Askari wa Bunge wakiwatoa wakiwatoa ndani ya ukumbi Wabunge wa Upinzani mjini Dodoma jana, baada ya kutokea mabishano kati yao na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

  • Wabunge wa Upinzani watolewa kwa kushupalia mjadala wa Udom, saba wapewa adhabu, wamshutumu Naibu Spika kwa kuzima hoja yao, wajipanga kumg'oa..
SAKATA la kuondolewa kwa wanafunzi 7,802 katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), limechukua sura mpya baada ya jana Bunge kuparaganyika na kulazimika kusitisha shughuli zake kwa muda huku Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari (Chadema), akitolewa 'mjengoni' kwa nguvu na askari wa Bunge.

Mbunge huyo alitolewa nje ya ukumbi wa Bunge akidaiwa kuwaongoza wabunge wenzake wa Kambi ya Upinzani kukaidi amri ya Naibu Spika, akitaka suala hilo lijadiliwe bungeni.
Baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu bungeni, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako, alitoa taarifa ya kurudishwa nyumbani kwa wanafunzi 7,802 waliokuwa wanachukua stashahada ya mafunzo ya ualimu wa sayansi Udom.
Prof. Ndalichako alisema uamuzi huo umetokana na mgomo wa walimu uliodumu kwa mwezi mmoja.
Alisema walimu hao waligoma kuwafundisha wanafunzi na jitihada za serikali kutatua mgomo huo zimefanyika bila mafanikio.
Alisema walimu wamegoma kuwafundisha wanafunzi hao wakipinga madai ya Mkaguzi wa Hesabu wa Ndani wa Udom kuwa madai yao ya kimaslahi hayako sahihi.
“Serikali haiwezi kumwingilia Mkaguzi wa Ndani na kwa sababu walimu wameonyesha kutokuwa tayari kufundisha, na wanafunzi wamekaa bila kusoma, serikali imeona ni busara wanafunzi waende nyumbani hadi ufumbuzi wa suala hilo utakapopatikana," alisema.
Aliongeza kuwa serikali itaangalia namna wanafunzi hao watakavyopata mafunzo katika mfumo utakaokuwa na tija kwao na taifa kwa ujumla.
MWONGOZO WA NKAMIA
Baada ya maelezo hayo, Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia, alisimama na kuomba mwongozo wa Spika akitaka sakata hilo kujadiliwa bungeni na kutafutiwa ufumbuzi kwa kuwa wanafunzi waliotakiwa kurejea nyumbani hawana makosa.

Nkamia ambaye alikuwa Naibu Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo katika serikali iliyopita, alisema: "Watoto hawa hawana makosa, wengi wa wanafunzi hawa wanatoka karibu nchi nzima, waliogoma ni walimu, lakini walioadhibiwa ni wanafunzi.
Nilikuwa naomba mwongozo wako. Hivi serikali ilikuwa haijaona umuhimu wa kumaliza tatizo na walimu ambao walikuwa ni wachache kwa muda mfupi badala ya kuwaadhibu wanafunzi 7,802?"
Aliongeza: "Jana (juzi), wanafunzi hao walionekana wakizurura Dodoma, wengi wao wakiwa ni vijana wenye umri wa miaka 16, wasichana na wavulana na haikujulikana walilala wapi.
"Serikali hamkuona haja kumaliza tatizo hilo? Kama Mkaguzi wa Ndani anasema hesabu hajakubaliana nazo, leo unawarudisha wanafunzi, hawana pesa ya kula wala mahali pa kulala. Naomba kutoa hoja ikiwezekana Bunge lijadili hoja hii."
KAULI YA NAIBU SPIKA
Akijibu hoja hiyo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alisema Bunge haliwezi kuuliza maswali ya vitu ambavyo havijawasilishwa bungeni.

"Kwa kuwa suala hilo lilitolewa maelezo na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, maana yake serikali inayo taarifa ya jambo hilo na linafuatiliwa," alisema.
Alisema Bunge haliwezi kuuliza maswali kuhusu taarifa ya vitu ambavyo havijawasilishwa bungeni ikiwamo taarifa ya Mkaguzi wa Ndani wa Udom.
“Mwongozo wangu ni kwamba, serikali imeshatoa taarifa juu ya suala hilo. Na kama kuna majibu ambayo hayajaeleweka katika maelezo ya waziri, hilo ndilo linaweza kuuliziwa maswali, lakini mwongozo wangu ni kuwa tunaendelea baada ya waziri kutoa maelezo,” alisema.
ASKARI WAINGIA BUNGENI
Baada ya kutoa majibu hayo, ndipo ulipozuka mjadala mzito miongoni mwa wabunge hao ambao walimtuhumu Naibu Spika kujigeuza wakala wa serikali, huku baadhi wakisikika wakisema: "Acha ubabe, acha uwakala wa serikali."

