SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema magari na vyombo vya moto vilivyosajiliwa Tanzania Bara,
havitaruhusiwa kutumika Zanzibar mpaka vitakaposajiliwa upya na kupewa namba, kuanzia Julai Mosi, mwaka huu.
Mpango huo umetangazwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohamed, alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2016/2017 katika Baraza la Wawakilishi, mjini hapa juzi.
Alisema hatua hiyo imechukuliwa na serikali kwa madhumuni ya kuweka usawa katika utekelezaji wa sheria na usajili wa vyombo vya moto baina ya pande mbili za Muungano.
Waziri Khalid alisema usajili wa vyombo vya moto, yakiwamo magari, si la Muungano ndiyo maana serikali imeamua kuweka utaratibu mpya kwa magari yanayoingizwa Zanzibar kutoka Tanzania Bara.
“Ili kuleta usawa katika utekelezaji wa sheria na usajili wa vyombo vya moto, kuanzia Julai Mosi, vyombo vya moto vyenye usajili wa Tanzania Bara vitapaswa kusajiliwa upya Zanzibar kama vingine vyote vinavyotoka nje ya nchi,” alisema.
Alisema kwa muda mrefu, vyombo vilivyosajiliwa Zanzibar, isipokuwa vile vya Serikali ya Mapindunzi Zanzibar (SMZ), vimekuwa haviruhusiwi kutembea Tanzania bara zikiwa na namba za usajili za Zanzibar.
Aidha, alisema serikali imefanya mabadiliko kwa magari yanayosafirishwa kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara na tofauti yake ya kodi watalazimika kulipia Zanzibar badala ya Tanzania Bara kama ilivyokuwa awali.
Kwa msingi huo, alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Kanda za Zanzibar, kuanzia Julai Mosi, mwaka huu, itakadiria na kukusanya tofauti yote ya kodi badala ya kazi hiyo kufanyika Tanzania Bara, kabla ya gari kusafirishwa kutoka Zanzibar.
Katika hatua nyingine, SMZ imetangaza rasimi kuwa ada ya ukaguzi wa bidhaa ya asilimia 0.6 ya thamani ya bidhaa pamoja na ada ya uthibitishaji wa bidhaa ya asilimia 10, kuanzia Julai zitaanza kutozwa Zanzibar.
Waziri Khalid alisema baada ya mapato hayo kukusanywa, yatahifadhiwa katika mfuko maalum na kutumika katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani nchini kote, ikiwemo uimarishaji wa Idara ya Ferodha na mpango mkuu wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB).
Alisema Sh. bilioni 6.68 zinatarajiwa kukusanywa kupitia ada hizo kwa bidhaa zinazoingizwa nchini baada ya kuthibitishwa na kufanyiwa ukaguzi wa ubora wake.
NIPASHE.
No comments:
Post a Comment