Jacob Louis 'Kaparata' akiingia kwenye gari lake alilolitengeneza mwenyewe kwa miezi mitatu.
Wananchi wakipigana vikumbo kulishangaa gari la 'Kaparata' katika viwanja vya maonyesho ya Biashara ya Kimataifa (Saba Saba) jijini Dar es Salaam.
Na Daniel Mbega
SIYO Jeep la Mmarekani wala Korando la Mkorea. Hili ni gari aina ya Kaparata ambalo limebuniwa na kutengenezwa na kijana Mtanzania, Jacob Louis ‘Kaparata’ (38), mkazi wa Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam ambaye ametumia vifaa vingi vinavyopatikana hapa hapa nchini.
Waliobahatika kuliona gari hili katika Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa – Saba Saba wamekiri kwamba huu ni ubunifu mkubwa ambao unastahili kuungwa mkono na serikali na mamlaka nyingine.
“Nimetumia vifaa vingi vinavyopatikana hapa nchini. Chassis nimeitengeneza kwa kutumia square pipe, bodi nimelisuka kwa kutumia brake pipes zinazotumika kutengenezea vitanda na nikatumia mabati ya gauge 18 ambayo yanatumika kutengenezea mageti,” anafafanua Kaparata.
Anaongeza: “Nilipomaliza kutengeneza chassis nikaenda kununua injini, diff, gear box na matairi, ambavyo vyote ni vya gari aina ya Suzuki Carry. Unajua Suzuki Carry ni fupi ina futi 10, lakini nilichokifanya ni kuongeza chassis hadi futi 12. Injini ina nguvu sana ila kigari kile kimenyimwa bodi. Sasa gari yangu hii imeonekana kuwa na nguvu, ina kasi.”
Kaparata anasema kwamba, gari yake ina muundo wa kipekee tofauti na gari lolote duniani na ameitengeneza kwa kipindi cha miezi mitatu tu kabla ya maonyesho ya mwaka huu ya Saba Saba ambapo limemgharimu kiasi cha Shs. 12,850,000.
“Nilipokuwa mdogo nilikuwa mtundu sana nikitengeneza magari na vitu mbalimbali kwa kuiga nilivyoviona, ndipo watoto wenzangu wakanipachika jina la ‘Kaparata’, ambalo nimelizowea na kuamua kuiita kampuni yangu kwa jina hilo.
“Tangu mdogo nilipenda kuangalia filamu na nilivutiwa na gari moja nililoliona kwenye filamu ya Delta Force ya Chuck Norris (The Flyer 72 Advanced Light Strike Vehicle) nikaapa kwamba lazima nije nitengeneze gari la aina hiyo,” anasema Kaparata.
Hata hivyo, anasema kwamba, alitumia muda wa wiki mbili kutengeneza chassis ambayo alihakikisha inanyooka na kukaa sawa kabla ya kuendelea na utundu mwingine.
“Hivi sasa nikitembea na gari yangu, hata kama tumeongozana na magari mengine ya kifahari, watu wataitazama gari yangu mitaani na wamevutiwa nayo huku wengine wakinitaka nitengeneze mengine niyauze,” anasema.
Anasema wakati anaanza kuitengeneza gari hiyo vifaa pekee alivyokuwa navyo ni drill machine, grander na welding machine – vifaa vitatu tu, ambapo mabati na vifaa vingine alivinunua.
Kwa kuwa yeye si fundi mchundo, mabati na vifaa vingine aliyapeleka kwa mafundi mchundo ambao walimkunjia kwa muundo na vipimo alivyovitaka yeye.
“Lakini nimeingia hasara kubwa kwa sababu wakati mwingine unampelekea mtu akukunjie bomba au bati, lakini anakosea, inabidi kulitupa na kutafuta jingine.
“Nilipokuwa nayabeba mabati kupeleka kwenye viwanda kwa ajili ya kukunja wengi waliniona kama mwendawazimu, wengine wakanikatisha tamaa na kusema magari wanatengeneza Wazungu miye Mswahili maskini wapi na wapi!” anasema.
Hata hivyo, anamshukuru mkewe Elizabeth William aliyemzalia watoto Beatrice (14), William (10) na Neema (2) ambaye alikuwa akimtia moyo kila wakati aendelee na ubunifu wake.
“Unajua hata kule kwenye viwanda nilikokuwa napeleka hawakuamini, kwa sababu nilipoyabeba mabati wengine walidhani nakwenda kutengeneza ndoo, lakini baada ya mabati hayo kukunjwa kama nilivyotaka, wote walishangaa,” anasema.
Ukilitazama gari hilo kwa mbali unaweza kudhani ni aina mpya ya Jeep ingawa muundo ni tofauti kabisa, na kama utalikaribia utashangaa kuona vikorombwezo vingi.
“Hiki kioo cha mbele ni cha Land Cruiser ila nimekata mashavu ya pembeni. Indicator ni za Bajaj aina ya TVS, shoo ni za vifaa mbalimbali vya magari. Nimeweka vent kama za Ranger za kuingizia hewa kwenye air cleaner na mengine kibao,” anasema.