Huku vijembe hivyo vikiendelea dhidi ya kiongozi huyo wa Bunge, baadhi ya wabunge wa pande zote mbili (CCM na Upinzani) walisimama na kuomba utaratibu.
Hata hivyo, Naibu Spika alisema: "Kanuni zinazohusu utaratibu ni pindi mtu anapokuwa amesimama na anaongea jambo ambalo linavunja kanuni, ndipo mbunge ataruhusiwa kuuliza utaratibu."
Dk. Tulia ambaye kabla ya kuwa Naibu Spika wa Bunge alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, alisema hakuna mbunge yeyote aliyezungumza wala kusimama kinyume cha kanuni, hivyo kuomba utaratibu haikuwa sawa kwa kipindi hicho.
Baada ya maelezo hayo, Mbunge wa Arumeru Mashariki (Nassari), alisimama na kuomba mwongozo akizingatia Kanuni ya 69 ya Kanuni za Kudumu za Bunge toleo la Januari 2016 akitaka mjadala unaondelea wa makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji usimame na Bunge lijadili suala la wanafunzi kuondolewa Udom.
"Wanafunzi 7,802 wanafukuzwa, makosa siyo ya kwao, chuo kimeshindwa kuwalipa wahadhiri, unawafukuza wanafunzi wa kike zaidi ya 4,000 usiku watakwenda wapi? Wengine hawana fedha, wanabakwa, sehemu ya wao kukimbilia ni bungeni ili tuwasemee, Bunge lisimamishe mjadala na tujadili suala la dharura," alisema nakuongeza:
"Hoja iko pale pale, Bunge lifungwe tuondoke bungeni, hakuna haja ya kuendelea kujadili bungeni wakati wanafunzi wanateseka."
Baada Nassari kuomba mwongozo huo, wabunge wa upinzani pamoja na baadhi ya wa CCM, walisimama na kupiga kelele wakitaka Bunge lijadili suala hilo, ndipo Naibu Spika akaamuru wabunge wote waliosimama watoke ndani ya ukumbi wa Bunge.
“Waheshmiwa wabunge naomba mkae, wabunge mliosimama naomba mtoke nje, Askari (wa Bunge), naomba muwatoe wabunge waliosimama, wabunge naomba tusikilizane, naahirisha Bunge hadi saa 10 jioni na naomba Kamati ya Uongozi ikutane sasa hivi,” alisema Dk. Tulia.
SAUTI ZA WABUNGE
Wabunge wa vyama mbalimbali waliozungumza na Nipashe nje ya ukumbi ya Bunge baada ya kusitishwa kwa muda kwa shughuli za Bunge jana asubuhi, walipinga kitendo cha Naibu Spika kuzuia hoja hiyo kujadiliwa bungeni.

JOSEPH SELASINI - CHADEMA
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alisema: "Watoto hawana pesa, watoto hawana sehemu ya kulala, no no, no! kama hii ndiyo siasa, basi Naibu Spika, Bunge limemshinda, halafu yeye ni mwanamke anashindwa kuwatetea watoto wa kike."

JOYCE SOKOMBI - CHADEMA
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Joyce Sokombi (Chadema), alisema: "Bunge lisipojadili suala hili, lifungwe tu. Serikali itoe jibu la uhakika kwa sababu ni makosa ya walimu, lakini wanakuja kuwaadhibu wanafunzi."

HAWA MWAIFUNGA - CHADEMA
Huku akibubujikwa na machozi, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), alisema: "Hadi saa tano usiku jana (juzi) watoto wa kike walikuwa wanazurura stendi, halafu Naibu Spika kama mama anashindwa kuwatetea watoto wa kike, ni aibu kubwa."

JOHN HECHE - CHADEMA
Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche, alisema amesikitishwa na Naibu Spika kuzuia hoja kujadiliwa bungeni kutokana na makosa ya serikali kutowalipa wahadhiri.

