Thursday 16 June 2016

Kwa hili la Taasisi ya Moyo, Kikwete anastahili pongezi!

NI dhahiri kwamba, maradhi ya moyo ambayo ni tishio duniani, yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku.


Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa kati ya mwaka 1990 hadi 2013 kumekuwa na ongezeko la vifo vinavyotokana na maradhi ya moyo kwa asilimia 41, kutoka watu milioni 12.3 hadi milioni 17.3 ambao hufariki kwa maradhi hayo. Kwa Tanzania, inaelezwa wagonjwa wa maradhi ya moyo wamekuwa wanaongezeka kwa asilimia 26 kwa mwaka.
Nimeanza kwa maelezo hayo nikilenga kumuunga mkono Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete kwa kupigania afya za Watanzania kwa kuomba fedha kutoka Serikali ya China mwaka 2007, ili kuweza kujenga Taasisi ya Upasuaji Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ambayo tayari imeshaanza kufanya kazi.
Kikwete, baada ya kuona Watanzania wengi wanasumbuliwa na tatizo la moyo, ambalo liliwapasa kwenda kutibiwa nje ya nchi, alithubutu kuomba msaada huo ili kuokoa maisha ya wananchi wake. Ni ukweli usiopingika kuwa maradhi ya moyo yameanza kuwa tatizo kubwa hapa nchini, hivyo hakuna budi kuchukua hatua thabiti ili kukabiliana nayo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mwaka 2014 watoto wapatao milioni 1.7 walizaliwa, kati ya hao asilimia 0.8 waliokuwa na tatizo la moyo ni sawa na watoto 13,600. Wengine walizaliwa na tundu kwenye moyo, mishipa ya moyo kukaa vibaya pamoja na valvu kubana.
Kutokana na hali hiyo kuwepo, ndipo Rais Kikwete alilazimika kuomba kusaidia kujengewa kituo hicho alipokuwa katika ziara yake ya kikazi nchini China mwaka 2007. Katika ziara hiyo, Kikwete alizungumza na Rais Hu Jintao aliyeridhia kutoa Sh bilioni 16.6 kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo, na Serikali ya Tanzania kutoa Sh milioni 10 kwa ajili ya kununua vifaa vingi muhimu.
Lengo kuu lilikuwa ni kupunguza kupeleka wagonjwa nchini India kwa matibabu. Hivi sasa Watanzania tunajivunia kutibiwa magonjwa ya moyo hapa hapa nchini.
Kwa mafanikio haya, tuna kila sababu ya kumshukuru Rais mstaafu Kikwete kwa jitihada na upendo wa dhati kwa wananchi wa Tanzania. Taasisi hii imeleta faraja kubwa kwa Watanzania kwa sababu siku za nyuma wagonjwa 440 walipelekwa India, kati ya hao, 220 walikuwa ni wagonjwa wa moyo.
Kwa idadi hiyo kupelekwa India, ni dhahiri kuwa wagonjwa wengi walibaki nchini wakitaabika na kuteseka kwa maumivu ikiwemo kutoweza kupumua vizuri, kuhema haraka haraka, miguu kuvimba na wengi kupoteza maisha yao mapema kutokana na kuchelewa kupata huduma stahiki.
Lakini uwepo wa taasisi ya JKCI, unatoa fursa kwa Watanzania wote kutibiwa katika taasisi hiyo ya moyo hapa nchini. Binafsi, nimeguswa na ninathubutu kusema `Asante Jakaya Kikwete’ kwa uthubutu na utu dhidi ya Watanzania wenzako kwani kwa kujua mazingira magumu yanayowakabili wagonjwa wa moyo, ulipigana kiume na kuhakikisha unawaachia zawadi ya taasisi ya moyo kabla ya kungatuka madarakani mwishoni mwa mwaka jana.
Hongera Kikwete kwa kuokoa maisha ya Watanzania hapa nchini, kwani kama sio kuona mbali kuhusu ugonjwa wa moyo, Watanzania wangeendelea kuteseka hata kupoteza maisha. Ninawasihi Watanzania wenzangu, kila mmoja amuunge mkono Kikwete katika kuokoa maisha ya raia wa taifa hili, angalau kwa kushiriki katika hatua yoyote muhimu ya kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji mbalimbali.
Aidha, tuiunge mkono taasisi ya JKCI, uongozi wake na watumishi wote ili izidi kushamiri na hivyo kutimiza ndoto za Rais mstaafu Kikwete na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha tiba ya moyo inapatikana kwa uhakika nchini.

IMEANDIKWA NA LUCY NGOWI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!