Kaparata anasema kwamba, ubunifu ni gharama kubwa, lakini mahali alipofikia kwa sasa anajiona kama ni mhandisi aliyebobea ingawa kikwazo ni mtaji pamoja na kutambulika na mamlaka zinazohusika.
“Mheshimiwa Rais Magufuli amesema anataka kuona Tanzania yenye viwanda ambayo ndiyo nia pekee ya kutengeneza aira kwa sisi vijana, sasa mimi nimeamua kuanza bila kupata msaada wa mtu yeyote mpaka nimekamilisha, ninachokihitaji kwa sasa kwanza ni kutambuliwa na serikali kwa ubunifu wangu, halafu niweze kupatiwa mtaji na mazingira bora zaidi ya kufanyia kazi.
“Kama leo nitaamua kutengeneza gari nyingine kama hii, ninaamini ndani ya mwezi mmoja nitakuwa nimeitengeneza na itakuwa bora kuliko hii kwa sababu nimejifunza makossa yote wakati nahangaika na hii hapa,” anaongeza.
Gari la kifahari la Kaparata limeacha gumzo kwa wageni wanaoshiriki na wanaotembelea maonyesho ya biashara ya kimataifa – Saba Saba, hususan Banda la SIDO.
“Kwani linauzwa kiasi gani? Hili linafaa sana kwenda nalo shamba,” alisema mwananchi mmoja. Mwingine akasema: “Hili ni zuri kama gari aina ya Jeep, la kutokea na familia kwenda kupunga upepo.”
Naam. Walikuwa ni wananchi waliotembelea Banda la SIDO alikoliegesha gari hilo kwa maonyesho pamoja na bidhaa zake nyingine, kwa kuwa yeye ni miongoni mwa vijana wanaonufaika na fursa za Shirika hilo la Viwanda Vidogo ambalo linawakusanya wajasiriamali na wabunifu pamoja ili kuonyesha kazi zao.
Yeye anafanyia shughuli zake katika eneo la SIDO Vingunguti na hata gari hilo ndiko lilikotengenezewa.
“Sikubahatika kusoma hata darasa moja kutokana na matatizo ya kifamilia, huu ni utundu wangu ambao nimekuwa nao tangu nikiwa mdogo. Nilianza kutengeneza magari ya kuchezea kwa kutumia mabati, lakini daima ndoto zangu zilikuwa kutengeneza gari langu mwenyewe, nashukuru Mungu ndoto hizo zimetimia,” anasema Jacob ambaye alizaliwa Mpanda mkoani Katavi kabla ya kuhamia Kigoma ambako baba yake Mzee Louis Jacob alikuwa dereva katika Mamlaka ya Pamba.
Akiwa mtoto wa saba kati ya watoto nane, Jacob anasema kwamba ni wawili tu kati yao waliowahi kuingia katika vyumba vya madarasa ambao ni dada yake wa pili kuzaliwa ambaye aliishia darasa la nne na kaka yake wa tatu kuzaliwa aliyemaliza darasa la saba.
Anasema, baada ya wazazi wao kutengana mwaka 1993, mama yao aliamua kuwachukua yeye na ndugu zake na kurudi Mpanda ambako maisha yaliendelea kuwa magumu mno.
“Elimu ya zamani, hasa ya darasa la sababu, haikuweza kumfikisha popote hata yule kaka yangu, kwa hiyo tulijikita katika shughuli za shamba tu,” anaeleza.
Hata hivyo, anasema kwamba licha ya kutoingia darasani, hivi sasa anajua kusoma baada ya kufundishwa kusoma a, e, i, o, u na mpwawe Sarah William mwaka 1993 na yeye akaziunganisha herufi hizo.
Kaparata anasema kwamba, mpaka anakamilisha kutengeneza gari lake hakuchukua hata senti tano ya mtu bali ni fedha zake mwenyewe kutoka katika vyanzo vingine.
Anasema kwamba, wengi walimcheka na kusema kama anazo fedha za kuchezea bora akawape maskini kwa vile asingeweza kufanikiwa kutengeneza gari, lakini kwa kuwa alikuwa na ndoto zake akaamua kuyapuuza maneno yao na kukwangua kila akiba aliyokuwa nayo kutimiza hayo malengo.
“Mimi ninafanyia kazi zangu pale SIDO Vingunguti, zaidi natengeneza mashine za kutotolesha vifaranga ambazo kidogo kidogo ndizo zinazoniingizia fedha, hivyo hata fedha za kutengenezea gari hili zimetokana na kazi hizo,” anasema.
Anaongeza kwamba, licha ya kutokusoma, lakini utundu na ubunifu wake vinamwezesha kuendesha maisha yake na amekuwa tegemeo kubwa kwa ndugu zake wote.
Amewaasa vijana wengine waliosoma na hawana ajira pamoja na wale ambao hawakubahatika kupata elimu kutokukata tamaa, bali wanaweza kutumia vipaji na nguvu walizojaaliwa na Mwenyezi Mungu kufanya maendeleo.
No comments:
Post a Comment