"Tatizo ambalo ninaliona mimi ni kwamba, Naibu Spika anachokifanya ni kuilinda serikali kwa sababu ameletwa na serikali. Kila kitu kinachokuja dhidi ya serikali, yeye anajaribu kuilinda. Anashindwa kutambua kwamba kazi ya Bunge ni kuisimamia na kuiwajibisha serikali.
Litakuwa Bunge la ajabu kama litaendelea na shughuli zake wakati watu waliowachagua wabunge kuja kufanya kazi wako mtaani wamefukuzwa. Tatizo kubwa tunashughulikia matawi badala ya mizizi."
Alisema: "Tatizo kubwa ni Bunge lenyewe kukubali kuchaguliwa Naibu Spika na serikali. Naibu Spika aliyechaguliwa na serikali hawezi hata dakika moja kufanya kazi za Bunge kwa maana ya kuisimamia serikali iliyomteua."
RITTA KABATI - CCM
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ritta Kabati, alisema: "Hili tatizo linatuhusu wabunge wote. Kosa ni la walimu si la wanafunzi. Wale walimu sidhani hata 100 wanafika, wamegoma, basi ilitakiwa kutafuta walimu wengine wa kuwafundisha badala ya kukimbilia kuwafukuza wanafunzi.

Aliongeza: "Serikali haijawatendea haki hawa watoto. Leo usiku nimelala na watoto watano wa kike. Wa kiume niliwasaidia kuwanunulia chakula tu maana siwezi kulala na watoto wa kiume."
JAMES MBATIA - NCCR MAGEUZI
Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia, alisema: "Kwa kifupi, utawala kwa maana ya Kiti cha Spika kiliyumba, namna bora ya kulisimamia suala hili kwa kuona kwamba ni jambo jepesi ilhali watoto wa Watanzania wako mitaani na wawakilishi wao wanataka ufumbuzi, lakini Kiti cha Spika kikatetereka ndiyo chanzo cha tatizo hili.

"Na mahali popote penye tatizo wote mnakuwa ni timu moja. Na bahati nzuri leo (jana) bungeni tumekuwa wamoja kwa pamoja wale wa chama tawala na upande wa upinzani. Ni suala ambalo linatakiwa kuisimamia serikali.
"Sasa bahati mbaya sana, utawala wa Bunge unaiogopa serikali. Badala ya kuuchukua huu mhimili ambao ni muhimu wa kusimamia serikali, muhimili huu unaiogopa serikali. Tatizo likishatokea, mnaacha toafuti zote, hii ni taaluma."
STANSLAUS MABULA- CCM
Mbunge wa Nyamagana (CCM), Stanslaus Mabula, alisema: "Kitendo kilichotokea si cha kuuangwa mkono na mzalendo yeyote ndani ya nchi hii.

Aliongeza: "Hawa ni watoto na wengi wao ni chini ya umri wa miaka 16, kitendo cha kuwapa saa 24 kutoka kwenye eneo lao la shule hakikuwa haki hata kidogo.
"Lakini pia kitendo kilichotokea bungeni leo hakiwezi kuwa sahihi kwa sababu taarifa hizi tulitegemea sana busara ya Spika ili iweze kufanya kazi tupate muda wa kujadili na tuone namna ya kuwasaidia hawa watoto."
FLATEI MASSAY - CCM
Mbunge wa Mbulu Vijijini (CCM), Flatei Massay, alisema: "Mimi mwenyewe nimekwenda usiku pale stendi ya mabasi nikakuta wanafunzi wa kike na wa kiume hawana nauli wala pesa za kujikimu, nikawasaidia. Nilitegemea leo tupate majibu mazuri ya serikali."

"Sisi wabunge lazima tusimame kwa pamoja kuwasaidia hawa vijana ili baadaye wasigeuke kuwa katika hali isiyokuwa nzuri. Wanaweza kuwa machangudoa na kufanya mambo mengi mabaya ili wapate fedha za kurejea nyumbani kwao," aliongeza.
LUCIA MLOWE - CHADEMA
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucia Mlowe alisema: "Mimi ni mwanamke, nimeumia sana. Naibu Spika ni mwanamke, hoja iko wazi jinsi hawa watoto wanavyoteseka kwa kosa la serikali.

Mbaya zaidi hawa watoto wanatolewa na maaskari kama vile ni wezi. Kama mbunge mwanamke nimeumia sana."
KANGI LUGOLA - CCM
Mbunge wa Mwibara (CCM), alisema: "Kitendo kilichotokea kule ndani kimenisikitisha sana, kimenisononesha sana na kimenivuruga sana. Wanafunzi zaidi ya 7,000 ambao walikuwa wanasoma kozi ya ualimu wa sayansi."

