UGONJWA wa homa ya ini (Hepatitis B) umetajwa kuwa hatari, usio na tiba na unaoua idadi kubwa ya watu kimya kimya na kwamba kati ya watu 100, watu wanane wanaweza kuwa na uambukizi sugu wa ugonjwa huo. Kadhalika, maambukizi ya ugonjwa huo ni makubwa mara 10 zaidi ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na kwamba asilimia kubwa ya wagonjwa huugundua wakati uko kwenye hatua za mwisho na hivyo kusababisha mgonjwa kupoteza maisha.
Akizungumza na gazeti hili kwenye mahojiano maalumu kuhusu ugonjwa huo nchini, daktari bingwa wa magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Tumbo na Ini, Idara ya Tiba katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk John Rwegasha alisema tatizo la ugonjwa huo ni kubwa.
Alisema ugonjwa wa homa ya ini aina ya (Hepatitis B na C) ndio unaoshambulia zaidi Watanzania na wengine wa nchi za Afrika Mashariki kuliko aina nyingine ya ugonjwa huo, ukiwemo Hepatitis A, D na aina nyingine.
Akifafanua, alisema unaenezwa na virusi aina ya Hepatitis B (HBV), ambavyo vinapoingia mwilini mwa binadamu, vinashambulia ini pekee na hivyo kulifanya wakati mwingine lisinyae na hatua mbaya zaidi ni mwathirika kupata saratani ya ini.
“Ni ugonjwa mbaya na hatari unaoua kimya kimya na wengi wetu hatuutilii maanani kama ugonjwa hatari, na maambukizi yake ni makubwa mara 10 zaidi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi,” alisema Dk Rwegasha.
Akielezea kwa undani ugonjwa huo aina ya Hepatitis B na C, alisema mtu mwenye maambukizi ya mojawapo ya aina hizo mbili za homa ya ini, anaweza kuishi kati ya miaka mitano hadi 20 bila kugundua kama ana ugonjwa huo, hadi pale dalili zinapoanza kujitokeza.
Alisema kwa kawaida dalili za ugonjwa huo zinapojitokeza, ni hatua za mwisho za ugonjwa ambapo ini huwa limeshaharibiwa kiasi kikubwa na hivyo tiba za magonjwa nyemelezi hutolewa kusaidia kuyapunguza makali, na wakati mwingine ini huwa limeshambuliwa na saratani na hivyo nafasi ya mgonjwa kuishi hupungua na kuwa chini ya kipindi cha mwaka mmoja.
Hepatitis B
Akizungumzia aina hiyo ya homa ya ini, Dk Rwegasha alisema hiyo ni moja ya ugonjwa unaoongoza kwa maambukizi nchini na kwamba virusi vyake vinapoingia mwilini vinaleta usugu na kuathiri ini. Alisema kwa mujibu wa taarifa za kitabibu, asilimia 95 ya watu wazima walioambukizwa ugonjwa huo hupona wenyewe bila tiba na hiyo inategemea kinga za mgonjwa katika mwili wake.
Alifafanua kuwa asilimia tano iliyobaki ndiyo mgonjwa huendelea kuwa na vimelea hivyo na kuwa sugu na hatimaye mgonjwa anapopimwa hubainika kuathirika na wengi hufa kutokana na magonjwa nyemelezi, yakiwemo saratani ya ini na wakati mwingine viungo vya ndani kama figo kushindwa kufanya kazi.
Wakati kiwango cha kupona wenyewe kwa watu wazima kikiwa kikubwa, kwa watoto takwimu za kitabibu kwa mujibu wa Dk Rwegasha ni kwamba asilimia 10 ya watoto walioambukizwa ugonjwa huo hupona wenyewe na asilimia 90 huendelea kuwa na virusi hivyo hadi pale dalili za ugonjwa zinapoanza kuonekana, hatua ambayo wakati mwingine huwa ni ya mwisho.
Hepatitis C
Akizungumzia aina hii ya homa ya ini, alisema watu walioambukizwa ugonjwa huo asilimia 80 virusi hivyo huendelea kushambulia ini na ugonjwa kuwa sugu ambapo uwezekano wa mgonjwa kupata saratani ni mkubwa sambamba na ini kusinyaa.
