Tuesday 14 June 2016

Wenye ualbino wahakikishiwa ulinzi


Dk. Abdallah Possi

Wenye ualbino wahakikishiwa ulinzi

SERIKALI imewapa uhakika wa ulinzi watu wenye Ualbino na kuahidi kushughulikia changamoto zinazowakabili.Akizungumza kwenye maadhimisho ya pili ya kimataifa ya siku yao, jana jijini Dar es Salaam Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Dk. Abdallah Possi, alisema unyanyapaa umebaki changamoto kubwa kwa kundi hilo.
Alisema uelewa mdogo dhidi ya walemavu na watu wenye Ualbino unawaathiri na kwamba jamii inapaswa kuungana ili kulitokomeza.



“Napenda kuuakikisha umma kwamba serikali imejiandaa kuongeza juhudi za kukabiliana na mauaji ya ualbino na kuhakikisha kwamba haki zao zinalindwa na changamoto zao zinashughulikiwa kwa wakati,” alisema.
Aliongeza kuwa nguvu kubwa itaelekezwa katika kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kupenda watu wenye ualbino na kuwaona kama wengine ambao wanaweza kutoa mchango kwenye uchumi wa nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Under The Same Sun, Vicky Ntetema, aliitaka serikali kutengeneza sera na sheria ya Ualbino ili kulinda haki na maslahi yao.
“Tunaamini kuwa itasaidia kurahisisha kazi za polisi, mawakili, waendesha mashtaka na mahakama kuhakikisha haki inatendeka kwa waliofikwa na madhila na ukatili dhidi ya binadamu. Itahakikisha kwamba walioathiriwa na ukatili huo na familia zao na za wale waliouwawa wanapata ushauri wa kisaikolojia na wanalipwa fidia,” alisema.
Naye Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, alisema vita dhidi ya mauaji ya watu wenye ualbino haiwezi kufanikiwa bila kuwashughulikia kikamilifu wanunuzi wa viungo hivyo ambao wanatumia nguvu ya fedha na madaraka waliyo nayo.
Aidha, aliwataka polisi kuwasaka na kuwakamata na kuwafikisha mahakamani wale wanaotengeneza soko la viungo vya watu wenye ualbino ili uuzaji wa miili ya watu hao iwe historia.
“Msikate tamaa Mungu ni mkubwa na wa maajabu na mkumbuke miili yenu ambayo wanaichezea ni kasha tu kikubwa ni roho zenu,” alisema.
“Kwa maoni yangu kuna jambo ambalo halijashughulikiwa kikamilifu ambalo ni wale watu kutokana na nguvu zao kifedha, madaraka yao wao ndio wanunuzi wa viungo na miili ya watu wenye ualbino, nafahamu na ninaipongeza serikali kwamba kuna jitihada kubwa za kushika na kuadhibu wale wanaoua,” aliongeza.
“Wanachukua hatua mbalimbali, lakini mahali ambapo hakujafanyiwa kazi ya kutosha ni kuchunguza na kubaini wale wanaonunua viungo au kutoa fedha ili ndugu zetu wauawe sijasikia mtu anayenunua viungo ameshikwa na kupelekwa mahakamani,” alisema.
“Hatuwezi kushinda vita dhidi ya mauaji bila kushughulikia kikamilifu, kuchunguza kikamilifu, eti wanaonunua viungo ni kina nani? wale wanaolipa fedha ni kina nani? Juhudi hizi zitaonekana pale watu hawa watakaposhughulikiwa kikamilifu,” alisema.
Aliwataka polisi kusaidia kuwasaka wahalifu ambao wakiweka nguvu zao mauaji hayo yatakomeshwa.
Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez, alisema ili kukomesha unyanyapaa dhidi ya ualbino ni lazima Serikali iwekeze kwenye utoaji elimu na kujenga uwelewa kwa wananchi.
Alisema ofisi yake itaendelea kuiunga mkono Serikali ili kuhakikisha watu wenye ualbino hawabaguliwi, hawanyanyapaliwi na wanapata huduma zote za kijamii.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!