Aliongeza: "Kinachosikitisha zaidi, watoto hawa kuanzia jana wamefanywa kama wakimbizi ndani ya nchi yao na hata wakimbizi huondolewa kwa utaratibu. Maamuzi yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Spika mimi sikubaliani nayo.
Ni maamuzi ambayo yanazidi kuwavuruga watoto, yanazidi kuwaharibu na wengine hatujui usalama wao leo wamelala vipi."
UONGOZI UDOM
Nipashe ilifanikiwa kuona waraka wa maadhimio ya kikao walichokutana wajumbe wa chama cha wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Udom, kilichojadili suala hilo kabla ya mgogoro huo kuwa mkubwa.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mgogoro huo ulisababishwa na DVC-ARC na DVC-PFA, baada ya kukataa kununua vifaa vya maabara kwa ajili ya kufundishia waalimu hao wa sayansi na pia, kuusaidia uongozi wa CNMS na CoEd kupata waalimu kwa idadi inayokidhi mahitaji.
Waraka huo pia, unaeleza kuwa kulihitajika ushirikiano wa hali na mali wa serikali kuhakikisha kazi inafanyika katika ubora unaowezekana na kukubalika, kuwalipa walimu kila inapotakiwa kufanya hivyo pamoja na kusema ukweli kwa Waziri, Katibu Mkuu na Watanzania kuhusu hali halisi ya uendeshaji wa mafunzo hayo.
UKAWA WASUSIA BUNGE
Katika hatua nyingine, wabunge wa upinzani kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba na Wananchi (Ukawa), walitoka nje ya ukumbi wa Bunge kupinga kuapishwa kwa wabunge kutoka Zanzibar jana asubuhi.

Kususia kwa kiapo hicho ni muendelezo wa msimamo wa wabunge wa upinzani kutotamtambua uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu visiwani humo.
Akizungumza na Nipashe nje ya ukumbi wa Bunge, Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea, alisema Ukawa ulishaweka wazi kuwa uchaguzi wa marudio uliofanyika Zanzibar ni haramu, hivyo hawawezi kuwatambua wajumbe hao.
Wabunge walioapishwa kwa mujibu wa Katiba ni Amina Iddi Mabrouk, Hussein Ibrahim Makungu, Jaku Hashim Ayoub, Machano Othuman Said na Wanu Hafidhi Ameir.
MNYIKA, UPINZANI WATOLEWA NA ASKARI BUNGENI
Waliporejea bungeni saa 10:00 jioni, Naibu Spika alisema: "Waheshimiwa wabunge, tulipositisha shughuli za Bunge asubuhi, niliagiza Kamati ya Uongozi ikakae ili tuweze kushaurina namna ya kumaliza tukio lililotokea leo asubuhi, lakini naona waziri tuliyemwagiza alete hiyo taarifa sasa hayupo humu bungeni."

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema yupo kwa niaba ya serikali, lakini alipopewa fursa ya kutoa taarifa hiyo akasema: "Nilishaambiwa kwamba taarifa kamili kwa sasa haipo."
Baada ya maelezo hayo mafupi ya Lukuvi, Naibu Spika aliwaomba wabunge kuendelea na mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji wakati wakimsubiri Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Ndalichako.
"Waheshimiwa wabunge, kwa wakati huu tunaendelea na shughuli iliyopo mbele yetu, Waziri atakapokuja atatupa taarifa," alisema Dk. Tulia.
Wakati kiongozi huyo wa Bunge akiruhusu mjadala huo uendelee, baadhi ya wabunge wa upinzani wakiongozwa na Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya, walisimama na kuomba mwongozo wa Spika.
Naibu Spika alikataa kuruhusu miongozo yao jambo ambalo liliibua minong'ono huku baadhi ya wabunge wakisikika wakihoji: "Tunaendelea na mjadala wa bajeti kwa kanuni ipi wakati hoja haijajibiwa?"
Wakati minong'ono hiyo ikiendelea, Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika na Heche (Tarime Vijijini-Chadema), walisimama na hawakuwa tayari kuketi walipotakiwa kufanya hivyo na Naibu Spika.
"Mheshimiwa Mnyika na Mheshimiwa Heche, naomba mkae. Mheshimiwa Mnyika naomba ukae, Mheshimiwa Mnyika naomba utoke nje, tafadhali Mheshimiwa Mnyika, nakusihi, naomba utoke nje. Mheshimiwa Mnyika naomba tusibishane. Askari naomba mtoeni Mheshimiwa Mnyika nje," alisema Dk. Tulia.
Baada ya uamuzi huo, Heche aliketi, lakini kukawa na minong'ono mingi bungeni huku wabunge wa upinzani wakisimama na kuomba mwongozo wa Spika.
Minong'ono hiyo iliyokwenda sambamba na kitendo cha wabunge wa upinzani kugonga meza na kusababisha utulivu kukosekana bungeni, ilimfanya Naibu Spika aite askari wa Bunge na kuwaamuru kuwatoa wabunge wote wa upinzani ndani ya ukumbi.
UPINZANI WAMSUSIA RASMI NAIBU SPIKA
Wabunge wa Upinzani Bungeni wamekubalina kutoigia katika vikao vyovyote vya Bunge vitakavyoongozwa na Naibu Spika, kwa kile walichokieleza kwamba amekuwa ni chanzo cha vurugu bungeni.