Hata hivyo, kwa nchi za Afrika Mashariki, Tanzania ikiwemo, uambukizi sio wa kiwango cha juu kama ilivyo kwa aina ya B, ambapo kwa aina hiyo C, kati ya watu 100, watu wawili ndio wameambukizwa. Dalili Alisema mtu mwenye ugonjwa huo ni vigumu kumtambua hadi pale vipimo vya damu vitakapofanywa na kwamba kwa nchini, hakuna mazoea ya kupima ugonjwa huo, hadi pale dalili zinapokuwa zimeanza kuonekana kwenye mwili wa mtu.
Alizitaja dalili zake kuwa ni pamoja na homa, tumbo kuuma upande wa juu, kichwa, mafua, macho kuwa njano na wakati mwingine hata mkojo kuwa njano na pia wakati mwingine mtu aliyeathirika na ugonjwa huo hana dalili.
Alisema ugonjwa ni hatari na wakati mwingine zaidi ya Ukimwi kwa sababu unaua watu wengi kimya kimya, na mtu anapogundua kuwa ameathirika na tatizo hilo, huwa ni kwenye hatua za mwisho na hivyo mgonjwa hupoteza maisha.
Maambukizi Alisema mtu mwenye maambukizi ya ugonjwa huo, huambukiza wengine kwa njia ya kuongezewa damu yenye virusi vya ugonjwa huo, kujamiiana, kujidunga sindano yenye virusi vya ugonjwa huo, majimaji ya mgonjwa kumpata mtu mwingine kama ana kidonda, pia mama anaweza kumuambukiza mtoto wakati wa kujifungua.
Alitoa mfano kuwa, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa waliolazwa kwenye wodi ya magonjwa ya mfumo wa chakula na ini, wamegunduliwa kuwa na Hepatitis B. Tiba Dk Rwegasha, akizungumzia tiba alisema kwa waliogundulika kuwa na Hepatitis B, hakuna, bali kuna dawa za kupunguza makali ya virusi ambayo hutumiwa na mgonjwa kwa kipindi chote cha uhai wake.
Alisema pamoja na kutokuwa na tiba, lakini chanjo ya ugonjwa huo, na hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya virusi hivyo na huwa kinga kwa kipindi cha maisha yake yote.
Kwa wenye maambukizi ya virusi aina C, tiba ipo, ingawa hakuna chanjo na kwamba tiba yake ni ghali na mgonjwa huwa kwenye tiba kwa muda wa miezi mitatu hadi sita, na gharama ya dawa ni kati ya Sh Milioni tatu hadi tano, kulingana na muda wa tiba.
Mikakati ya kuzuia Dk Rwegasha alisema mikakati ni kuongewa uelewa wa wananchi juu ya ugonjwa huo akiongeza kuwa, hata kwa baadhi ya wataalamu wa tiba wanashindwa kuuelezea ugonjwa wenyewe, jambo linalosababisha maambukizi kuendelea kwa kasi na kuongeza tatizo nchini.
Kauli ya serikali Akizungumzia ugonjwa huo na hatua zinazochukuliwa na serikali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema ni kweli ugonjwa huo umekuwa tishio na haujapewa kipaumbele cha kutosha.
Alisema maambukizi ya ugonjwa huo nchini yanaongezeka na kwamba pamoja na kuongezeka huko nchi haikuwa na takwimu sahihi zinazoonesha ukubwa wa tatizo, ingawa lipo na kwamba hivi sasa wizara imeanza mchakato wa kufanya marejeo ya sera ya afya ya mwaka 2007, ili kuingiza ugonjwa huo kwenye magonjwa ya vipaumbele.
Ameibainisha kuwa, serikali ilitilia mkazo zaidi kwenye chanjo kwa watoa huduma walio kwenye sekta ya afya tena kwa wale wanaohusika zaidi au moja kwa moja na wagonjwa wa ugonjwa huo, na kuongeza kuwa kutokana na ukubwa wa tatizo kuna haja sasa ya kuangalia sera ya afya.
Alisema baada ya kufanya mapito ya sera hiyo wataangalia jinsi ya kujikita zaidi kwenye kinga ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, ambao idadi kubwa ya wananchi hawana uelewa wa ugonjwa huo na athari zake, hadi pale mgonjwa anapougua.
No comments:
Post a Comment