Monday, 25 July 2016

Utumikishwaji umemwondolea mtoto huyu ‘utoto’ wake

KATIKA mtaa mmojawapo jijini Dar es Salaam, namshuhudia mtoto.
Namkadiria kuwa na umri kati ya miaka 10 na 12. Anachuuza karanga. Inasikitisha kuona mtoto huyo, akifanya shughuli hiyo katika mazingira ambayo si rafiki kwake. Maana yuko peke yake; hana uangalizi wowote . Anavuka barabara bila kujali hatari ya kugongwa na magari. Lakini pia, ananiambia kuwa hulazimika kupita baa moja hadi nyingine kusaka wateja wa kununua karanga hizo.


“Nazunguka maeneo mengi...mpaka karanga ziishe,” anasema Majuto (si jina halisi) ambaye anaweka bayana kuwa kutwa hushinda mtaani akiuza karanga. Anasema hasomi shuleni. Anasema alitoka kijijini katika mkoa mmojawapo kwa lengo la kwenda jijini Dar es Salaam kutafuta kazi. Anadokeza kuwa ameajiriwa na mama mmoja mkazi wa Magomeni na hulipwa ujira wa Sh 20,000 kwa mwezi na pia kupewa chakula.
Dakika chache nilizozungumza na mtoto huyo, ananieleza hali halisi ya maisha ya nyumbani kuwa ni ya umasikini. Anasema ‘tajiri’ anayemuuzia karanga, alimfuata kijijini kwao na akaomba wazazi wake aende naye Dar es Salaam kumfanyia kazi. Ninapomuona Majuto, narejea pia kwa watoto wengi wanaotumikishwa kwa kuajiriwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo majumbani, uchimbaji madini, uvuvi, kilimo, baa, hotelini, ujenzi na ukataji mbao.
Hawa ndiyo watoto ambao wameoneshwa kwenye utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na matokeo yake kutolewa hivi karibuni jijini Dar es Salaam. Utafiti huo ni wa Utumikishwaji wa Watoto wa mwaka 2014 (2014 NCL), Tanzania Bara ambao umeonesha ukubwa wa tatizo la utumikishwaji watoto. Matokeo ya utafiti huo yameonesha kati ya watoto milioni 15 wenye umri kati ya miaka 5 -17, watoto milioni 4.2 sawa na asilimia 28.8 (akiwemo Majuto), wanatumikishwa katika kazi mbalimbali za kiuchumi.
Utumikishwaji au ajira za watoto katika jamii , unafanyika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo changamoto za kiuchumi katika jamii nyingi za Waafrika. Hili ni tatizo linaloonekana kuathiri ukuaji wa watoto na maendeleo yao shuleni na hata kuchangia changamoto katika mfumo wao wa maisha ya kila siku. NBS kupitia matokeo yake ya utafiti, inaweka bayana kwamba, hali ya utumikishwaji wa watoto nchini; hususan katika kazi hatarishi kwa maisha yao, ni changamoto kubwa inayokabili wananchi wengi hasa waishio maeneo ya vijijini.
Utafiti huo wa NBS kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,Kazi,Ajira, Vijana, Wenye Ulemavu ; Shirika la Kazi Duniani (ILO) pamoja na Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) unaweka bayana ukubwa wa tatizo hilo la utumikishwaji watoto kwenye kazi za kiuchumi na zisizo na hatari zinazowakabili.
“Lengo la utafiti huo ni kupata viashiria vya hali ya watoto wanaofanya kazi za kiuchumi na zisizo za kiuchumi, hali ya utumikishwaji wa watoto, utumikishwaji wa watoto kwenye kazi na mazingira hatarishi, hatari mbalimbali ambazo watoto wanapata,” anasema Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa.
Anasema, “Utafiti huo hufanyika kila baada ya miaka mitano na utafiti wa mwisho ulifanyika mwaka 2006/2007.Tafiti hizo hutakiwa kufanyika kila baada ya miaka mitatu au kila robo ya mwaka kwa nchi zenye uwezo wa kukusanya takwimu hizo.” Anasema Sekta ya Kilimo, Misitu na Uvuvi imeendelea kuwa sekta inayoajiri watoto wengi zaidi ikiwa na kiwango cha asilimia 92.1 ya watoto wote wanaojihusisha na shughuli za kiuchumi na wengi wao wanaishi vijijini.
Anasema athari wanazozipata watoto hao kwa kujihusisha na ajira ni pamoja na za kiafya, kisaikolojia, mahudhurio shuleni na nyinginezo zinazomnyima mtoto fursa ya kupata haki yake ya utoto na maendeleo ya baadaye ikizingatiwa kwamba, watoto ni taifa la kesho. Dk Chuwa anasema matokeo ya utafiti huo ni changamoto kwa serikali na wadau wengine kufuatilia na kutathmini malengo yaliyowekwa.
Malengo hayo yako katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na mipango mingine ya Maendeleo ya nchi ukiwemo Mpango wa Kwanza wa Maendeleo ya Taifa ulioishia mwaka 2015/2016 na pia Malengo Endelevu na Maendeleo ya Dunia ya mwaka 2030 kuhusu haki ya kumlinda na kuendeleza maendeleo ya watoto. Licha ya Tanzania, takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) za mwaka 2000 hadi 2012, zinaonesha utumikishwaji wa watoto umekuwa ni tatizo kubwa duniani.