Pia, wamesema watajadili ajenda ya kutokuwa na imani na Naibu Spika huyo.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliyasema hayo muda mfupi baada ya Naibu Spika kuwatoa nje wabunge wa upinzani kufuatia kugomea kusikiliza hitimisho la mjadala makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji iliyokuwa inahitimishwa na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge.
“Ni pendekezo langu kwa wabunge wa upinzani kuwa tatizo kubwa la Bunge la 11, la msingi kabisa ni Naibu Spika, na kwa sababu tumeona mara kwa mara Bunge hili likivurugika, mienendo ya bunge inavurugika, maamuzi ya Bunge yanapuuzwa kwa sababu tu ya ujio wa Naibu Spika anayeitwa Tulia Ackson... mimi pendekezo langu kwa wabunge, leo la kwanza ni tujadili ajenda ya kutokuwa na imani ya Naibu Spika, sambamba na hilo nitapendekeza siku yoyote Naibu Spika atakapokuwa katika kiti sisi tutoke nje,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema Kamati ya Uongozi ilipokaa asubuhi baada ya vurugu, ilishauri kuwa Bunge litakaporudi jioni, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia atoe maelezo kuhusu suala la wanafunzi wa Udom kufukuzwa kwa niaba ya serikali
Alisema ilipofika jioni wakati wa vikao vya Bunge, Naibu Spika akafanya makosa mawili, moja likiwa kusitisha mjadala uliokuwa unaendelea bungeni wa kujadili makadirio ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji, na la pili ni kuufunga mjadala huo kwa kumwita Naibu Waziri kuja kufanya majumuisho.

Alisema Spika anatakiwa kuwaheshimu wabunge na mawazo yao na taratibu za kuendesha Bunge.
Mbowe alisema uamuzi uliotolewa jana na Naibu Spika, ni wa kituko ambao hajawahi kuuona tangu aanze kuingia bungeni kwa mara ya kwanza.
“Ninaomba kuwaambia Watanzania kuwa Spika aheshimu mawazo ya wabunge, na siyo wakati wote taratibu zinazoundwa zinakuwa ni za haki, kanuni zilizotungwa kwa ajili ya kuzima haki na maslahi ya watu wengi hatutaziheshimu na ni bora watufukuze, hatutafanya utii,” alisema Mbowe.
Katika hatua nyingine, Naibu Spika, alitoa alisema Bulaya na Nassari watafikishwa katika Kamati ya Maadili kwa sababu ya kurusha vitabu na makaratasi kwa askari wa Bunge wakati wakitolewa nje.
WABUNGE SABA WAFUNGIWA
Katika hatua nyingine, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, imewafungia wabunge saba kutokana na utovu wa nidhamu na kufanya vurugu bungeni.

Wabunge hao ni Bulaya na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kuhudhuria vikao vyote vilivyobaki vya mkutano wa Tatu wa Bunge la 11 kuanzia jana Mei 30, 2016 na vikao vyote vya Mkutano wa Nne wa Bunge la 11 kutokana na ukiukaji wa kanuni na kuonyesha dharau kwa Spika na kuchochea vurugu katika kikao cha Januari 27, 2016.
Wabunge Pauline Gekul, Gobless Lema, Zitto Kabwe na Halima Mdee, wamefungiwa kuhudhuria vikao vyote vilivyobaki vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11 kutokana na utovu wa nidhamu na dharau kwa Spika.
Mbunge Heche, amefungiwa kudhuria vikao 10 mfululizo vya Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11 kuanzia jana kutokana na vurugu za Januari 27, 2016, lakini amepewa adhabu ndogo kulinganishwa na wengine kwa kuwa alitoa ushirikiano kwa kamati.
Adhabu zilisomwa bungeni mjini hapa jana jioni na Mwenyekiti wa kamati hiyo, George Mkuchika.
Imeandikwa na Sanula Athanas, Gwama Alipipi na Augusta Njoji.

NIPASHE.