Monday, 11 July 2016

Nyayo za miaka 3,700,000 zagunduliwa




SERIKALI imetangaza rasmi ugunduzi mpya wa nyazo za zamadamu eneo la Laetoli lililoko ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ambazo ni za watu wanaodaiwa kuishi miaka milioni 3.7 iliyopita.




Ugunduzi huu ni wa pili mkubwa kufanyika baada ya ule wa Dk. Mary Leaky na wenzake uliofanywa mwaka 1978 katika eneo hilo.
Akitoa taarifa rasmi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alisema ugunduzi huo unaendeleza uthibitisho pekee hadi sasa kwamba zamadamu walianza kusimama na kutembea wima kwa miguu miwili kama binadamu wa sasa miaka milioni 3.7 iliyopita na waliishi eneo la Laetoli.
“Ugunduzi huu unazidi kuipaisha Tanzania katika nyanja za utafiti wa chimbuko la binadamu, hususan, katika kutembea wima kwa miguu miwili badala ya mikono na miguu," alisema Prof. Maghembe.
“Ugunduzi huu unaongeza vivutio vya kitalii hapa nchini pamoja na kukuza sekta hii na faida zinazoambatana na utalii kama kipato cha fedha za kigeni, uendelezaji wa elimu na tafiti mbalimbali, ajira kwa kada zote na kujulikana kwa Tanzania duniani.”
Alisema ugunduzi huo unatokana na kazi ya tathmini ya urithi wa utamaduni uliofanywa na mshauri mwelekezi kampuni ya GMP Consulting Engineers ya Arusha.
Alisema mshauri mwelekezi ana mkataba na NCAA ya kutekeleza kazi za ubunifu wa michoro na usimamizi wa ujenzi wa Makumbusho ya Nyazo za Zamadamu wa Laetoli.
Lengo la makumbusho hiyo ni kuzihifadhi na kuzionyesha nyayo hizo kwa watalii na kwamba makumbusho hiyo inatarajiwa kugharimu si chini ya Sh. Bilioni 12 hadi kukamilika ujenzi wake.
Alisema ili kutekeleza kazi ya kutathmini athari za mradi kwenye urithi wa utamaduni, mshauri mwelekezi aliwatumia watafiti Profesa Fidelis Masao na Dk. Elgidius Ichumbaki wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufanya kazi hiyo.
“Wakati wanatekeleza tathmini hiyo, mwezi Septemba 2014, Josephat Gurtu, Augustine Sungito na Eliya Bura waligundua kilichosadikika kuwa nyayo zingine za zamadamu,” alisema.
Alisema kitaalam ilitakiwa sasa kupata uthibitisho kama nyayo hizo kweli ni zamadamu au la, hivyo kuanzia Julai mosi, mwaka huu, NCAA ilialika wataalamu kutoka sehemu mbalimbali duniani wakiongozwa na watafiti wa nchini kuthibitisha kama kweli nyayo hizo ni za zamadamu na katika muda wa siku 10 wataalam hao waliweza kuthibitisha hilo.
“Wataalam wamethibitisha kuwa nyayo hizi ni za zamadamu na mimi Waziri wa Maliasili na Utalii ninatangaza rasmi kuwepo kwa nyayo hizi mpya hapa Laetoli zenye takribani miaka milioni 3.7,” alisema.
Utafiti huo umefanywa na watafiti na wahifadhi kutoka NCAA, Idara ya Mambo ya Kale, Makumbusho ya Taifa, Chuo
Kikuu Kishiriki cha Udaktari cha Mtakatifu Francisco, Ifakara; Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Colorado, Marekani.

Wengine walitoka Chuo Kikuu cha Wisconsin, Chuo Kikuu cha Rutgers, vyote vya Marekani, Chuo Kikuu cha St. Petersburg, Urusi na Chuo Kikuu cha Manitoba, Canada.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!