Tuesday 14 June 2016

Mongella asema wamebaini vikundi vya kukodi vya mauaji



Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella

Mwanza. Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amefichua kwamba Jeshi la Polisi linafanyia uchunguzi wa kina taarifa za kuwepo vikundi maalumu vinavyokodiwa kufanya uhalifu na mauaji ya watu wakiwamo vikongwe na wenye ulemavu wa ngozi.


Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi hivi karibuni ofisini kwake jijini Mwanza, Mongella alisema amekuwa akipewa taarifa hizo tangu alipoteuliwa kuwa mkuu wa mkoa huo, kwamba katika Kanda ya Ziwa kuna vikundi na watu maalumu wanaofanya mauaji.
“Tangu nilipofika Mwanza nimekuwa nikipewa taarifa kuwa huku usukumani kuna watu wanaotumika kwa uhalifu. Nimeambiwa siyo kila mtu anaua ila kuna watu wanaokodiwa. Hao ndiyo hukodiwa kuua vikongwe, albino,” alisema Mongella.
“Sasa tumeweka mikakati, tunafuatilia taarifa hizo. Na tumetoa maelekezo, tukiambiwa tu tunafika mara moja. Lakini tumesema tukikuta albino au kikongwe ameuawa viongozi wote wa eneo husika tunawakamata,” alieleza.
Mongella ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga alisema ukifutilia matukio ya vikongwe au albino kuuawa utakuta wanachukuliwa katika mazingira tata kutoka kwenye nyumba ambazo hata wengine wamelala humo. “Tumesema sasa basi,” alisisitiza.
Katika ufafanuzi wake Mongella alisema waliovamia maduka ya M-Pesa kilikuwa kikundi cha uhalifu na watuhumiwa walikamatwa wakiwa na silaha aina ya SMG na risasi 144.
Vilevile, alisema tukio la kuuawa watu saba wa familia moja katika kijiji cha Sima Wilaya ya Sengerema linahusiana na ugomvi wa mali. “Ule ulikuwa ugomvi wa kifamilia kuhusu mali. Inawezekana walilenga kuua mtu mmoja, lakini kwa vile wauaji walionekana wakawaua hata ambao hawakulengwa. Wauaji ni kikundi kilichokodiwa kutoka Geita na walikamatwa wote,” alisema.
Mkuu wa mkoa alisema matukio haya yote yanatofautiana kwani uchunguzi wa awali kwa mauaji katika Msikiti wa Rahman unaonyesha kulikuwa na ugomvi katika msikiti huo na wahusika wameshakamatwa.
Katika shambulio hilo lililofanyika Mei 18 usiku, watu wasiojulikana waliuvamia na kuua watu watatu waliokuwa wanaswalisha akiwamo imamu wa msikiti huo, Feruz Ismail. Wengine waliouawa ni waumini wawili; Mbwana Rajab na Khamisi Mponda.
“Halafu likaja tukio la Bulale, Mwenyekiti (Alphonce Mussa) akauawa. Yeye alitoka kwenye mkutano, njiani alikutana na mume na mke wenye ugomvi. Polisi wanafanyia kazi tuhuma za marehemu kuhusika katika ugomvi wa mashamba,” alifafanua.
Alisema japokuwa yamefanyika mauaji ya kutisha ukweli hayana uhusiano na ugaidi kwa kuwa kila tukio lina sababu zake.
Kufuatia tukio la majambazi kuvamia, kupora, kujeruhi na kuua wafanyabiashara wa maduka ya fedha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema tayari wamewatia mbaroni watu watatu wanaodaiwa kuhusika na mtandao huo wakiwa na bunduki aina ya SMG ikiwa na magazine nne na risasi 144.
Pia, alisema watuhumiwa hao walikutwa na kofia moja ya kuficha uso, hijabu mbili, jaketi moja pamoja na mabegi mawili wanayotunzia silaha zilizokuwa zimefichwa kwenye nyumba wanayoishi.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga aliwahi kusema vyombo vya dola tayari vimebaini mitandao saba ya uhalifu mkoani Mwanza.
Kitwanga ambaye pia ni mbunge wa Misungwi aliwaeleza wapigakura wake kuwa tayari mitandao miwili kati ya hiyo saba ilikuwa imeangamizwa, huku jitihada za kuangamiza iliyosalia zikiendelea.

Uchumi
Mongella alisema uhalifu mwingine unafanywa na vijana kutokana na matatizo ya kiuchumi na ili kuhakikisha wanapunguza tatizo hilo, mkoa umeweka mikakati kadhaa inayolenga kuinua kipato cha watu.
Kwanza, kwa kutambua kwamba jiji la Mwanza ni kitovu cha mawasiliano na biashara kwa nchi, wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki alisema wamejipanga kuvutia uwekezaji. “Tayari wawekezaji wameanza kuwekeza katika viwanda; kuna kiwanda cha mifuko (Kisesa), kiwanda cha nyama (Usagara) na kiwanda cha chuma (Nyakato) ambavyo vitaongeza ajira kwa vijana na kuboresha biashara maeneo jirani,” alisema.
Mongella alisema katika azma hiyo hiyo hivi karibuni uongozi ulikaa na wafanyabiashara kujadili maeneo ya uwekezaji na kwamba kuanzia Julai itakuwapo ramani ya mpango mji itakayoonyesha maeneo ya uwekezaji, ya biashara na shughuli nyingine za kijamii.
Katika sekta ya Kilimo alisema wanataka kuunda vikundi vya kilimo cha pamba na mazao mengine ili kuondokana na tatizo la njaa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!