Monday, 11 July 2016

Serikali yashiriki msiba wa watu 9 waliozama Ruvuma

MIILI yote tisa ya watu waliozama katika ajali ya kivuko cha mto Ruvuma iliyotokea hivi karibuni, akiwemo mtoto wa miezi mitano, imepatikana na maziko kufanyika kwa ushirikiano wa familia na serikali.


Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Dk Binilith Mahenge, ilisema kuwa miili iliyopatikana ni ya watu wote waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
Taarifa hiyo iliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Omari Jela (11), Fadhili Hamis (8), Hadija Said (41), Zulfa Ally (14), Awetu Mohamed (14), Omar Waziri (13), Stumahi Abdallah (miezi 5), Rajabu Machupa (17) na Tupishane Mustafa (5).
Ajali hiyo ilitokea Julai 2, mwaka huu, saa 8: 00 mchana ikihusisha boti iliyokuwa ikitoka kijiji cha Mkenda Songea kwenda kijiji cha Mitomoni Nyasa. Boti hiyo inakadiriwa ilibeba watu kati ya 30 na 50 ambao baada ya ajali, tisa walizama na 36 waliokoloewa. Kazi ya kutafuta miili ilianza Julai 3 na kukamilika Julai 9.
“Napenda kuwajulisha wananchi wa Ruvuma na taifa kwa ujumla kuwa miili yote tisa ya watu waliozama imepatikana. Taratibu za mazishi zimefanyika kwa familia zikishirikiana na Serikali,” alisema.
Serikali imewapongeza wote walioshiriki kufanya kazi hiyo ya utafutaji wa miili .
“Kipekee inawashukuru wananchi wa vijiji vya Mkenda na Mitomoni kwa ushirikiano wao walioutoa kwa kikosi kazi nilichokiunda kusimamia zoezi la utafutaji miili,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa katika taarifa hiyo.
Alipongeza pia uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwa kutoa boti ya kisasa iliyofanya kazi kubwa ya kutafuta miili ndani ya mto Ruvuma na kufanikisha upatikanaji wa maiti wote.
Kutokana na ajali hiyo, Mahenge aliwataka Wakuu wa Wilaya zote za Ruvuma kutambua na kuainisha vivuko vyote vilivyopo ndani ya maeneo yao na kisha kufanya sensa ya vyombo vya usafiri vinavyotumika kuvusha abiria na mizigo na kuona umakini wake.
Aliwataka watambue wamiliki na waendeshaji wa boti kwenye mito na Ziwa Nyasa na waweke utaratibu wa abiria wote kujisajili kila watumiapo vyombo vya majini. Aidha, aliwataka wananchi wote kuzingatia sheria na taratibu kila watumiapo vyombo vya moto kuepusha ajali zinazosababisha vifo na ulemavu.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!