SERIKALI imesema hali na mwelekeo wa Tanzania ni mbaya kutokana na kukithiri kwa uharibifu mkubwa wa mazingira, ambao kwa sasa takribani asilimia 61 ya nchi hiyo iko hatarini kuwa jangwa.
Kutokana na hali hiyo, serikali hiyo imetangaza vita dhidi ya uharibifu huo wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kuainisha mikakati yenye lengo la kutengeneza Tanzania ya kijani.
Tayari imetangaza kampeni ya kitaifa ya upandaji miti nchi nzima, ikiwa ni pamoja na kuanza mchakato wa kutengeneza sheria ndogo kwa ajili ya kudhibiti uharibifu huo, lakini pia kusimamia kisheria utaratibu wa upandaji miti kuanzia ngazi ya vijiji, kata, kitongoji, tarafa, wilaya na mkoa.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/17, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, January Makamba, alisema kila mwaka nchi hiyo inapoteza hekta 372,000 sawa na ekari milioni moja za misitu.
“Matokeo yake katika miaka 10 iliyopita nchi yetu imepoteza eneo la misitu linalolingana na ukubwa wa nchi ya Rwanda. Kasi ya upoteaji wa misitu inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka,” alisema January.
Alisema hali hiyo inatokana na matumizi makubwa ya bidhaa za misitu, akieleza kuwa asilimia 90 ya nishati inayotumika nchini inatokana na misitu na kwa Jiji la Dar es Salaam pekee hutumia magunia 200,000 hadi 300,000 ya mkaa yenye wastani wa kilo 50 kwa mwezi.
Alisema kutokana na matumizi hayo yanayochangia uharibifu wa mazingira kwa sasa vyanzo vingi vya maji vimeharibika, mvua zimekuwa hazitabiriki, mafuriko na ukame umeongezeka kwenye maeneo mengi na rutuba ya ardhi imepungua.
Alisema katika kukabiliana na uharibifu huo wa mazingira wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha imeandaa mkakati wa kitaifa wa miaka mitano wa upandaji na utunzaji miti utakaogharimu kiasi cha Sh bilioni 105.2.
Alisema lengo la mkakati huo ni kuimarisha na kuboresha kampeni ya upandaji miti nchini na kwa mwaka wa fedha ujao, serikali imejipanga kuhakikisha kila kijiji, kitongoji, mtaa, kaya na kila taasisi inapewa lengo la upandaji miti.
Pamoja na serikali kuendelea kusimamia Sera, miongozo na mikataba ya mazingira iliyopo, imebainisha kuwa ili kutimiza majukumu yake Mfuko wa Mazingira kwa mwaka ujao wa fedha utahitaji Sh bilioni 100.
Alisema fedha hizo zitatumika kufanya ufuatiliaji, utafiti, tathmini na uchambuzi wa hali ya uharibifu wa mazingira, kugharamia mkakati wa serikali wa upandaji miti, kugharamia miradi ya uhifadhi wa mazingira na kusaidia jamii zilizoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, January alisema katika jitihada za kukabiliana na uharibifu wa mazingira Serikali inaendelea kutekeleza mikataba mbalimbali ya mazingira ikiwemo mkataba wa kupambana na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame.
Mkataba mwingine ni wa Stockholm wa kudhibiti kemikali zinazodumu katika mazingira kwa muda mrefu na Mkataba wa Montreal unaohusu kemikali zinazomong’onyoa tabaka la hewa ya ozone.
Aidha, alitaja mkataba mwingine utakaoendelea kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha kuwa ni Minamata unaohusu udhibiti wa matumizi ya zebaki. Katika makadirio hayo, January aliomba Bunge liidhinishe makadirio ya bajeti na matumizi ya Sh bilioni 20.3.
Kiasi hicho kinajumuisha Sh bilioni 9.4 za fedha za matumizi ya kawaida na Sh bilioni 10.9 za miradi ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Dk Dalaly Kafumu, aliitaka serikali ihakikishe kuwa suala la mazingira linapewa kipaumbele kwa kutengewa bajeti ya kutosha.
Alisema kutokana na hali halisi ilivyo ni vyema serikali ikaendelea na utaratibu wa kuwaondoa wakazi waliojenga mabondeni ili kuepusha maafa. Naye Msemaji wa Kambi ya Upinzani bungeni kuhusu mazingira, Pauline Gekul aliitaka serikali kutoa kipaumbele zaidi katika suala la mazingira kwa kuwa mazingira bora ndio uhai wa sasa na vizazi vijavyo.
No comments:
Post a Comment