Asilimia 11 ya watoto wote duniani wenye umri kati ya miaka mitano na 17 wanatumikishwa kwenye ajira za aina mbalimbali. Serikali kupitia Naibu Waziri wa Nchi-Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Dk Abdallah Possi inaitikia mwito wa Dk Chuwa juu ya umuhimu wa kufanyia kazi takwimu hizo kwa lengo la kukabili tatizo la utumikishwaji watoto. Dk Possi anasema serikali itaendelea kupambana vikali na kupinga utumikishaji wa watoto nchini na kuhakikisha kiwango hicho cha asilimia 28.8 kinapungua kwa kasi kubwa.
Miongoni mwa mikakati ya serikali inayotajwa na Naibu Waziri kuwa imeshafanyika kukabili tatizo, ni uanzishwaji wa mpango wa elimu bure ambao umehamasisha wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shuleni na hivyo kupunguza tatizo la ajira za utotoni. “Matokeo ya utafiti yameonesha kuwa utumikishwaji wa watoto unaendelea kuongezeka kadri umri unavyokuwa na hii inatokana na watumikishaji kuhitaji watoto wenye nguvu nyingi kuliko tija hivyo kufanya watoto wenye umri mkubwa zaidi kukosa fursa ya kupata elimu,” anasema Dk Possi.
Anasema serikali itahakikisha inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kwa dhati kupata takwimu sahihi kwa ajili ya maendeleo ya watoto na taifa kwa ujumla. Anaiomba ILO kuendelea kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kufanya uchambuzi zaidi wa kitaalamu kupata makadirio ya viwango vya utumikishwaji wa watoto katika ngazi za chini ikiwemo wilaya na mikoa ili kupata hali halisi .
Pia anawashukuru wadau wengine wa maendeleo, ikiwemo ILO, Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) na Shirika la Idadi ya Watu Duniani, DFID, Benki ya Dunia na Canada kwa michango ya kifedha na kiufundi iliyowezesha kukamilika kwa utafiti huo ambao haukuibua tatizo la utumikishwaji pekee, bali pia na matumizi mabaya ya muda kwa watoto. Utafiti huo umebaini watoto wanatumia muda mwingi katika starehe badala ya kusoma kwa bidii na maarifa.
“Matokeo ya starehe hizi ni mimba za utotoni ambazo zimeendelea kuongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2012 hadi asilimia 27 mwaka 2015. Hii ni changamoto ambayo serikali inaifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuweka sheria kali kwa wale watakaobainika kuwapa mimba watoto ,” anasema Dk Chuwa.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, watoto hutumia zaidi ya nusu ya muda wao wa siku; Yaani asilimia 58.8 kwa shughuli za kujihudumia na usafi binafsi, huku wasichana wakionekana kutumia muda mrefu zaidi kwa shughuli hizo, kwa kiwango cha asilimia 59.2 ikilinganishwa na wavulana wanaotumia asilimia 58.3,” anasema Dk Chuwa wakati wa kutoa matokeo.
Dk Chuwa anasema shughuli za kujisomea kwa watoto zilichukua nafasi ya pili kwa matumizi ya muda kwa kiwango cha asilimia 15.5 ambapo wavulana walitumia muda mrefu zaidi kwa shughuli za kujisomea ambao ni asilimia 16.4 ikilinganishwa na wasichana waliotumia wastani wa asilimia 14.6.
Anasema hali hiyo haiendani na Kauli ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Hapa Kazi Tu, kutokana na watoto kutumia muda mwingi katika starehe badala ya kusoma kwa bidii na maarifa ili kuwa na taifa la kesho lenye wasomi wanaokwenda na wakati kwa maana ya kutumia teknolojia ya kisasa na kuongeza tija katika uzalishaji na kuongeza uchumi na hatimaye kupunguza umasikini.
Hata hivyo anasema matumizi ya muda unaotumika kwenye starehe ni jukumu la mazazi na jamii kukabiliana nayo. Anahimiza pia utaratibu wa kusoma na kuratibu matumizi ya runinga kwa watoto kwa kufuatilia aina ya vipindi. Mkurugenzi huyo wa NBS anasisitiza wadau wote kuendelea kuchambua takwimu hizi zinazotokana na utafiti, kwa lengo la kutoa elimu zaidi kwa umma kuhusu mapambano dhidi ya utumikishwaji wa watoto.
Kwa ujumla, matokeo haya ya utafiti yanapaswa kumgusa kila mtu katika jamii kuhakikisha Majuto na watoto wenzake wananusuriwa kwenye ajira. Ingawa zipo sababu nyingi zinazosababisha utumikishwaji huu, mojawapo ikiwa umasikini wa familia za watoto husika, takwimu hizi zitumike kubuni mikakati ya kunusuru watoto hawa na athari za kimwili, kisaikolojia hatimaye, warudishiwe utoto wao uliopotea kutokana na kuingia kwenye ajira zikiwemo hatarishi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!