Kilimo Bora Cha Pilipili Hoho Na Faida Zake
Zao hili hutumika kama kiungo kwenye vyakula mbalimbali kama vile vyama, viazi na ndizi. Vilevile hutumika katika kutengeneza kachumbari na kuweza kukaushwa na kusagwa ili kupata unga.
Viini lishe vinavyopatikana katika pilipili tamu au hoho ni Vitamini A,B,C na madini aina ya chokaa na chuma.
MAZINGIRA:
Zao hili hukua vizuri kwenye hali ya hewa yenye joto la wastani (nyuzi joto 18 hadi 20) za Sentigredi, joto likizidi vichomozo, maua na matunda huanguka.
Huhitaji mwinuko wa kuanzia usawa wa bahari hadi mita 1,500 na mvua za wastani kiasi cha milimita 600 hadi 1500.
Udongo unaofaa kwa zao hili ni ule wenye rutuba, mboji nyingi, kina kirefu na usiotuamisha maji.
AINA:
Kuna aina nyingi za pilipili hoho. Baadhi ya aina zinazostawishwa nchini ni California, Wonder, Emerald Giant, Sweet Neapotitan, Yolo Wonder, Pimiento na Keystone Resistant Giant. Aina zingine ni kama vile Ruby King, Ruby Giant, Libert Bell na Yolo Wonder B.
KUPANDA MBEGU:
Mbegu zinaweza kupandwa moja kwa moja shambani au kuoteshwa kwanza kwenye kitalu na baadaye kuhamishiwa shambani.
Kuotesha mbegu Kitaluni.
Kabla ya kusia mbegu tengeneza tuta lenye upana wa mita moja. Urefu wa tuta utategemea eneo la shamba linalotarajiwa kupandwa. Weka mbolea za asili zilizooza vizuri kiasi cha ndoo mbili au zaidi katika eneo la mita mraba moja. Changanya mbolea na udongo vizuri, kisha tengeneza vifereji vyenye nafasi ya sentimeta 10 hadi 15 kutoka kifereji hadi kingine. Kina cha kifereji kiwe sentimeta moja hadi tatu katika eneo hilo, kiasi hiki kitatoa miche ambayo itatosha kupandikiza katika eneo la mita mraba 100.
Baada ya kusia fukia kwa kutumia udongo laini au mbolea za asili zilizooza vizuri. Weka matandazo na kisha mwagilia maji. Endelea kumwagilia kitalu kila siku asubuhi na jioni hadi mbegu zitakapoota. Mbegu huota baada ya siku sita hadi 10. Mara zitakapoota ondoa matandazo. Endelea kumwagilia maji hadi wakati miche inakuwa tayari kwa kupandikizwa.
KUTAYARISHA SHAMBA
Tayarisha shamba vizuri mwezi mmoja kabla ya kupandikiza miche, katua ardhi katika kina cha kutosha sentimeta 30 kwenda chini, weka mbolea za asili kiasi cha tani 10 hadi 15 kwa hekta. Kiasi hiki ni sawa na debe moja kwa eneo la mita mraba moja changanya mbolea na udongo vizuri.
Ikiwa eneo hilo lina upungufu wa madini aina ya fosiforasi kama itakavyothibitishwa na wataalam, weka mbolea ya chokaa aina ya TSP. Kiasi kinachotakiwa ni kilo 200 kwa hekta. Lainisha udongo siku tatu au tano kabla ya kupandikiza miche.
KUPANDIKIZA MICHE:
Miche huwa tayari kwa kupandikizwa shambani baada ya wiki nne hadi 10. Wakati huu huwa na majani sita hadi manane na urefu wa sentimeta 10 hadi 15.
Pandikiza miche katika nafasi ya sentimeta 40 hadi 50 kutoka shimo hadi shimo na sentimeta 60 hadi 75 kati ya mstari na mstari. Ikiwa mbolea za asili hazikuwekwa wakati wa kutayarisha shamba, weka kiasi cha nusu kilo hadi moja katika kila shimo la kupandia.
