni istilahi. Utasikia mara kadhaa watu wakisema, ”Gari ilikuwa kwenye mwendokasi, kwa hiyo liligongana uso kwa uso na gari jingine lililokuwa linatokea pande wa pili.”
Wanachokusudia kusema ni kwamba mwendo wa gari hilo ulikuwa wa kasi sana. Kimsingi wangesema gari lilikuwa kwenye mwendo wa kasi. Mwendokasi ni istilahi inayofasiliwa kuwa ni umbali chombo kiliosafiri kwa muda fulani. Ina maana kuwa ukigawanya umbali kwa muda fulani unapata mwendokasi.
Kwa mfano, ikiwa gari limesafiri umbali wa kilometa hamsini kwa saa moja, tunasema mwendokasi wa gari hilo ni kilometa hamsini kwa saa.
Kama kuna shule karibu na barabara, madereva wanapaswa kuendesha magari yao kwa mwendokasi usiozidi kilometa thelathini kwa saa kuepuka kuwagonga wanafunzi na wapita njia wengine.
Tungependa kuona kwamba maneno hayo yanatumika kwa usahihi majumbani, shuleni na hata ofisini na muhimu zaidi kwa waandishi wa habari.
Tunakubali kuwa neno linaweza kuwa na maana zaidi ya moja lakini tusitumie fursa hiyo kuwaongezea wanafunzi matatizo. Sote tunajua sasa kuna vuguvugu la kufundisha masomo kwa Kiswahili katika ngazi zote za elimu.
Pia waandishi wameanza kuandika vitabu kwa kutumia istilahi za masomo hayo. Ni vizuri maneno yakatumika kwa maana iliyokusudiwa ili kusiwe na utata. Kama kuna kipimo cha metriki kilichozoeleka tofauti na ilivyotarajiwa ni hekta.
Kipimo tulichorithi kwa Waingereza ni eka kilichotokana na matumizi ya yadi. Watu wengi waliosoma wakati huo walijua kuwa eka ni eneo la mraba wenye yadi sabini kwa sabini.
Kwa kipimo kisichokuwa rasmi ilikuwa ni mraba wa hatua sabini kwa sabini na kilitumiwa sana na wanakijiji kupimia ardhi zao. Kipimo cha hekta ni mraba wenye meta mia moja kwa mia moja.
Nadhani unaona moja kwa moja jinsi hekta ilivyo rahisi kihesabu ukilinganisha na eka.
Eneo la hekta moja ni meta za eneo 10,000 ukilinganisha na eka ambayo ni yadi za eneo 49,000.
Meta 100 ni urefu unaokaribia urefu wa kiwanja cha mpira wa miguu. Ni rahisi kwa mtu kuona ukubwa wa hekta kwa kutumia mazingira hayo.
Kwa hilo, tunajipongeza.
No comments:
Post a Comment