Thursday, 9 June 2016

POLISI YAWAANGUKIA VIONGOZI WA DINI MATUKIO YA UHALIFU


JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha, limetaka ushiriki wa viongozi wa dini na siasa katika kukabiliana na matukio ya uhalifu.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Charles Mkumbo, aliyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wa dini na siasa jijini hapa juzi “Jeshi la Polisi pekee haliwezi kukabiliana na uhalifu bali kwa kushirikiana na viongozi wa dini na wa kisiasa wataweza kuushinda uhalifu,” alisema.
Alisema viongozi wa dini na siasa ni wadau wakubwa wa kuimarisha amani kutokana na ushawishi walionao kwa waumini wao na wananchi wanawaongoza.
Alisema jeshi lake litakuwa bega kwa bega kupokea taarifa za uhalifu na kuzifanyia kazi haraka.
Alisema bila amani hakutakuwa na shughuli zozote za maendeleo ikiwamo uwezekaji na hata waumini hawataweza kwenda misikitini na makanisani kutokana na hofu ya kiusalama.
“Sote tunajukumu la kufichua uhalifu na wahalifu kupitia taarifa za waumini wetu hasa kwa viongozi wetu wa dini kuendelea kuhubiri na kutoa mawaidha katika makanisa na misikiti huku madiwani waendelee kufanya hivyo katika maeneo yao ya kiutawala,” alisema.
Sheikh wa Wilaya ya Arusha, Abraham Salum, alisema kikao hicho kimekuja wakati muafaka kwani Mikoa ya Tanga na Mwanza kumejitokeza vitendo vya uvunjifu wa amani matukio ambayo hapo awali hayakuwapo nchini.
Alitaka jeshi hilo kuongeza weledi katika kupambana na uhalifu huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo.
Akichangia mjadala huo, Padre Festus Mangwangi wa Parokia ya Mtakatifu Theresia, alisema viongozi wa dini wana dhamana kubwa ya kulisaidia jeshi hilo kuhubiri amani kupitia waumini wao.
Alisema amani iliyopo idumishwe kwani baadhi ya nchi zinavurugu na zinatamani amani iliyopo hapa nchini.
NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!