Siku moja kabla ya kung’oa miche, mwagilia tuta ili kulainisha udongo. Ng’oa miche pamoja na udongo wake kisha pandikiza katika kina cha sentimita mbili zaidi kuliko ilivyokuwa kwenye kitalu. Pandikiza miche wakati wa asubuhi au jioni. Mara baada ya kupandikiza mwagilia maji ya kutosha.
KUTUNZA SHAMBA
· Kuweka matandazo.
Tandaza nyasi kavu ili kuhifadhi unyevu ardhini, kuongeza rutuba ya udongo, kuzuia uotaji wa magugu, na mmmomonyoko wa ardhi.
· Palizi.
Palilia shamba kila magugu yanapoota. Wakati wa kupalilia pandishia udongo kuzunguka shina ili kuifunika mizizi, na kuzuia mmea usiangushwe na upepo mkali.
· Kumwagilia Maji.
Pilipili hoho hustawi vizuri iwapo zimepata maji ya kutosha. Hivyo umwagiliaji wa mara kwa mara hasa wakati wa kiangazi ni wa muhimu.
· Kuweka Mbolea.
Zao hili huhitaji mbolea za kukuzia. Hizi ni kama mbolea ya S/A, CAN, Urea na mbolea ya mchanganyiko aina ya N.P.K Mbolea ya mchanganyiko (N.P.K) huwekwa wakati maua yanapoanza kutoka. Kiasi kinachowekwa ni gramu tisa hadi 10 (kijiko kimoja kikubwa) kwa kila mmea. Majuma manne baadaye weka CAN, S/A au Urea. Weka gramu sita (kijiko kidogo cha chai) kwa kila mche, kama utatumia CAN au S/A. ikiwa utatumia Urea, weka gramu tatu ( nusu kijiko cha chai) kwa kila mche).
Wadudu waharibifu na Magonjwa.
Wadudu.
· Vidukari au wadudu Mafuta ( Aphids).
Hivi ni vijidudu vidogo vyenye rangi nyeusi, kijani au kahawia. Hushambuliwa majani kwa kufyonza utomvu wake na kusababisha mmea kudumaa.
Vidukari huzuiwa kwa kunyunyizia dawa kama vile Dimothoate au Selecron.
· Mbawakau.
Ni wadudu wenye rangi nyeusi iliyochanganyika na kahawia. Mabawa yao kwa nje ni magumu. Hushambulia shina karibu na usawa wa ardhi na kulifanya liwe na nundu.
Zuia wadudu hawa kwa kutumia mojawapo ya dawa zifuatazo; Carbaryl, au Dimecron.
· Fukusi wa Pilipili (Pepper Weevil)
Mdudu huyu ni hatari sana kwa zao hili na mashambulizi kufanywa na funza wake wenye rangi nyeupe. Funza hawa hula sehemu ya ndani ya vichomozo na matunda machanga nan kusababisha kuanguka. Angamiza wadudu hawa kwa kutumia moja ya dawa zifuatazo; Actellic, Sumithion au Carbaryl.
· Vithiripi (Thrips)
Hivi ni vijidudu vidogo vyenye rangi ya njano. Hushambulia majani na husababisha mmea kuwa na rangi nyeupe yenye kung’aa. Mmea pia kunyauka kuanzia kwenye ncha ya jani. Vijidudu hivi pia kueneza magonjwa yatokanayo na virusi.
Zuia vijidudu hivi kwa kutumia dawa kama vile;- Cyrmethrin, Sumicidin au Dimercon.
· Sota (Cutworms)
Hawa hukata miche michanga karibu na usawa wa ardhi. Ili kuwazuia wadudu hawa, tumia dawa kama vile Carbaryl, Sumicidin au Ekalux. Nyunyizia mara baada ya kupandikiza.
· Inzi Weupe (White flies).
