Thursday, 7 July 2016

JPM amwaga burungutu safari ya hija

.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemwaga burungutu la fedha kusaidia Waislamu ambao watakwenda kuhiji Agosti mwaka huu.
“Najua kuna Waislamu watakwenda kuhiji nadhani Agosti, naomba kama inaruhusiwa na mimi nichangie kitu kidogo kadri ya uwezo wangu, nimejipigapiga na mimi nikaona nichangie kitu kidogo, kana inaruhusiwa naomba Mufti uje nikukabidhi,” alisema Magufuli alipokuwa akizungumza katika Baraza la Eid el Fitri jijini Dar es Salaam jana.


Baada ya kutamka maneno hayo, alishika begi dogo kama briefcase akampa msaidizi wake ambaye alilifungua na kuchomoa burunguti la noti na kumkabidhi Mufti, Sheikh Mkuu Zubeiry Ally. Hata hivyo haikufahamika kiasi cha fedha hizo.
Kabla ya kutoa fedha hizo, awali akimkaribisha Rais Magufuli kuhutubia, Mufti Zubeiry aliwataka Waislamu kutumia Bakwata katika safari za hija zitakazogharimu Dola 3,800 kwa mtu mmoja.
Awali Magufuli alikuwa ameahidi kitita cha Sh2 milioni kwa kijana aliyesoma dua katika sherehe hizo pamoja na kiasi kingine kama hicho kwa kundi la Kaswida lililotumbuiza.
Katika hotuba yake, Dk Magufuli alisema Serikali yake ipo katika mchakato wa kurejesha heshima yake ingawa kuna watu wachache watakaoguswa kwa kuisababishia hasara Serikali.
Rais Magufuli aliyekuwa mgeni rasmi katika baraza hilo la Eid el Firti alisema Tanzania ni nchi tajiri lakini baadhi ya watu wamesababisha watu waendelee kuwa masikini.
“Tanzania hii ni tajiri sana, kila kitu kipo. Juzi mpaka wamegundua Helium tani za kutosha. Kila madini yapo hapa. Lakini kwa nini tuko masikini? Kwa nini watu wana shida? Ndiyo maana tumeamua kwa niaba yenu turudishe heshima yetu. tulete mabadiliko ya kweli na katika kufanya hayo wapo watu watakaoguswa, lakini ni wachache sana kuliko wale waliokuwa wanaguswa kwa kuibiwa, ni wachache waliokuwa wanadhulumiwa,” alisema Rais Magufuli.
Alisema kwa miezi saba tangu alipochaguliwa kuingia madarakani Serikali yake imetekeleza mambo kadhaa ikiwa pamoja na kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari, kurudisha nidhamu ya watumishi wa umma, kudhibiti matumizi mabaya ndani ya Serikali, kuongeza mapato na mengineyo.
“Pamoja na hatua hizo ni dhahiri kuwa bado tuna safari ndefu katika kutimiza yale tuliyokusudia na tuliyowaahidi Watanzania. Naomba niwahakikishie kwamba dhamira ya kuwahudumia kwa nguvu zetu zote pamoja na vipaji vyote bado tunayo.
Tuna sababu ya msingi na tuna imani kuwa Mungu yupo kuhakikisha kuwa tunaipeleka nchi yeti mbele...” alisema Rais Magufuli huku akiwataka waumini hao kuiombea Serikali.
Aliwataka viongozi wa dini ya Kiislamu kuwahimiza waumini wao kushiriki katika shughuli za maendeleo hususani katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao utekelezaji wake umeanza mwezi huu.
“Tusipofanya kazi hatutapata pesa. Ndiyo maana wale waliozoea kupata fedha za bure wameanza kusema fedha zimeisha mifukoni. Hela haiji bila kufanya kazi,” alisema.
Kuhusu mali za Waislamu zilizodhulumiwa, Rais Magufuli alisema atawasaidia kuzirejesha. Alimpongeza Mufti wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Zubeiry akisema alikuwa mstari wa mbele katika kurejesha mali hizo kabla hata hajapewa cheo hicho.
“Nakumbuka wakati nikiwa Waziri wa Ardhi, kabla hujawa Mufti, pamoja na viongozi wa Bakwata na wengine, ulifika ofisini kwangu ukieleza jinsi mali za Waislamu zilivyokuwa zinadhulumiwa. Ninafamu pamekuwa na hiyo tabia ya baadhi ya viongozi wenye mali kuwatumia viongozi wa Bakwata na dini nyingine katika kuwarubuni na kuingia ubia, mali hizo baadaye huwa zinapotea kabisa,” alisema na kuongeza:
“Tujitahidi kwa nguvu zote kusimamia mali hizi, zisije kuwa chanzo cha kuvunjika kwa amani. Tunapenda wawekezaji lakini wanachokiahidi hawatekelezi, haiwezekani.
Haiwezekani na wala haikubaliki kwa watu kwa ujanja wao na wakati mwingine kwa kutumia wanasheria wao kukalia mali za Waislamu. Mali za Waislamu lazima zirudi na za Wakristo zirudi ili amani iwepo.”
Baraza hilo lilihudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Katibu wa Bakwata Sheikh Suleiman Lolila na mabalozi wa nchi mbalimbali na waumini wa dini hiyo.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!