WAKAZI wawili wa vijiji vya Gokeharaka na Masangura, wilaya ya Kurya, nchini Kenya, wameuawa na wananchi wenye hasira baada ya kukurupushwa usiku na kukamatwa katika kijiji cha Nyabisaga, kata ya Pemba, wilayani hapa.
Diwani wa Kata ya Pemba, Ngocho Seronga, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyabisaga, Sagamo Nyamang'ondi na Mtendaji wa kijiji hicho Gasirigwi Chach, waliliambia Nipashe mwishoni mwa wiki kuwa, watu hao ambao wanadaiwa kuwa majambazi kutoka nchini Kenya walikuwa na bunduki walivamia kijiji hicho usiku wa saa 3:00 kwa nia ya kutaka kufanya uhalifu, lakini wananchi waliwabaini na kupeana taarifa na kujipanga kukabiliana nao.
Alisema wananchi waliokuwa eneo hilo walipiga mayowe yaliyosababisha wanakijiji wengi kujitokeza na kuanza kuwafukuza watu waliokuwa na bunduki na mapanga na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wwaili kati ya wanne.
Alisema watuhumiwa wawili akiwmo aliyekuwa na silaha walifanikiwa kutoroka na kuingia nchini Kenya.
"Wananchi waliokuwa na hasira waliwashambulia huku wakiwahoji ambapo mmoja alipoteza maisha palepale na mwenzake alipoteza maisha kabla ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya Tarime,” alisema.
Alisema kundi la majambazi wanaodaiwa kutokea nchini Kenya limekuwa likiwasumbua wananchi wa vijiji vya mipakani upande wa Tanzania, hasa vya Borega, Kebeyo, Nyabisaga, Gwitiryo, Pemba, Kyoruba na Sirari kwa kuwashambulia na kupora mali na kutokomea nchini humo katika vijiji vya Nyamaranya, Nyametaburo, Masangura, Gokeharaka na Kurutiange.
Polisi wilayani hapa wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Andrew Satta, amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea, huku akiwahimiza wananchi kutojichukulia sheria mkononi badala yake wanapowakamata watuhumiwa badala yake wawapeleke katika vyombo vya sheria
No comments:
Post a Comment