LUSAKA, ZAMBIA
BAADA ya kumpiga dansa wake aitwaye Pamela, mwanamuzki Koffi Olomide (pichani)amefutiwa maonyesho aliyotarajia kufanya nchini Zambia.
Taasisi ya Kilimo na Biashara ya Zambia imefuta maonyesho ya mwanamuziki huyo kutoka DR Congo ambayo yalipangwa kuanza kesho Jumatano na kuendelea hadi Jumatatu ijayo.
Rais wa taasisi hiyo, Ben Shoko katika taarifa yake alisema kwamba kitendo alichofanya Koffi si cha kiungwana.
Ijumaa iliyopita akiwa Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta, (JKIA) Nairobi, Koffi alinaswa katika video akimpiga teke dansa huyo kwa kilichodaiwa kwamba dansa huyo alikorofishana na mwanamuziki wa kundi hilo aitwaye, Cindy Le Couer ambaye amekuwa na uhusiano wa kimapenzi na Koffi tangu mwaka 2012.
Pamoja na kamera kumnasa, Koffi alikana kumpiga dansa huyo badala yake alijitetea kwamba alikuwa akimkinga na vibaka.
Tukio hilo mbali na kuamsha hisia za chuki kwa Koffi pia limemfanya ashutumiwe kwao DR Congo kutokana na matukio mbalimbali ya kikorofi ambayo amekuwa akihusishwa nayo.
No comments:
Post a Comment