Rais Magufuli (Kulia) akimjulia hali Mzee John Malecela
(Katikati) nyumbani kwake. Kushoto ni mke wa John
Malecela mama Anna Kilango Malecela
Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli leo amewatembelea na kuwajulia hali Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe. Job Ndugai na Makamu wa Rais Mstaafu
wa Tanzania na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Samuel
Malecela Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na kuwajulia hali, Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone na kupata nguvu haraka ili waweze kuendelea na majukumu yao ya kawaida katika ujenzi wa Taifa.
Akizungumza na Rais Magufuli nyumbani kwake Salasala Jijini Dar es Salaam spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai amemshukuru Rais Magufuli kwa kumtembelea, kumjulia hali na kufuatilia kwa ukaribu wakati wote alipokuwa akipata matibabu nchini India hadi aliporejea hapa nchini.
"Kwa kweli nimefarijika sana, kwanza naomba nimshukuru sana Mhe. Rais kwa sababu nilipopata matatizo haya ya maradhi alikuwa karibu sana na mimi nikiwa hapa nchini na hata nilipopelekwa nchini India alinipigia simu mara kwa mara na kunifariji sana, na hapa amekuja kuniona kwa niaba ya watanzania kwa kweli namshukuru sana na namuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa moyo huu wa kuwajulia hali wale wenye matatizo mbalimbali"
Lakini niwahakikishie Watanzania, kwamba kwa sasa nina nafuu kubwa sana, naweza kufanya kufanya kazi nyingi tu sasa lakini tuendelee kuombeana" Ameeleza Mhe. Ndugai alipokuwa akizungumzia hali yake kwa sasa.
Kwa upande wake Makamu wa Rais Mstaafu na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. John Samuel Malecela pamoja na kumshukuru Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli kwa kumtembelea amesema afya yake inazidi kuimarika na pia amewashukuru Madaktari wanaompatia matibabu.
"Mheshimiwa Rais nakushukuru sana, namshukuru pia Mama Janeth Magufuli kwa kunitembelea na kunifariji, naendelea vizuri na matibabu na afya yangu imeimarika kwa kiasi kikubwa" Ameeleza Mhe. Malecela.
Rais Magufuli mara baada ya kufanya mazungumzo na Spika Ndugai, wakapiga picha ya pamoja akiwa na mke wake pamoja na mke wa Ndugai.
Wakifanya maombi
No comments:
Post a Comment