Sunday, 24 July 2016

Umasikini unatumikisha watoto


HUWA inauma sana ninapokuta mtoto akifanya kazi zisizolingana na ‘utoto’ wake.


Watoto wengi wamekuwa wakifanyishwa kazi zinazowadhulumu utoto wao, zinawanyima maendeleo ya kimwili na kiakili na nyingine kuwavunjia hadhi na heshima yao. Ukitaka kushuhudia ukweli juu ya hili, tembelea maeneo ya uchimbaji madini ambako wamekuwa wakishuhudiwa watoto wakilazimika kuingia migodini ama kuchimba au kwenda kutega baruti. Nenda baadhi ya baa, ambako unakuta mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 anafanyishwa kazi za kuuza vileo hadi usiku wa manane.
Ikiachwa uhalisia wa kazi yenyewe kutokuwa rafiki kwa mtoto, bado malipo yanapatikana kwa njia zinazoendelea kumdhalilisha na kumvunjia heshima. Ukifika mitaani nako, hususan mijini, wanashuhudiwa watoto wadogo wakichuuza bidhaa mbalimbali barabarani.
Licha ya kukabiliwa na hatari ya kugongwa na magari, kupigwa jua muda mrefu na hata kunyeshewa na mvua, watoto hao huhimili matatizo hayo kwa lengo la kupata chochote. Bado wamekuwa wakishuhudiwa baadhi ya watoto wakifanya kazi za umakenika, wengine wakisukuma mikokoteni, ujenzi, uvuvi na nyingine wasizostahili kufanya.
Watoto wengi wamekuwa wakilazimika kutumikishwa kwenye maeneo/ kazi hizo ambazo nyingi ni hatarishi huku sababu kuu ninayoiona ikiwa ni umasikini. Wapo wanaofanya kazi hizo kwa baraka za wazazi na wengine kwa msukumo wao wa kupata mahitaji ambayo hayawezi kupatikana ndani ya familia.
Ingawa lipo kundi la watoto ambao utukutu unaweza kuwafanya walazimike kuingia kwenye kutumikishwa, hao ni wachache ikilinganishwa na wanaosukumwa na umasikini. Ninaposema utukutu, namaanisha baadhi ya watoto ambao hutoroka nyumbani kwa kufuata mkumbo na kujiingiza kwenye ajira zisizolingana na umri wao.
Itakumbukwa kwamba, Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali inayohimiza kulinda watoto dhidi ya utumikishwaji. Mfano, Mkataba namba 138 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) wa mwaka 1998, umeainisha umri ambao mtoto anaweza kufanya kazi.
Mkataba huo umetoa nafasi kwa nchi wanachama kuweka umri kulingana na muundo wake wa kielimu. Mkataba mwingine ni namba 182 wa mwaka 2001 unaozuia watoto kutumikishwa kwenye mambo mabaya kama vile vitani. Pia upo mkataba wa mwaka 1989 ulioridhiwa na Tanzania mwaka 1991 kuhusu haki za watoto.
Tanzania katika kuunga mkono juhudi hizi za kimataifa za kupambana na ajira kwa watoto, mwaka 2004 ilitungwa sheria ikiainisha umri wa mtoto kuingia kazini miaka 14. Lakini bado chini ya sheria hiyo, inasisitizwa ajira husika zisiwe kwa kazi ambazo ni za hatari kwa afya ya mtoto na pia zisiwe katika mazingira yasiyofaa.
Hivi karibuni, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imezindua matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka 2014 juu ya utumikishwaji wa watoto na kuonesha tatizo bado lipo. Matokeo hayo ya utafiti wa utukishwaji wa watoto wa mwaka 2014, Tanzania Bara yameonesha kati ya watoto milioni 15 wenye umri kati ya miaka mitano hadi 17, watoto milioni 4.2 sawa na asilimia 28.8 wanatumikishwa katika kazi mbalimbali za kiuchumi.
Ingawa takwimu za utafiti huo zinaonesha kushuka kwa kiwango cha utumikishwaji kutoka asilimia 31.1 za mwaka 2006 hadi asilimia 28.8 za 2014, bado tafiti hizi zinapaswa kufumbua macho na kufungua masikio ya serikali na wadau wengine kutafuta namna ya kukabili tatizo hili.
Utafiti umeonesha ukubwa wa tatizo na sasa kilichobaki, ni serikali na wadau wengine kujikita katika kukabili chanzo cha tatizo. Kama nilivyosema awali, umasikini ndiyo chanzo kikubwa. Kama alivyoelekeza Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa, ufuatiliaji na tathmini unapaswa ujielekeze katika kutekeleza malengo yaliyowekwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na mipango mingine ya maendeleo ya nchi, yakiwemo malengo endelevu na maendeleo ya dunia ya mwaka 2030 kuhusu haki ya kumlinda na maendeleo ya watoto.
Pamoja na takwimu za Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuonesha utumikishwaji watoto ni tatizo la kidunia, haiondoi ukweli kwamba hapa nchini tunahitaji mikakati yetu madhubuti ya ama kupunguza tatizo au kukomesha. Jukumu hili la kukomesha utumikishwaji lazima liguse kila mmoja katika jamii.
Wakati serikali ikiangaliwa kuwa mdau wa kwanza wa kusaka mikakati ya kukabili tatizo ikiwemo kukabili umasikini uliopindukia, bado mzazi na mlezi anapaswa kujitathmini anavyochangia tatizo.
Lakini pia, watu wanaokubali kutumia umasikini wa watoto hao na familia zao kuwatumikisha, pia wanapaswa wakubali kuelekezewa vidole kutokana na kuchangia tatizo kuendelea. Hata hivyo nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa mpango wake wa elimu bure ambao naamini utanusuru watoto kadhaa waliolazimika kuacha masomo kutokana na kukosa ada na michango mingine.
Matokeo yake, waliona suluhu ni kwenda kutumikishwa katika kazi mbalimbali. Watoto wengine licha ya kuendelea na masomo, walikuwa watoro kwa sababu ya ama kulazimishwa na familia au wenyewe kwenda kutafuta vibarua wapate ada na michango mingine ya shuleni.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!