Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata.

 

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kuzindua mpango huo jijini Dar es Salaam jana, Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, alisema mpango huo una lengo la kubadili mfumo wa sasa wa kuhifadhi kumbukumbu za walipakodi ili kuendana na ukuaji wa teknolojia.
Kidata alisema mpango huo pia umelenga kuwawezesha kuwa na idadi sahihi ya walipakodi, kuondoa walipakodi hewa na wale ambao wamekuwa hawajihusishi na biashara kutokana na sababu mbalimbali, zikiwamo za vifo.
Pia alisema kupitia mfumo huo, wanatarajia kuboresha huduma za ulipaji wa kodi na kuongeza ufanisi katika suala la usimamizi wa ukusanyaji kodi kwa kiwango cha juu na kufikia katika malengo ambayo wamejiwekea ya ukusanyaji mapato na kuwezesha gharama za ulipaji kodi kuwa nafuu na walipakodi kulipa kwa hiari.
"Mfumo tunaoutumia sasa wa kutoa namba za utambulisho, una upungufu mkubwa, si wa kisasa na pia unaonyesha idadi kubwa ya walipakodi wakati wengine si walipakodi. Kwa hiyo huu wa sasa utatusaidia kufika pale tunapotaka kwa sababu wale watakaoingizwa watakuwa ni wanaostahili tu," alisema Kidata.
"Uhakiki huu utafanyika nchi nzima, lakini kwa sasa tunaanza na mikoa ya kikodi ya Dar es Salaam, Ilala, Kinondoni na Temeke kwa kipindi cha miezi miwili na baada ya hapo tunakwenda nchi nzima. Ni vema wananchi watambue umuhimu wa uhakiki wa namba zao, waende katika ofisi za TRA katika maeneo yao kwa sababu uhakiki hauchukui muda mwingi,” aliongeza.
Naye Kamishna wa Mapato ya Ndani, Elijah Mwandumbya, alisema kwa wale watakaoshindwa kuhakiki namba zao, wataondolewa katika orodha ya wamiliki wa namba hizo na watashindwa kuendesha shughuli zao zinazohitaji TIN.
Alisema kwa wale watakaokaidi kuhakiki namba zao na wakaendelea kuzitumia, watachukuliwa hatua kali za kisheria watakapobainika.
Alisema idadi ya Watanzania wenye TIN mpaka sasa ni milioni 2.18 japokuwa siyo wote wanaopata huduma kwao.
Alisema usajili wa namba hizo ulianza juzi, lakini bado wananchi wengi hawajapata mwamko kwa kuwa ndio unaanza.