Ni vidudu vidogo vyenye rangi nyeupe, na huonekana kama vumbi la unga vikiwa kwenye majani. Mmea ukitikiswa huruka.
Hushambulia mmea kwa kufyoza utomvu wake, na hueneza ugonjwa wa virusi unaosababisha kujikunja kwa majani.
Inzi weupe wanaweza kuzuiwa kwa kutumia Sumicidin, Sapa Diazinon au Diclorvos.
· Utiriri Mwekundu (Red Spidermites)
Hawa ni wadudu wadogo wenye rangi nyekundu au rangi ya machungwa yaliyoiva. Huonekana upande wa chini wa majani na hushambulia mmea kwa kufyonza utomvu wake.
Zuia utitiri kwa kutumia dawa kama vile Kelthane, Dimethoate na Diazinon.
Magonjwa
· Magonjwa ya Virusi
Magonjwa haya hutokana na virusi. Husababisha majani kudumaa, kukunjamana, na kuwa na rangi ya njano. Ili kuzuia magonjwa haya, zingatia yafuatazo;-
- Panda aina ya pilipili zinazostahimili mashambulizi j ya magonjwa haya.
- Ng’oa miche inayoonyesha dalili za magonjwa haya.
- Zuia wadudu wanaoeneza magonjwa ya virusi kwa kutumia dawa ya Kelthane 30 E,
C, Dimethoate, Diazinon na Ekalux.
- Badilisha mazao. Baada ya kuvuna pilipili tamu, zao linalofuata lisiwe la jamii la zao hili kwa mfano nyanya na bilinganya.
Chule (Anthracnose)
Ugonjwa huu husababishwa na ukungu. Hushambulia matunda na kuyasababisha kuwa na makovu j ya mviringo yenye rangi nyeusi iliyochanganyika na kahawia.
Zuia ugonjwa huu kwa kunyunyizia mojawapo ya dawa zifuatazo: Dithane - M 45, Topsini - M, Ridomol au Kocide,
· Madoa Bakteria (Bacterial Leaf spot)
Ugonjwa huu husababishwa na viini vya vya bacteria. Hushambulia majani machanga j na baadaye matunda. Dalili j zake ni kuonekana kwa madoa ya njano kwenye majani na matunda.
Zuia ugonjwa huu hkwa kupanda mbegu zilizothibitishwa na wataalam.
· Kuoza Mizizi (Root Rot)
Huu ni ugonjwa wa ukungu unaoshambulia mizizi na kusababisha kuoza. Mmea hunyauka na hatimaye hufa. Ugonjwa huu hupendelea sana hali ya unyevunyevu na joto jingi, hivyo zuia hali hii kwa kuepuka kupanda pilipili kwenye sehemu h inayotuamisha maji.
Hali ikiwa mbaya, tumia dawa za ukungu h kama vile Dithane M 45, Tpsin - M 70 au Ridomil.
· Mnyauko Verticilium (Verticilim Wilt)
Huu pia ni ugonjwa unaoletwa na ukungu ambao hupatikana kwenye udongo. Hushambulia shina na kulisababisha libadilike rangi na kuwa ya kahawia. Baadaye mmea hunyauka na kufa. Unaweza kuzuia ugonjwa huu kwa kubadilisha mazao.
KUVUNA
Pilipili hoho huwa tayari kwa kuvunwa baada ya wiki 10 hadi 14 tangu kupandikiza miche. Uvunaji huendelea kwa muda wa wiki nane hadi 10. Muda wa kuvuna hutegemea aina na matumizi. Pilipili kwa ajili ya matumizi ya nyumbani huvunwa zingali na rangi yake ya kijani kibichi inayong’aa . zile za kisindika kiwandani huvunwa zikiwa zimekomaa na zenye rangi nyekundu. Matunda yakivunwa tangali machanga hunyauka kwa urahisi, kusinyaa na hupunguza wingi wa mazao. Wastani wa mavuno huwa kwa hekta ni tani 30 hadi 45.
No comments:
Post a Comment