Tuesday, 3 May 2016

SHEHENA BANDARI YA DAR KUONGEZEKA HADI TANI 38


KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Alois Matei, amesema ifikapo 2030 kiasi cha mizigo inayoingia bandarini hapo kitaongezeka hadi kufikia tani milioni 38 kutoka tani milioni 16 za mwaka wa fedha 2014/15.





Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kiasi cha shehena ya mizigo inayopita katika Bandari ya Dar es Saaam katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia tisa kila mwaka, huku shehena ya mafuta na makontena ikiongezeka kwa kasi zaidi.
“Bandari inakabiliwa na tatizo la uchakavu wa miundombinu na kina kifupi cha maji cha mita tisa na ufinyu wa lango la kuingilia meli lenye upana wa mita 140 ambalo linaruhusu meli za urefu usiozidi mita 243 kuingia, huku meli kubwa zinazozidi hapo zikishindwa kuingia,” alisema Matei.
Alisema ili kuwezesha meli kubwa kuingia na kuhudumia ongezeko kubwa la mizigo linalotarajiwa kwa miaka 14 ijayo, kunahitajika kufanyika maboresho makubwa ya miundombinu na mifumo ya utendaji kazi.
“Kina cha maji si kikubwa kuweza kuruhusu meli kubwa kutia nanga na kwa sasa meli zinazoingia ni ambazo zinahitaji kina cha mita kuanzia 14 wakati kwa sasa bandari ina kina cha mita tisa.
Alisema maboresho hayo yatakayogharimu dola za Marekani milioni 690, yatafanyika kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Mradi huu umefadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mfuko wa International Bank for Reconstruction and Development (IBRD) ambao watatoa mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 600 na Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DFID) watakaotoa ruzuku ya kiasi cha dola za Marekani milioni 30, huku serikali kupitia Mamlaka ya Bandari ikitarajiwa kuchangia dola milioni 60,” alisema.

Kwa upande wake, Mhandisi Mkuu wa Mitambo na Umeme, Mary Mhayaya, akizungumzia ‘flow meter’ mpya ya Kigamboni, alisema Novemba, 2014 serikali kupitia mamlaka ya usimamizi wa bandari nchini iliingia mkataba na kampuni ya M/S Woodgate Trademark co. Ltd kwa ajili ya kuleta na kujenga ‘flow meter’ mpya.
“Mita hiyo aina ya Brodie (Single product flow control Metering system) imefungwa katika eneo la Kigamboni hivyo sasa mafuta aina ya dizeli yanayoshushiwa kwenye boya la SPM yatapita kwenye ‘flow meter’ mpya kabla ya kusukumwa kwenda kwenye hifadhi ya matenki mbalimbali ya waagizaji wa mafuta,”alisema Mhayaya.
Alisema mradi huo ambao umegharimu dola za Marekani milioni 6.5 ulikamilika Aprili 21, mwaka huu na baada ya kufanya uhakiki kwa kushirikiana na wadau wa mafuta, mita hizo zilizopo zinaweza kuanza kutumika rasmi kibali cha WMA kitakapotolewa wakati wowote.
“Wataalamu wa kutoa huduma kwenye mita hizo wamekwishapata mafunzo ya jinsi ya kuzitumia kwa ufanisi zaidi,” aliongeza

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!