Thursday, 4 August 2016

Zitto ampigia magoti Magufuli



KIONGOZI Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amemwomba Rais John Magufuli aruhusu mikutano ya kisiasa nchi nzima, umoja wa vijana wa chama hicho ulibainisha jijini jana.




Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za chama hicho, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo, Bakari Licapo, alisema chama hicho kimeingiwa na hofu ya kudhoofika na kufa iwapo Rais Magufuli hatalegeza msimamo wake wa kutoruhusu mikutano ya vyama vya siasa nje ya eneo la mshindi wa uchaguzi.
Wiki iliyopita, Rais Magufuli aliagiza kwamba shughuli za mikutano ya kisiasa zifanyike ndani ya jimbo la mbunge au diwani husika na kuhutubiwa na mshindi wa eneo husika.
Licapo alisema kufuatia agizo hilo, Zitto aliwaagiza viongozi wengine wa chama pamoja na wanachama, kumuandikia barua Rais Magufuli ili awaruhusu kufanya mikutano ya kisiasa.
“(Sasa) sisi vijana tumeamua moja kwa moja kwenda kutekeleza maagizo ya Kiongozi wa chama, Zitto Kabwe, kumuandikia barua Rais ili abatilishe agizo hilo na kuruhusu mikutano hiyo,” alisema Licapo.
Mwenyekiti huyo wa Ngome ya Vijana ya ACT alisema wanamuomba Rais azipokee barua hizo.
Ngome ya Vijana hiyo imesema endapo agizo la Rais litatekelezwa kikamilifu, mikutano ambayo itafanywa na chama hicho itakuwa ni katika Jimbo la Kigoma Kaskazini pekee.
Kwa upande wa madiwani, Licapo alisema mikutano ya ACT itafanyika katika kata 49 tu zilizochukuliwa na chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana, hali ambayo itadhoofisha na kukiathiri chama hicho kisiasa moja kwa moja.
Alieleza kuwa agizo hio ni msiba kwa chama hicho kutokana na kuwa na jimbo moja pamoja na kata chache za udiwani.
Tamko la wiki iliyopita ilikuwa mara ya pili kwa Rais kutoa agizo hilo, mara ya kwanza ikiwa Ikulu wakati akipokea taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Katika hafla hiyo, Rais Magufuli alisema sasa ni wakati wa serikali kutimiza ahadi ilizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi huo hivyo masuala ya siasa yasubiri hadi mwaka 2020.
Mbali na siasa, mkutano huo wa viongozi wa Ngome ya Vijana ya ACT-Wazalendo na waandishi wa habari uligusia masuala ya elimu.
Mratibu wa Elimu wa chama hicho, Kitentya Luth, alisema Rais Magufuli kama ana nia ya dhati ya kuboresha elimu nchini anatakiwa kutoa agizo jipya.
Alimtaka kuwaamuru watumishi wa umma, wabunge, wakuu wa mikoa na mawaziri kuwasomesha watoto wao katika shule za umma ili kuondoa matabaka kati ya shule hizo na za binafsi.
Alisema agizo hilo litakuwa ni mwarobaini wa uboreshaji wa shule za umma kwa sababu viongozi hao ni moja ya wadau wakubwa wa kusimamia na kupanga sera za elimu nchini.
“Iwapo watoto wao watasoma katika shule za umma, watatunga sera nzuri na kusimamia vizuri (elimu) kwa kuwa inagusa vizazai vyao,” alisema Luth.
Imeandikwa na Christina Mwakangale na Hanifa Ramadhani

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!